26 May 2011

Kazi nguvu kuongoza wasio na ajira-Wasira

Na Raphael Okello, Bunda

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Uhusiano na Uratibu, Bw. Stephen Wasira amesema kuwa ni kazi ngumu kwa serikali yoyote kwa vijana kuongoza nchi
ambayo vijana wake wengi hawana ajira kwa kuwa wao ndio nguvu kazi ya taifa.

Akizungumza na wadau wa maendeleo wilayani Bunda jana katika mkutano maalumu ulioitishwa na Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Bw. Agrey Mwanry na baadaye katika mikutano ya hadhara katika vijiji mbalimbali jimboni humo, Bw. Wasira aliwataka vijana wafanye kazi na kuepuka alichokiita kuwa ni propaganda ya wanasiasa baada ya uchaguzi.

Alisema maisha bora kwa kijana yoyote itakuja tu pale ambapo atajituma kufanyakazi na kwamba hata kama serikali ingeboresha miundombinu yote, bado itakuwa vigumu kupata maendeleo ya kudumu bila vijana kutuma katika kazi.

Bw. Wasira ambaye ni mbunge wa Jimbo la Bunda alisema vijana wengi nchini kwa sasa hawana ajira, hivyo ni rahisi kushawishiwa kujiingiza katika vitendo vya uvunjivu wa amani kwa miamvuli ya kudai maisha bora, hivyo wanahitaji kusaidiwa.

Aliwataka vijana wengi wanaomaliza masomo yao katika vyoo mbalimbali nchini kutumia elimu yao kuboresha maisha yao kwa kuanzisha ujasirimali kutokana na fani aliyoisomea, ili wawe mifano kwa wenzao ambao hawakubahatika kupata elimu ya juu.

“Unajua kama una vijana wengi ambao hawajishughulishi katika uzalishaji mali huku wakitumia muda mwingi kukaa vijiweni, ni rahisi kwao hata wakishawishiwa kuandamana au kufanya jambo lolote bila kuelewa madhara yanayoweza kutokea kutokana na vitendo hivyo,” alisema Bw. Wasira.

Alisema ni jukumu la serikali kuwawezesha vikundi vya vijana kujiajiri ili kuwaepusha na vishawishi mbalimbali kwa kuwa muda wote watakuwa na kazi za kuwaingizia kipato.

Bw. Wasira alisema serikali inajitahidi kugawa na kutumia rasilimali kidogo zilizopo katika kuhakikisha kuwa maendeleo yanapatikana, licha ya changamoto nyingi zilizopo, hivyo vijana wanapaswa kutambua hilo na kujituma zaidi kutumia fursa zilizopo.

Alifafanua kuwa ni vema wakurugenzi wa halmashauri kuweka mipango ya kusaidia vikundi vya vijana katika halmashauri zao kupitia mifuko mbalimbali ikiwa ni pamoja na TASAF, SIDO na fedha kutoka Local Government Fund.

1 comment:

  1. Mbona wewe Mheshimu serikari ilikujari,tatizo ni CCM wewe ni mtu ulitakiwa usiwepo kabisa katika duru hili ila kwa UCCM wenu na UFIDA ndio mnaona haiwezekani

    ReplyDelete