Na Godfrey Ismaely
JESHI la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) limesema kuwa mara baada ya kukamilisha ukusanyaji wa masalia ya mabomu ambayo yalilipuka katika kambi ya
jeshi hilo iliyopo Gongolamboto, jijini Dar es Salaam hivi karibuni hatua za kuyalipua zitaanza leo hadi Juni 21, mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari kutoka katika Kurugenzi ya Habari na Uhusiano Makao Makuu ya Jeshi hilo yaliyopo Upanga ilieleza kuwa zoezi hilo, halitakuwa na madhara kwa wananchi waishio karibu na kambi hiyo pamoja na wale waliopo katika maeneo mengine ya jiji ukiwamo mkoa wa Pwani.
"Kufuatia milipuko ya mabomu Februari 6, 2011 katika kambi ya jeshi iliyopo Gongolamboto, kikosi kazi cha jeshi kilikuwa katika hatua za kuyakusanya masalia, hivyo kikosi kazi hicho kinaingia katika hatua nyingine ya kulipua masalia hayo pamoja na viwashia ambavyo siyo salama kuvisafirisha kwenda mbali na mji," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza.
"Ulipuaji wa masalia hayo utafanyika ndani ya kambi ya jeshi Gongolamboto kuanzia Mei 26 hadi Juni 21, 2011 isipokuwa Jumapili na Jumamosi na zoezi hilo litaanza majira ya saa tano hadi sita mchana," iliongeza sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha jeshi hilo limewaomba wananchi wanaozunguka katika maeneo hayo kutokuwa na wasiwasi wowote huku likiwataka kuendelea kufanya kazi zao kwa madai kwamba milipuko hiyo haitakuwa na madhara yoyote kwao.
"Wananchi wote wa Dar es Salaam na Pwani hususan wanaozunguka katika eneo la Gongolamboto tunawataarifu kuwa mabomu hayo hayatakuwa na madhara kwao hiyo waendelee na shughuli zao," iliongeza sehemu ya taarifa hiyo.
No comments:
Post a Comment