27 May 2011

CDA yakabwa koo kamati ya Bunge

Na Gladness Mboma 

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, uongozi  wa Mamalaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) imeshindwa kutetea hoja zilizoko ndani ya nyaraka za
taarifa ya maendeleo ya mamlaka hiyo hatua ilisababisha Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma kuutoa nje uongozi huo.

Hatua ya kutolewa nje inatokana na uongozi wa mamlaka hiyo kushindwa kujibu maswali yaliyokuwa yakiulizwa na kamati hiyo juu ya nyaraka zao.

Hali hiyo ilijitokeza Dar es Salaam jana mbele ya kamati hiyo ambapo Mkurugenzi Mkuu wa CDA, Bw. Martine Kitila aliieleza Kamati kwamba katika kipindi cha nyuma mamlaka hiyo ilikuwa inalegalega na baada ya kubadilishwa uongozi wamekuwa na mabadiliko makubwa katika utendaji wa kazi.

Bw. Kitila alisema pamoja na mabadiliko hayo kuna tatizo la Serikali kushindwa kutoa fedha za kutosha kwa ajili ya uendeshaji, ambapo mwaka uliopita ilitoa sh. bilioni 1.6 na mwaka huu imetoa sh. bilioni 1.8.

Baada ya kutoa taarifa fupi ya CDA, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Bw. Deo Filikunjombe  alimhoji Bw. Kitila kama amepitia vema taarifa hiyo kwa kuwa hesabu zake hazikuwekwa sahihi, hali ambayo iliifanya kamati kuhoji maswali ambayo yalionesha kuichanganya CDA.

"Pamoja na taarifa yako nzuri, lakini sisi kamati tunanatambua fika hakuna maendeleo CDA, kwani hata mapato yanashuka kutoka sh. bilioni 4.5 hadi kufikia sh. milioni 18, je, Serikali inaweza kuhamia Dodoma kwa hali hii kweli,"alihoji.

Bw. Filikunjombe alisema kuwa kuna taarifa kwamba baadhi ya watumishi wa CDA wanakodisha minara ya Vodacom na fedha haziwasilishwi CDA, hivyo akamweleza wazi Mwakilishi wa  Mwenyekiti wa Bodi, Bw. Charles Palangyo kuwa katika uongozi wake bado haujakaa sawa sawa.

Kutokana na taarifa hizo za kujikanyaga wameutaka uongozi huo kukaa chini na kuangalia wanakuzaje kipato katika upimaji na ugawaji wa viwanja na kusisitiza kwamba suala la serikali kuhamia Dodoma ni lazima liwe la vitendo na si maneno.

"Ninyi mnataka serikali ihamie Dodoma wakati hesabu zenu tumezitazama zinatetereka, mwaka juzi mlipewa sh. bilioni 2 na mwaka huu wa fedha mmepewa tena sh. bilioni mbili, sababu za kwamba hampewi mtaji ndio maana mnashuka si kweli mahesabu yenu ya ndani yanashuka,"alisema.

Bw. Filikunjombe ameutaka uongozi huo kuhakikisha wanatambua kiasi cha pango wanachokusanya,ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za kuonesha wanapodai ili kamati hiyo iweze kuwasaidia.

Pia aliutaka uongozi huo kuhakikisha naangalia vyanzo vipya vya mapato ambavyo wanaweza kuingiza katika shirika na kusisitiza kwamba hesabu walizokwenda nazo mbele ya kamati hiyo si sahihi, kwani wana hati zaidi ya 14 lakini hazionekani zilipo.

Bw. Filikunjombe ameomba Mwakilishi wa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Fedha za Serikali, Bw. Johanes Kisiri kufanya uchunguzi wa mapato ya minara ya simu, uthibitisho wa taarifa za Mkaguzi kutokana na kuwepo kwa taarifa za kukinzana.

2 comments:

  1. haaa haaaa,i just knew something like this will happen one day,blaa blaaa blaa but no utendaji

    ReplyDelete
  2. Wananchi nao wana gamba la kujivua. Ni hili la Dodoma kama Makao Makuu ya nchi. Serikali ya Chama Tawala (CCM )imengàngània Dodoma kama Makao Makuu tangia uamuzi wao mbovu uliochukuliwa na mtu mmoja,Rais Nyerere. Sasa mzigo (au Ufisadi wa Kisiasa) umebebwa na Wananchi.Waheshimiwa na Watawala wetu wanakula chao kwa kuwa na Serikali mahali pawili.Wanalipana Posho wakiwa Dodoma!!Watanzania tu wapole ( Wajinga ? ) sana jamani!!

    ReplyDelete