Grace Ndossa na Agnes Mwaijega
VIONGOZI wa vyama vya siasa wametakiwa kuacha malumbano na badala yake watumie busara zao kuelimisha wananchi kuhusu mchakato mzima wa
kuundwa kwa katiba mpya.
Kauli hiyo ilitolewa Dar es salaam jana na Jaji Joseph Warioba alipokuwa akizungumza kwenye mkutano uliondaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) wa kujadili mchakato mzima wa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kuundwa kwa katiba mpya.
Alisema kuwa viongozi wanatakiwa kutumia busara zao katika kuelimisha wananchi kuusu katiba iliyopo na namna ya kuunda katiba mpya.
"Viongozi wanatakiwa kuacha malumbano ya kisiasa na kuelimisha wananchi waweze kutoa maoni yao kuhusu uundwaji wa katiba mpya inayotakiwa na kumtetea mtu wa chini," alisema Warioba.
Pia alisema serikali ina wajibu wa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu katiba ya sasa pamoja na msingi wa kuundwa kwa katiba mpya.
Alisisitiza kuwa kifungu cha 2 9,19,28 vinatakiwa kufanyiwa maboresho ya juu ili kuwapa wananchi uwezo wa kushiriki katika kutoa maoni yao pamoja na kukosoa.
Naye Rais wa Chama cha Wanasheria Tanzania (TLS) Bw. Francis Stolla alisema kuwa serikali inatakiwa kuzingatia mambo matatu ili kufanikisha mchakato wa kupata katiba mpya utakaokidhi mahitaji ya wananchi.
Alitaka elimu itolewe kwa wananchi juu ya katiba na sheria itakayowekwa ya kuundwa kwa katiba isiwekewe kinga pamoja na wananchi kuelimishwa namna ya kuundwa kwa katiba mpya.
No comments:
Post a Comment