29 April 2011

Yanga sasa kusajili watatu pekee

Na Elizabeth Mayemba

UONGOZI wa Klabu ya Yanga, umepanga kusajili wachezaji watatu pekee wa kimataifa kutoka nchi za Uganda na Ghana.Katika wachezaji hao mmoja atatoka Ghana na
wengine wawili wanatokea nchini Uganda.

Hata hivyo tayari wachezaji mbalimbali kutoka nchini Zambia, Ivory Coast, Nigeria, Cameroon na Ghana wameanza kutuma maombi katika klabu hiyo, kutaka kufanyiwa majaribio.

Akizungumza Dar es Salaam jana mmoja wa viongozi wa Yanga, ambaye hakutaka kuandikwa jina lake gazetini kwa madai kuwa si msemaji wa mambo ya usajili, alisema uongozi wa klabu hiyo umepanga kusajili wachezaji watatu pekee wa kimataifa kwa kuwa kwa sasa wana wawili.

"Nafasi zilizobaki ni za wachezaji watatu tu na tumelenga kusajili Waganda wawili na Mghana mmoja, ili kukamilisha idadi ya wachezaji watano wa kimataifa," alisema kiongozi huyo.

Alisema wachezaji waliokuwepo awali katika timu hiyo, kipa namba mbili Mserbia Ivan Knezevic na Waghana wawili Isaack Boakye na Ernest Boakye uongozi hauna mpango wa kuwaongezea mikataba mipya.

Kiongozi huyo lisema kwa sasa klabu hiyo ina wachezaji wawili wa kimataifa, kipa namba moja Yaw Berko na mshambuliaji kutoka Zambia, Davies Mwape.

Alisema kocha Sam Timbe, atakapokuja nchini ndiye atakayekamilisha taratibu zote za usajili, baada ya Kamati ya Usajili ya klabu hiyo kumaliza mchakato wake.

No comments:

Post a Comment