Na Addolph Bruno
KOCHA Mkuu wa timu ya taifa ya vijana 'Vijana Stars' Jamhuri Kihwelu 'Julio' amewaomba mashabiki wa soka nchini kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu hiyo, itakapocheza
na Uganda kesho katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Vijana Stars itamenyana na Uganda 'The Cobs' mchezo wa marudiano wa kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika 'All African Games', baada ya mchezo wa awali kufungwa mabao 2-1 ugenini.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Julio alisema kikosi chake kinaendelea vyema na maandalizi pamoja na kufanyia kazi upungufu uliojitokeza katika mechi ya awali.
Alisema ana uhakika wa kulipa kisasi kwa The Cobs, kutokana kugundua mbinu zao uwanjani baada ya kufanya mazoezo mazuri.
"Kwanza namshukuru Mungu na pia nawashukuru wachezaji wangu kwa kunielewa katika kipindi hiki cha maandalizi, kutokana na ari waliyoionesha tutashinda kwa sababu tunawafahamu wapinzani wetu na tunaowaomba mashabiki waje kwa wingi uwanjani," alisema Julio.
Alisema kutokana na maandalizi hayo watahakikisha wanaibuka na ushindi, lakini kazi itakua nyepesi kwao kama mashabiki watafurika kwa wingi uwanjani kesho na kuwashangilia kwa nguvu.
Naye Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema jana kuwa Uganda imewasili nchini jana saa 10.30 jioni, ikiwa chini ya Ofisa wa Shirikisho la Vyama vya Soka Uganda (FUFA), Sam Lwere.
Alisema mchezo huo utachezeshwa na waamuzi raia wa Burundi, Athanase Niyongabo, Jean Itakizimana, Felix Bazubwabo na mwamuzi wa akiba Ramadhani Ibada pamoja na Kamishna, Gspard Kaipuke ambao wamewasili jijini jana saa 11 jioni.
No comments:
Post a Comment