29 April 2011

Kujivua gamba kwa CCM hakuondoi uchakavu wake- Mbowe

Na Suleiman Abeid, Shinyanga

WATANZANIA wameshauriwa kutobabaishwa na mabadiliko yanayofanywa na Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwa  utaratibu wa viongozi wake
kujivua ‘gamba’ hauondoi uchakavu wa chama hicho.

Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. Freeman Mbowe alipokuwa akitoa salaam za pole kwa wakazi wa Mkoa wa Shinyanga kutokana na kifo cha Mwenyekiti wa Mkoa wa Chama hicho, Marehemu Philipo Shelembi kilichotokea mwishoni mwa wiki iliyopita.

Bw. Mbowe alisema kitendo kinachofanywa hivi sasa na CCM kwa kuwavua magamba viongozi wake wanaotuhumiwa kwa vitendo vya ufisadi hakiwezi kuwasaidia lolote Watanzania kwa vile wanaovuliwa ‘gamba’ hawafikishi katika vyombo vya dola kuadhibiwa.

Alisema kwa kadri siku zinavyokwenda ndivyo chama hicho kinavyozidi kupoteza umaarufu wake huku kikionesha wazi kuzeeka na hivyo hakistahili kupewa tena nafasi ya kuongoza nchi.

Hata hivyo alisema moja ya sababu zilizosababisha viongozi wa CCM kuanza kuchukua hatua za kuvuana magamba inatokana na maandamano ya amani yaliyoendeshwa na CHADEMA katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa hivi karibuni na kuwafanya viongozi hao wa CCM kushtuka usingizini.

“Mwanzoni tulipotangaza nia yetu ya kufanya maandamano ya amani na mikutano ya hadhara kwa nchi nzima, hawa watani wetu walitubeza na kudai maandamano hayo yangesababisha uvunjifu wa amani nchini, lakini baada ya kuona maandamano yamefanyika na hakuna amani iliyovunjika wakata hayari.

“Tuliandamana kwa amani na kulaani vitendo kadhaa viovu vilivyokuwa vikifanywa na viongozi mafisadi ndani ya CCM ikiwemo suala la kupinga malipo kwa Kampuni Bandia ya DOWANS na ugumu wa maisha, wananchi wakatuelewa, na ndipo sasa CCM ikaona haina ujanja bali ije na gea ya kuvuana gamba,” alisema Bw. Mbowe.

Hata hivyo alisema suala la kujivua gamba siyo ufumbuzi wa matatizo ya Watanzania bali kinachohitajiwa ni vitendo kuona kero mbalimbali sasa zinapatiwa ufumbuzi na kuwa na maisha bora.

Pia alisema Watanzania wanachohitaji kuona ni serikali ikomeshe vitendo vyote vya ufisadi miongoni mwa watendaji wake pamoja na kuwafikisha katika vyombo vya dola wale wote wanaotuhumiwa kwa vitendo ya ufisadi ili haki kutendeka na kwamba CHADEMA itaendelea kufanya maandamano ya amani bila kumuogopa mtu.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi  (CHADEMA),  Bw. John Shibuda ambaye pia hivi sasa ni Kaimu Mwenyekiti wa CHADEMA mkoani Shinyanga alisema utamu wa kuku huonekana katika uchanga wake na siyo uzeeni na kwamba CCM hivi sasa hawana utamu wowote kwa Watanzania.

Alisema ni vyema hivi sasa wakati CCM wakivuana magamba wakachukua tahadhari kubwa kwani kuna kila dalili wakajikuta wakipata ulemavu wa ngozi baada ya kujivua gamba kama walivyokusudia.

“Ndugu zangu wana Shinyanga, pamoja na kwamba leo hii tuna msiba wa kuondokewa na kipenzi chetu, aliyekuwa mpiganaji wa haki za wanyonge, Marehemu Shelembi, lakini ni budi pia tukaelezana ukweli kuwa hawa wenzetu CCM sasa wamechoka, wamezeeka inabidi waondoke.

“Wakati nikiwa ndani ya chama hicho, nilimweleza Rais Jakaya Kikwete, huyu ni rafiki yangu kipenzi kuwa awe makini vinginevyo CCM itamfia mikononi mwake wakati wowote kutokana na hali ya mambo ilivyokuwa ikienda, hakunielewa, lakini sasa kuna kila dalili ya kusambaratika kwa chama hicho.

“Kujivua gamba kunakoendela hivi sasa kuna hatari wakajikuta wanapata ugonjwa wa ngozi ambao ni hatari zaidi, mimi ninawaonya watahadhari wasigeuke vinu vya kukoboa na kusaga malighafi za uongo, watu hawatawaelewa, utamu wa kuku huonekana katika uchanga wake na siyo uzeeni,” alisema  Bw. Shibuda.

3 comments:

  1. mlienda kwenye msiba auuuuuuuuuuuuuu?

    ReplyDelete
  2. tatzo la ccm n kwamba magamba yanavua magamba.kikwete n gamba kuu kuu linahitaj kuvuliwa il ccm ipone

    ReplyDelete
  3. kikwete n balaa na janga la ccm na taifa kwa ujumla.ole wetu watanzania.chadema endeleen kutusemea wanyonge

    ReplyDelete