*Asema kuwa vyama vyote havifai ni'ovyo'
*Ahoji pia uhalali wa Kamati ya Maadili
*Nape:Vijana tupigane kurejesha uadilifu
Na Rachel Balama
WATANZANIA wametakiwa kubadili fikra kuhusu Katiba mpya na kutambua kuwa sio kama kikombe cha dawa kinachotolewa na
Mchungaji Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Masapila, kinachotibu maradhi yote.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Profesa Issa Shivji, wakati akitoa mada kuhusu nafasi ya Azimo la Arusha katika katiba mpya.
Prof. Shivji, aliyekuwa kwenye kongamano katika ukumbi wa Nkrumah, Chuo Kikuu cha Dar es salaam alisema licha ya kwamba katiba ni mchakato wa kujadili, kuchambua na kujenga misingi imara hauwezi kumaliza kila kitu.
Kuhusu nafasi ya wananchi katika Katiba mpya alisema ni nafasi yao kujadili matatizo mbalimbali yanayowakabili kwa kujitokeza badala ya kuwaachia wanasiasa pekee kazi hiyo.
Alisema mchakato wa katiba mpya ni muhimu kuliko katiba yenyewe hivyo ni vyema wananchi wakashiriki kwa hali na mali kuujadili."Mchakato wa katiba mpya ni muhimu kuliko katiba yenyewe, ni nafasi ya wananchi kutoa matatizo yao ili yaweze kutafutiwa ufumbuzi ni vyema nafasi hiyo ikatumika vizuri," alisema.
Akizungumzia Azimio la Arusha Prof. Shivji alisema utaendelea kuwasumbua wananchi hususan vijana kwa kuwa hakuna kiongozi wala chama chochote cha siasa kinacholikumbuka Azimio.
Alisema kimsingi Azimio la Arusha halikuzungumzia maadili isipokuwa lilikuwa na masharti ya uongozi pamoja na miiko. "Wazo zuri kwa Azimio la Arusha kuingia kwenye katiba kusiwe na ndoto kwa kuwa hayo ni pambambano kutokana na mfumo uliopo,"alisema.
Alisema vyama vya siasa vilivyopo sasa hakuna hata kimoja kinachoweza kusema kina malengo ya kuwanufaisha wananchi. "Vyama vyote vina lengo la kuingia madarakani, katika hilo wanaweza kufanya chochote kitakachowawezesha wao kuingia madarakani,"alisema Prof. Shivji.
Alisema kutokana na hali hiyo hakuna mategemeo ya vyama hivyo kuleta mabadiliko katika mfumo wa manufaa kwa wananchi walio wengi isipokuwa kwa manufaa yao binafsi.
Alisema Azimio la Arusha ilizingatia zaidi mashariti na misingi ya uongozi kwa kuwa maadili yanatokana na familia na si jambo la kufundishwa hivyo haoni sababu ya kuwepo kwa Tume ya Madidili.
Katika hatua nyingine mwanataaluma huyo amewageukia wanafunzi wa vyuo vikuu nchini wanaojiunga na vyama vya siasa na kupewa uongozi si cha kuuenzi azimio. Aliwataka wanafunzi hao kutokubali kununuliwa na vyama kwa kupewa uongozi na kutolea mfano yeye binafsi kuwa kama angekubali angekuwa mwanzilishi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kwa upande wake Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) Bw. Nape Nnauye, alisema Azimio la Arusha ni moja ya kitu cha msingi hivyo mchakato wa katiba mpya ni fursa ya kurudisha uai wa Taifa.
Aliwataka vijana kufunga mikanda kupambana na kurudisha misingi ya Azimio la Arusha kwenye katiba mpya na kuwataka kuwa imara na ma thubutu zaidi kwa kuwa haitakuwa kazi raisi.
Naye Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Bw. Joseph Butiku, ametaka wanafunzi wa UDSM na vyuo vingine nchini kufanya utafiti kubaini ni wapi taifa lilipotoka, lilipo na linapoelekea.
Alisema utafiti huo utasaidia kuleta mabadiliko kwa kuwa nchi inafikia miakam 50 ya uhuru ikiwa na hali isiyoridhisha hivyo katiba mpya iwe chachu ya mabadiliko kifikra na utendaji.
Alisema Azimio la Arusha ina miiko migumu na linafafanua wazi kwamba kama mtu akitaka kuwa kiiongozi hasijishughulishe na mali badala yake awe mtumishi wa wengine hususan wanyonge. Kongamano hilo lililoandaliwa na wanafunzi wa UDSM iliazimia Azimio la Arusha kuingizwa kwenye Katiba Mpya.
No comments:
Post a Comment