18 May 2011

Mzimu jengo la magari bandarini waitafuna wizara

Na Edmund Mihale

SIKU chache baada Wizara ya Uchukuzi kutoa taarifa zilizodaiwa kuchakachuliwa mbele ya Rais Jakaya Kikwete alipotembelea Bandari ya Dar es Salaam kuhusu mradi wa
kupokelea na kuhifadhi magari bandarini, vyanzo kutoka ndani ya wizara hiyo vinasema baadhi ya vigogo wanajipanga kukwepa aibu hiyo kwa kuitupia lawama Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kwa madai kuwa mradi huo ni ufisadi.

Machi mwaka huu, Rais Kikwete alipofanya ziara ya kukagua shughuli mbalimbali za bandarini hiyo, alielezwa kwamba mradi huo ambao umesitishwa, ulilenga kujenga jengo la kuuzia magari (bonded werehouse) kinyume na ukweli halisi ambapo jengo hilo lilikuwa maalumu kwa ajili ya kupokelea na kuhifadhi magari bandarini hapo (multi storey car park) ili kuondoa msongamano.

Vyanzo vya kuaminika kutoka ndani ya wizara hiyo vimeeleza kwamba miaka 2008/09 bandari ilikabiliwa na ongezeko kubwa la shehena ya magari jambo lililosababisha nafasi ya kuyapokea kuwa finyu na kusababisha yawekwe kwenye maeneo ya shehena zingine.

Baada ya malalamiko mengi kutoka kwa wadau juu ya hali hiyo, TPA  ilianza mchakato wa kujenga jengo hilo kwa kushirikiana na sekta binafsi kwenye eneo la pembezoni mwa mpaka wa bandari na Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka jijini Dar es Salaam (DAWASCO) ambalo halingeweza kutumika kwa mahitaji mengine zaidi ya hayo.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa TPA ilitangaza tenda kwa mujibu wa sheria na kampuni mbalimbali za ndani na nje ya nchi zilijitokeza.

Kampuni ya EMK Group ya Mombasa Kenya ndiyo iliyoshinda. Walieleza kuwa wangejenga jengo la kuhifadhi magari yapatayo 8,000 kwa mara moja ambalo lingegharimu sh. bilioni 44 na TPA isingegharamia chochote kwenye mradi huo.

Vyanzo vimedai kwamba kwa maslahi binafsi, baadhi ya vigogo wizarani hapo wanaopiga vita mradi huo, wameanza mkakati kueneza propaganda kuwa kuna ufisadi wa sh. bilioni 40 kwenye mradi huo.

Vyanzo hivyo vimedokeza mkakati huo unaibuka baada ya kuwepo taarifa kwamba Kampuni ya EMK Group iliyoshinda tenda hiyo imekusudia kuishitaki serikali kupitia wizara hiyo na kudai fidia ya mamilioni ya fedha.

Majira lilipomtafuta Katibu Mkuu wa Wizara Uchukuzi, Bw. Omari Chambo kuzungumzia suala hilo, alimjibu kuwa yuko nje ya mji na kumtaka mwandishi kufika ofisini kwake leo saa tatu asubuhi.

No comments:

Post a Comment