Na Zahoro Mlanzi
KATIKA hali isiyotarajiwa na mashabiki wengi wa soka nchini, kiungo wa mabingwa wapya wa soka Tanzania Bara, timu ya Yanga, Athuman Idd 'Chuji', amesaini
makubaliano ya awali na wapinzani wao wa jadi, Simba kuichezea timu hiyo.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya viongozi wa Yanga kuanza mazungumzo naye pamoja na winga Shamte Ally, baada ya mikataba yao ya awali, kumalizika kwa ajili ya kuitumikia tena timu hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana jijini Dar es Salaam jana, na kuthibitishwa na mmoja wa viongozi wa Kamati ya Utendaji ya timu hiyo bila kupenda jina lake litwaje, alisema Chuji alisaini mkataba juzi saa saba mchana, katika hoteli ya Royal Palm iliyopo katikati ya jiji la Dar es Salaam.
Alisema mkataba huo ni wa awali na wamekubaliana msimu unaokuja kiungo huyo kuvaa jezi za Simba, kama ilivyokuwa hapo awali.
"Unajua haya mambo bado hayajakamilika, ila ni kweli jana (juzi) Mwenyeki wa Kamati ya Usajili, Zakaria Hanspope na Makamu Mwenyekiti, Geofrey Nyange 'Kaburu', walikutana na mchezaji huyo," kilisema chanzo hicho na kuendelea;
"Mkutano huo ulifanyika katika hoteli ya Royal Palm majira ya saa saba mchana na kwamba, walimalizana kila kitu, ila wanachosubiri ni fomu mama za usajili kutoka TFF (Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania)".
Alipotafutwa Kaburu kuzungumzia suala hilo, kupitia simu yake ya kiganjani, iliita zaidi ya mara tatu, bila kupokelewa.
Gazeti hili halikuishia hapo, lilimtafuta Ofisa Habari wa klabu hiyo, Cliffold Ndimbo kuzungumzia suala hilo, ambapo alisema mpaka jana mchana hakuwa na taarifa zozote juu ya mchezaji huyo.
"Mhhh! hizo taarifa bado sijazipata mpaka sasa, kama unavyojua mambo mengi ya usajili, bado yanaendelea, na pia mazungumzo na wachezaji hao, mambo yapo ila tusubiri muda ufike," alisema Ndimbo.
Chuji alijiunga na Yanga misimu sita iliyopita na kuipa mafanikio makubwa, yakiwemo kutwaa ubingwa Ligi Kuu Bara zaidi ya mara tatu, Kombe la Tusker mara mbili na Ngao ya Jamii.
Kabla ya kujiunga na timu hiyo, aliichezea Simba msimu mmoja akitokea Polisi Dodoma.
No comments:
Post a Comment