04 May 2011

CHADEMA ilitumia bil. 1.5/- urais-Mbowe

Na Tumaini Makene

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeweka hadharani gharama za matumizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana, kuwa kilitumia jumla ya
sh. bilioni 1.5, katika nafasi ya mgombea urais, huku kikitoa changamoto kwa chama tawala, CCM, nacho kufanya vivyo hivyo, kwa mujibu wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi.

Chama hicho pia kimetoa angalizo kwa wagombea wa nafasi mbalimbali katika Baraza la Vijana la CHADEMA taifa (BAVICHA), kikiwataka kujiepusha na mchezo wa kampeni chafu kama vile matumizi ya rushwa, kwani hayatavumiliwa 'hata chembe ili uchaguzi uwe huru na haki kwa vitendo'.

Kimesema kuwa fedha hizo za uchaguzi, kiasi cha sh. milioni 1,526,417,674 zilitumika kuanzia Julai mpaka Oktoba mwaka jana, zilitokana na vyanzo mbalimbali vya mapato ambavyo sehemu kubwa ni vya ndani ya nchi, ikiwemo ruzuku ya chama kutoka serikalini na ada za wagombea wa nafasi mbalimbali na wanachama waliojiunga wakati huo.

Chanzo kingine ni mikopo ya huduma na vifaa kutoka kwa marafiki, wanachama na wapenzi wa chama hicho, michango na misaada mbalimbali kutoka kwa watu wa namna hiyo walioko ndani ndani na nje ya nchi, ambapo fedha zote zilitumika kuanzia wakati wa ziara ya kutafuta udhamini wa mgombea urais, Dkt. Willibrod Slaa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana wakati akitoa tamko la maazimio ya vikao viwili vya Kamati Kuu na Baraza Kuu la (CHADEMA), Mwenyekiti wa CHADEMA, Bw. Freeman Mbowe alisema kuwa chama hicho bado kinafanya tathmini ya gharama za wagombea ubunge na udiwani, ili nazo ziwekwe hadharani.

"Waambieni jamaa zetu wa CCM nao wafanye hivi kama wataweza, maana katika ile sheria ya gharama za uchaguzi walijiwekea nafasi kubwa ya kutumia gharama kubwa wakati wa uchaguzi, wakataka mgombea urais atumie sh. bilioni 50, sisi tuna uhakika kuwa wametumia zaidi ya bilioni 50.

"Lakini unapangaje kutumia bilioni 50 kwa mgombea urais pekee katika nchi maskini kama hii. Tumeweza kutumia fedha hizi kwa mgombea wetu wa urais bila fund (fedha) kutoka nje ya nchi, tofauti na propaganda zinazosemwa kuwa tunafadhiliwa na mataifa ya nje, ingawa tulipombana aliyesema, Waziri Simba (Sofia), akasema waandishi wa habari mlimwelewa vibaya," alisema Bw. Mbowe.

Nafasi ya uenyekiti Shinyanga

Bw. Mbowe alisema Kamati Kuu ya CHADEMA, imetengua uamuzi wa Kamati ya Uongozi Mkoa wa Shinyanga, iliyomteua Mbunge wa Maswa Magharibi, Bw. John Shibuda kuwa Kaimu Mwenyekiti wa CHADEMA mkoani humo, kufuatia kifo cha Bw. Shelembi Magadula aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo.

Alisema kuwa CC ya chama hicho ilipima mantiki ya busara ya uongozi wa Mkoa wa Shinyanga kuamua kukaimisha nafasi hiyo kwa kasi ya haraka wakati hata aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo ya mwenyekiti wa mkoa, akiwa hajazikwa, akisema 'kasi hiyo si utamaduni wa CHADEMA'.

"Baada ya kifo cha ndugu yetu na kiongozi wetu Shelembi, ambacho kwa kweli
kilisababishwa na CCM baada ya kumsababishia ugonjwa wa moyo kwa kumhujumu katika matokeo kwani alikuwa ameshaambiwa na mkurugenzi ameshinda ubunge ajiandae kutangazwa, lakini CCM na serikali wakazuia, wenzetu wa Shinyanga waliona busara ya kuziba pengo hilo haraka.

"Walipata busara ya kuziba pengo haraka wakisukumwa na hofu ya kifo na wakati mwingine kuogopa wapinzani wetu CCM wasije wakajipenyeza hapo. Kamati kuu imepima mantiki ya busara hiyo na kuona si sahihi. Hapa ieleweke vyema hatuvutani na uongozi wa mkoa...kuna sehemu kama Iringa na Mbeya nafasi za uenyekiti ziko wazi muda mrefu, kwa nini Shinyanga iwe haraka hivyo?" alihoji.

Juu ya udhalilishaji aliodai wanafanyiwa madiwani wa CHADEMA, akitolea mifano ya halmashauri za Moshi na Mkoa wa Dar es Salaam (Kinondoni), alitoa angalizo kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi kuwa kama hatajirekebisha, watamfukuza kazi na kama serikali itamlinda, watamfungia milango nje kama ambavyo waliwahi kufanya Halmashauri ya Karatu.

Pia alisema vikao vyote viwili vya Kamati Kuu na Baraza Kuu, vimekubaliana na mtindo wa kupeleka ujumbe kwa njia ya kutoka bungeni na maandamano ya amani kudai haki za wananchi na uwajibikaji wa serikali kwa wapiga kura, vikisema kuwa utaratibu huo uendelezwe na utumike kila fursa inapotokea.

"Katika kikao cha Kamati Kuu tumekubaliana tusilale kwa sababu bado
hakijaeleweka...katika uchaguzi wa BAVICHA tusingependa kuona tone wala harufu ya rushwa, hilo hatutavumilia hata chembe, hatutaki uchaguzi wa kudhalilishana, nasi tutawasimamia uchaguzi uwe huru, haki na amani.

Mshahara wa Katibu Mkuu

Akijibu maswali ya waandishi wa habari, Bw. Mbowe alilazimika kutoa ufafanuzi juu ya mshahara na marupurupu ya Katibu Mkuu, Dkt. Willibrod Slaa, kuwa anayopokea sasa ni yenye hadhi ya mbunge, maamuzi yake yalipitishwa na vikao vyote halali vya chama hicho kwa kuzingatia umuhimu wa majukumu yake katika nafasi hiyo kwa sasa.

Akijibu juu ya matumizi ya helkopta inayotumika katika mikutano na operesheni mbalimbali za chama hicho, Bw. Mbowe alisema kuwa imetumia jumla ya gharama ya sh. 292,594,500, kwa ukarabati, matunzo, gharama za rubani na ada za kuirusha na kutua. "Hatulipi gharama za kukodi, maana ni ya mwanachama wetu mwenye uchungu Mzee Ndesamburo."


Tuhuma dhidi ya Ridhiwan

Akijibu maswali kwa upande wake juu ya tishio la kufikishwa mahakamani na Ridhiwan Kikwete kwa kumtuhumu kuwa anatumia nafasi ya baba yake, Rais Jakaya Kikwete kujitajirisha kiasi cha kuwa na utajiri usiolingana na umri wake, Dkt. Slaa alisema 'mwambieni akimbie...atangulie mahakamani haraka'.

"Huko ndiko ukweli utakapojulikana. Unajua CHADEMA tuna uzoefu na hawa watu, propaganda sisi hazitusumbui...tulipowataja mafisadi na ufisadi wao pale Mwembeyanga Septemba 15, 2007, walisema tufute kauli zetu la sivyo watatupeleka mahakamani, tukawaambia watangulie mahakamani, mpaka leo hakuna aliyekwenda.

"Kwenye ile sheria yetu ya PCCB iko wazi kabisa...ndiyo maana kule Tabora nilisema imefikia hatua PCCB ifutwe haina inachokifanya...sheria iko wazi mtu akionekana ana utajiri ambao hauna maelezo kama vile katika majengo mtu huyo anabanwa atoe maelezo, kama ni watumishi wa serikali zipo namna za kuwabana...sasa atangulie mahakamani," alisema Dkt. Slaa.

Ununuzi wa magari

Akijibu juu ya ajenda ya manunuzi wa magari ambayo iliripotiwa na gazeti moja (si Majira) kuwa 'iliwasha' moto katika kikao cha Kamati Kuu, Dkt.
Slaa alisema kuwa lazima tofauti ya mawazo iwepo kila palipo na kikao cha watu wengi, kwani hiyo ndiyo demokrasia, lakini hatimaye uamuzi hupitishwa.

Alisema kuwa magari ambayo chama hicho kinapendekeza yanunuliwe, yamekuwa yakitumiwa na chama hicho kwa muda mrefu, mengine yakiwa bado mapya, tangu uchaguzi mkuu wa mwaka jana, hivyo chama kikaona ni vyema yakanunuliwa ikiwa ni moja ya mikakati ya kujipanga kirasilimali kwa ajili ya kuchukua nchi mwaka uchaguzi wa mwaka 2015.

"Sasa hili jambo linataka kufanywa propaganda, hivi utafikiri magari yamenunuliwa China au wapi sijui...magari haya mengine tumekuwa tukiyatumia ndani ya chama mpaka sasa yanaendelea kuhudumia...kama alivyowaambia mwenyekiti kuwa moja ya vyanzo vyetu ilikuwa ni misaada ya huduma na vifaa.

"Mwaka jana ilifikia mahala tukamwomba mwenyekiti atusaidie magari kwa uwezo wake.

Akanunua magari akijua kuwa yakimaliza kazi ya chama yatarudi katika biashara zake, lakini tumeendelea kuyatumia mpaka leo...hakukuwa na moto wowote katika kikao...mwandishi wala hakutaka kuniuliza na mimi ndiye msemaji mkuu wa chama, ningempatia hata namba za magari hayo," alisema Dkt. Slaa.

Kifo cha Osama bin Laden

Bw. Mbowe alisema pamoja na kuwa kifo chochote si jambo la kufurahia, lakini chama hicho hakikubaliani na ugaidi kama moja ya suluhisho katika kutafuta amani na maridhiano ya kudumu, vivyo hivyo CHADEMA hakiungi mkono suala la nchi moja kutumia mabavu na nguvu za kijeshi kuingilia uhuru na mamlaka ya nchi nyingine ndani ya mipaka yake.

"Osama alikuwa ni controversial (mtata), akiwasilisha hisia za makundi mawili tofauti, kundi moja likiamini ni jasiri mpigania haki kundi jingine likimuona ni gaidi...kama mnavyojua CHADEMA hatu-deal na individuals (watu mmoja mmoja), tuna-deal na issues (hoja).

"Hatuungi mkono ugaidi kwani si njia mwafaka ya kutafuta amani na maridhiano, lakini pia hatuungi mkono matumizi ya nguvu za ziada za kijeshi hata kuingilia sovereignty (uhuru) ya nchi nyingine." 

5 comments:

  1. "CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeweka hadharani gharama za matumizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana, kuwa kilitumia jumla ya
    sh. bilioni 1.5, katika nafasi ya mgombea urais, huku kikitoa changamoto kwa chama tawala, CCM, nacho kufanya vivyo hivyo, kwa mujibu wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi."

    Wewe mpiga Disci hizo zilikuwa fedha zako na usiudanganye umma kwamba ni gharama za chama yaani kwa maneno mengine wewe ni fisadi.
    Mh DJ, elimu na upeo wa mambo ya kimataifa bado ni changa umetoa mawazo zero kwa swala la marehemu Osama.

    ReplyDelete
  2. Tusilete siasa wakati Osama ni mtu hatari. Unategemea nani aende kumzui Osama asiendelee na ugaidi wake? hakuna nchi ya Afrika yeyote wala kiongozi wa afrika mwenye uwezo wa kusikilizwa na nchi za kiarabu, zaidi ya kujipendekeza na kulishwa Harua, kahawa na kupewa vitu vya thamani kama mlivyodanganyika wakati wa ukoloni.

    Kama sie tumeweza kusahau jinsi walivyotutesa wakati wa ukoloni kwa kutu uza utumwani, kupasua wanawake wenye mimba matumbo yao, kuwaingilia wanume kinyume na maumbile na nk. mbona wao hawa samehani

    hata sie tungekuwa na nguvu za uchumi na kijeshi, mwarabu angetukoma.

    we mboye acha hizo!

    ReplyDelete
  3. HIVI MPK LINI TUNAFANYWA MAMBUMBUMBU KUWA WAO NI WEREVU SAANNA KAMPENI YA URAISI ILIKUWA NZITO NA PESA ZILIZOTUMIKA NI NYINGI KULIKO HIZO ZILIZOTAJWA ILA HAPA WANAOGOPA KUELEZA UKWELI MAANA ITABIDI WAELEZEE WALIKOZIPATA NA KUTAKA KUFUTA ILE KAULI YA KUWA WANAFADHILIWA NA NCHI ZA NJE WAMEFICHA BAADHI YA MATUMIZI.KWA MWENYE AKILI TIMAMU KUZUNGUKA NCHI HII NA HELKOPTA PAMOJA NA POSHO ZA HAO ANAOZUNGUKA NAO NA GHARAMA ZA MALAZI HICHO NI KIASI KIDOGO SANA HAWASEMI UKWELI.NA KUHUSU HUYO MBOWE NA SLAA WAKE NI MAFISADI WAMENUNUWA MAGARI MITUMBA WAKAIINGIZA KATIKA KAMPENI SASA ANADAI CHAMA KIYANUNUWE WAKATI NI HELA ZILEZILE ZINAZUNGUKA,HUYO NI MFANYA BIASHARA NA MCHAGA HAWEZI KUFANYA KAZI ISIYO NA TIJA. AMMA KWELI HATA CHONGO UTAIITA KENGEZA KILA KINACHOSEMWA KINAUNGWA MKONO NA WAFUASI WAKE MAANA WENGI NI MAMBUMBUMBU!! NDIO MAANA HATA ZITO ALIPINGA HILO LAKINI
    UDIKTETA WAKALIPITISHA KWA NGUVU HALAFU WANAJIDAI WAKO WAZI DUUHH, KWELI WAJINGA NDIO WADANGANYAO

    ReplyDelete
  4. Hawa ni mafisadi tena wezi wakubwa,hata haiingii akilini Chagga dev& bilicannas co.
    Wanjifanya maamuzi yao ya kisomi na uwazi wkt wanawaburuza wajumbe watakavyo,hizo gharama ni chache si kweli, na pia hizo gari alishazitumia akajifanya anasaidia zifanyie kampeni sasa anaona ruzuku imeongezeka anaziuza wakati ni mitumba zimeshachoka ni aibu kubwa lakini wapo kwa maslahi yao si vinginevyo.Fikiria hata wakati kabla ya kampeni magazeti yaliandika makubaliano ya Slaa na CDM kuwa akikosa Uraisi basi alipwe mshahara kama wa mbunge wakakanusha,sasa leo ni yapi tena? Na ikumbukwe wakati alipokuwa bungeni akipiga kelele pesa wanazolipwa ni nyingi zipunguzwe? Sasa mbona zake hadai zipunguzwe, mkuki kwa nguruwe kwa binadamu mchungu?

    ReplyDelete
  5. hawa watu wanatuchezea hawasomi nyakati viongozi kuweni makini hakuna jambo lisilo na mwisho

    ReplyDelete