Na Tumaini Maduhu
OFISA Utamaduni Manispaa ya Ilala, Shani Kitongo ameiomba Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo kuisaidia wilaya hiyo kifedha ili iweze kuibua vipaji
katika Manispaa hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana juu ya changamoto zinazoikabili Manispaa hiyo, Shani alisema wilaya hiyo imeshindwa kutimiza malengo yake katika kuhakikisha inaibua vipaji na kukuza michezo kutokana na ufinyu wa bajeti waliyonayo.
Alisema ili wilaya hiyo iweze kufika mbele na kupiga hatua, Serikali na wadau mbalimbali wa michezo nchini wanatakiwa waiunge mkono katika kuichangia kwa mawazo na fedha ili iweze kupiga hatua.
``Mimi mwenyewe, Ofisa utamaduni sina gari wala bajeti yoyote ya kwenda kuwatembelea wadau wangu, bali ninalazimika kutumia mguu wangu kwa kuwa nina mapenzi na Watanzania wenzangu hususani katika kuhakikisha tunainua na kuibua vipaji vya michezo.
Katika hatua nyingine, Kitongo alitoa mwito kwa wasanii kutoa taarifa pale wanapopata mialiko ya kwenda sehemu mbalimbali nchini ili pale watakapopata matatizo iwe rahisi katika kuyatatua.
``Sisi wenyewe, wasanii ni mashahidi tumejionea wasanii wanapopata matatizo hata huko walipo inakuwa shida kuwasaidia kutokana na kutokufuata taratibu maalumu zakusafiria,`` alisema Kitongo.
No comments:
Post a Comment