17 May 2011

CHADEMA Geita yabeza propaganda za CCM

Na Faida Muyomba, Geita
 
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilayani Geita kimewataka viongozi (CCM) kutotumia fedha za wananchi kwa kueneza propaganda wanazodai
za uongo majukwaani, badala yake wafanye kazi ya kuwaletea maendeleo wananchi.
 
Pia chama hicho kimesema mkakati wa CCM wa kujivua gamba, hauna tija kwa Watanzania bali hizo ni dalili za kushindwa kuwashughulikia mafisadi ndani ya chama hicho.
 
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Mwenezi wa chama hicho wilayani Geita, Bw. Ignas Karashani, wakati akizungumza na umati wa watu waliohudhuria mkutano wa hadhara, katika mji mdogo wa Katoro juzi.
 
Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama hicho ngazi ya wilaya, pamoja na madiwani, ukiwa na lengo la kuwaeleza wananchi namna wanavyopambana na ufisadi unaodaiwa kufanywa na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita.
 
Alisema, "CHADEMA tunawataka CCM na Nape wao waache kuifuatafuata Chadema kwa kutunga uongo majukwaani bali wafanye shughuli zinazowaletea maendeleo wananchi."
 
Aliongeza, anazunguka majukwaani eti wanadai wamejivua gamba, sote tunajua kuwa nyoka hauliwi kwa kuvuliwa gamba bali kupigwa kichwa na kufa, hivyo CCM wamedhihirisha kushindwa kuongoza nchi hii wanatakiwa kujiondoa wenyewe madarakani."
 
Katibu huyo alisema, Watanzania wamechoshwa na ugumu wa maisha wanaopambana nao kila siku, hivyo viongozi wa CCM wanatakiwa kutafuta njia za kuwakomboa katika janga hilo na si kukalia kujibu mapigo  yanayotolewa na viongozi wa CHADEMA.
 
Chama hicho kina madiwani wanane katika Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, ambapo hivi karibuni walisusia upitishaji wa bajeti kwa madai ya kutopewa muda wa kupitia kabrasha kabla ya kikao.

4 comments:

  1. Karashani hivi anaewafuata wenzake ni nani? CCM au CDM?Nyie kila kukicha ni kuzusha uongo na kuwalaghai watu tukijibu tunawafata nyinyi ndio muache kupoteza muda wa watu wakuzalisha mali kila kukicha ni mikutano na maandamano mnakula posho zenu wao mnawaacha pakavu kwenu sawa kwetu si sawa. ninasikitika kusema kuwa cdm kuongoza nchi hii kwa sasa baaaaddo,labda mubadilike

    ReplyDelete
  2. mtoa maoni wa kwanza, mbona umeshindwa kutaja uongo huo unaosemwa na cdm. maandamano hayo ndiyo yaliyoleta viguvugu la katiba na ndiyo yaliyozuia bil.98 za dowans zisilipwe na ndiyo yanayowatoa usingizini mawaziri kutoka kwenye maofisi DSM kwenda kijijini kusikiliza kero za wananchi wao.kuhusu CDM kuongoza nchi hilo ni swala la wananchi kuamua na mimi nikiwa kama raia wa Tanzania ningelipenda kuona mabadiliko kwani tumechoka kuongozwa na watu walewale wanaotoa excuse chungu nzima za kwanini hatuna umeme wala maji miaka 50 baada ya uhuru.

    ReplyDelete
  3. tatizo la watanzania ambao hawaelewi kabisa nini chadema wanafanya ila kwa ujinga wao wa fikira watabaki kuwa tanzania yenye jamii mskini zaidi duniani lakini ni tajiri wa raslimali.Soma historia ya Singapore utaona walivyoendelea na huku tunawazidi mbali natural resources.mlowezi aliyewafanya kuwa mazuzu aliwamaliza kabisa.shabikieni tu ccm na umaskini utazidi kuwachapa hadi mwisho sisi wengine hatuna hamu hata yakusikiliza mikutano ya ccm.

    ReplyDelete
  4. Yaani humu kila nikisoma maoni naona kuna watu mashabiki wa ccm au chadema. Au hivyo vyama vimewapa hao watu laptops na kazi yao ni matusi na kuwachanganya watu kwenye hii mitandao, mie naona hiyo katiba mpya iwe na sehemu ya viongozi wanaojitegemea. Kiongozi achaguliwe kwa uwezo wake na manufaa ya Taifa sio lazima chama. Mataifa mengine yanafanya hivyo. Chadema na ccm ni wale wale watoto wa akina Mbowe, Kawawa, nk. tuinataji mabadiliko. Vyama vyote haviwajali watu wa chini, kila mtu anakimbilia madarakani tu. Tumechoka.

    ReplyDelete