15 May 2011

Kibaha wagoma kufanya mtihani rahisi

Na John Gagarini, Kibaha

WANAFUNZI wa kidato cha nne Shule ya Sekondari ya Kibaha wamegoma kufanya mtihani wa Kiswahili wa moko kwa madai kuwa wanaufahamu kwa kuwa
ulishafanyika mwaka 2007.

Wanafunzi hao wakizungumza na waandishi wa habari jana shuleni hapo walisema kuwa wanailaumu Bodi ya Mitihani ya Kanda ya Mashariki kwa kurudia mtihani ambao ulishafanyika miaka minne iliyopita.

Baadhi ya wanafunzi hao akiwemo Jackson Mpika, Jackson John, Mwaita Kapaya na Methew Haidan wamesema kuwa mitihani hiyo haitawasaidia chochote ikiwa ni kipimo cha maandalizi ya mitihani ya taifa inayotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Waliweka bayana kuwa si mara ya kwanza kufanya kitendo hicho cha kurudia mitihani kwa hiyo imekuwa ni mazoea ya bodi hiyo kurudia mitihani ya miaka ya nyuma hali inayosababisha baadhi ya wanafunzi kubweteka kwa kuzoea hali hiyo.

Malalamiko hayo walishatoa pia kuanzia mitihani ya kidato cha pili bila kufanyika marekebisho yoyote, hivyo kuamua kufanya mgomo.

Mwalimu wa somo la Kiswahili katika shule hiyo, Bw. Casto David alikiri kutokea kwa hali hiyo na kusema kuwa walimu wamekuwa hawashirikishwi katika utungaji wa mitihani hususan wa somo hilo tofauti na ilivyokuwa wakifanya katika miaka ya nyuma.

Kidato cha nne katika Kanda ya Mashariki wapo katika mitihani ya moko ambayo ilianza Jumatatu wiki hii na Mei 12 ulikuwa ukifanyika mtihani wa Kiswahili ambao waliugomea wakihitaji ubadilishwe na kurudiwa Julai mwaka huu ili kuwaweka sawa kitaaluma katika mtihani wa Taifa.

No comments:

Post a Comment