01 May 2011

Madiwani wa CHADEMA wazua tafrani baraza la madiwani

Na Grace Ndossa 

MADIWANI wanaotokana na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Manispaa ya Kinondoni, jana walizua vurugu na kusababisha Kikao
cha bajeti ya Baraza la Halmashauri hiyo kuvunjika.

Licha ya Madiwani hao kuzua tafrani kubwa huku baadhi yao wakichana nyaraka hiyo,bajeti hiyo ya sh.bilioni 23 ilipitishwa chini ya kifungu cha 17 cha Kanuni za serikali za Mitaa.

Hali hiyo ilitokea katika ukumbi wa mkutano wa Baraza hilo iliyokuwa ikiongozwa na Meya wa Manispaa ya Kinondoni Bw. Yusuf Mwenda na kuhudhuriwa na wabunge wawili ndani ya Wilaya hiyo.

Chanzo cha vurugu hizo ulitakjwa kuwa ni madiwani wa CHADEMA kutaka ahadi zao zitengewe fedha huku vipaumbele vilivyokuwepo vikizidi mapato. Madiwani wa CHADEMA walidai kuwa Ilani ya Chama  Cha Mapinduzi (CCM) nio imetengewa fedha nyingi  huku za kwao zikitengewa fedha kidogo.

Vurugu hizo zilifikia hatua mbaya zaidi baada ya Diwani wa Kata ya Kibamba (CCM) Bw.Issa Mtevu, kutaka kuzipacha na mwenzake wa Kata ya Kunduchi (CHADEMA) Bi. Janeth Ritha.

Baada ya hali Meya Bw. Mweda alitumia kifungu hicho cha 17 kuwahoji wanaoafiki bajeti hiyo ambapo Madiwani wote wa CCM waliikubali hivyo kupitishwa rasmi huku wenzao wakiwazomea.

Baada ya madiwani wa CCm kupitisha bajeti hiyo Meya Mwenda aliahirisha kikao hicho huku akidai madiwani wa CHADEMA wamekiuka taratibu za baraza. Diwani wa Kata ya Ubunge (CHADEMA) Bw.Boniface Jacobo, alichana nyaraka hiyo wakati akiondoka nje ya ukumbi.

Akizungumzia tukio hilo Meya Mwenda alisema madiwani wote waliochana bajeti pamoja na kuzua vurugu watachukuliwa hatua kali za kisheria na Kamati ya Maadili.

Alisema chanzo cha vurugu hizo ni uelewa mdogo wa madiwani hao na kwamba ni wengine hawajitambua kama ni viongozi wanaowakilisha wananchi.

Alisema Kamati ya Maadili ya Baraza hilo litakaa wiki ijayo kujadili vurugu hizo na hatua za kuchukuliwa dhidi ya Madiwani hao walionesha utovu wa nidhamu.

Alisema iwapo walikuwa na mapendekezo ambayo wangetaka yawekwe wangewasilisha hoja ili kama bajeti haitoshi ipewe kipaumbele katika bajeti ijayo. Alisema hata katika Bunge zipo hoja zinazowasilishwana na kukataliwa hivyo si kweli kwamba kila kitu wanachotaka kinafanyika.

Kwa upande wake Mbunge wa Kinondoni (CCM) Bw. Idd Azzan, alisema kitendo hicho ni utovu wa nidhamu na hauwezi kuvumiliwa.

Alionyesha kushangwazwa na madiwani hao kwa maelezo kuwa walikaa kujadili bajeti hiyo kwa muda wa siku tano mfululizo kuangalia jinsi fedha hizo zitakavyotumika katika miradi mbali mbali.

Alisema kama wangekuwa makini wakati wa kujadili namna ya kutekeleza miradi ya maendeleo katika Wilaya hiyo kwenye bajeti wangekataa kabla kikao hicho badala ya kufanya kitendo cha aibu mbele ya jamii.

Alisema madiwani hao wangeomba muda wa ziada kupata ufafanuzi wakati wa mjadala badala ya kufanya kitendo hicho kinachoweza kutafsiriwa kuwa walikuwa na ajenda yao ya siri kujitafutia umaarufu kisiasa.

Katika mwaka wa fedha uliopita Baraza hilo lilipitisha sh. bilioni 14 hivyo kwa bajeti ya sasa ya bilioni 23 ni sawa na ongezeko la bilioni saba.

Hivi karibuni Wabunge wa CHADEMA walilalamikiwa kuzuia vurugu bungeni huku suala la zomea zomea likionekana kuwa la kawaida kwa sasa ndani ya chombo hicho muhimu.

1 comment:

  1. ubabe unaotumiwa na viongozi wa ccm kutokana na uwingi wao ndio chanzo cha vurugu zote!viongozi wa ccm tumieni ubongo kufikiri na si matumbo kabla ya kutoa maamuzi ya kukomoana!!! lakini ipo siku mtalia kilio cha mbwa mwizi!!!!!!!!!!!!!!

    ReplyDelete