06 April 2011

Watoto 500 Tamasha la kuadhimisha Siku ya Malaria

Na Zahoro Mlanzi

WATOTO zaidi ya 500 wa jijini Arusha, wanatarajiwa kushiriki katika tamasha la mpira wa miguu la kuadhimisha siku ya Malaria duniani litakalofanyika kesho
kwenye Uwanja wa Sheikh Amr Abeid, jijini humo.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Mradi wa Chuo Kikuu cha Johns Hopkins, Furaha Kabuye alisema kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa soka kama Benki ya NMB na Kiwanda cha A to Z, wameamua kuendesha kliniki ya watoto itakayohusisha wanafunzi wa shule za msingi tu.

Alisema wanafunzi hao watashiriki mchezo huo kwa nyakati tofauti, ikiwa na lengo la kuadhimisha siku ya ugonjwa huo duniani ambao umekuwa ukiuwa watu wengi kwa kipindi kifupi.

"Kilele cha maadhimisho hayo ni Aprili 25, mwaka huu ambapo barani Afrika mtoto mmoja hupoteza maisha kila baada ya sekunde 30 ambapo pia husababisha umasikini kwa jamii kutokana na kuharibu nguvu kazi katika jamii," alisema Kabuye.

Alizitaja shule zitakazoshiriki tamasha hilo ni Sanawari, Mwangaza, Daraja, Meru, Levolosi, Engosengu, Unga na Makumbusho ambapo michezo hiyo itakuwa chini ya Kocha Mkuu wa timu ya Taifa 'Taifa Stars', Jan Poulsen.

Naye Mkurugenzi wa Ufundi wa shirikisho hilo, Sunday Kayuni alisema alikishukuru chuo hicho na kwamba watatumia nafasi hiyo kuhakikisha wanaandaa utaratibu kwa wanafunzi hao kuendelezwa.

Alisema watawaalika makocha mbalimbali wa jiji la Arusha kwenda kuangalia vipaji vya wanafunzi hao na kwamba wanafunzi watakaoshiriki watapatiwa vyeti na vyandarua kila mmoja.

No comments:

Post a Comment