17 April 2011

Babu wa Loliondo ayavuruga mapato ya Halmashauri Bunda

Na Raphael Okello,Bunda

HALMASHAURI ya Wilaya ya Bunda mkoani Mara imepoteza mapato ya makusanyo yanatokanayo na maegesho ya magari kwa asilimia 20 muda mfupi baada ya
serikali kuchagua mji wa Bunda kuwa kituo cha kutoa vibali kwa wagonjwa wanaoenda Loliondo kutoka Kanda ya Ziwa na nchi jirani.

Hayo yalielezwa katika baraza la madiwani ya halmashauri hiyo jana kuwa tangu serikali wilayani Bunda kuchagua eneo la maegesho ya magari ya kituo hicho sasa hawawezi kukusanya mapato kwa kuwa magari
yanaegeshwa kiholela.

Mwenyekiti wa Halmashuri ya Wilaya ya Bunda Bw. Joseph Marimbe aliliambia baraza hilo kuwa suala la ukusanyaji wa mapato wa halmashauri katika vyanzo vyake ni la kisheria hivyo wamiliki wa magari yaendayo Loliondo kupitia kituo cha Bunda ni sharti watozw ushuru.

“Suala la ushuru ni suala la lazima, kwa sababu hata huko Loliondo wanatozwa ushuru….hii inawezesha pia kuboresha huduma muhimu kwa wasafiri hao katika kituo hicho,”alifafanua Bw. Marimbe.

Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Bunda katika baraza hilo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Bunda Bw.Severine Lalika alisema agizo la kituo hicho kutoa vibali kwa wagonjwa wa Loliondo kutoka kanda ya ziwa ilitoka serikali kuu.

Alisema suala la ukusanyaji wa ushuru kwa magari yanayofika kituoni hapo itajadiliwa katika kamati ya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mara ili kuona uwezekano wa wasafiri hao
kutozwa ushuru.

Kutokana na kauli hiyo,madiwani wa halmashauri hiyo kwa kauli moja ilimtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Bw. Cyprian Oyier awasiliane na mkuu wa wilaya hiyo ili magari hayo ya Loliondo yanayosajiliwa kituoni hapo  watoe ushuru  ili kuepuka mapato ya halmashauri hiyo kushuka zaidi jambo ambalo liliungwa mkono na mkurugenzi huyo.

Akiunga mkono Bw. Oyier alisisitiza kuwa kwa mwaka wa fedha 2010/2011 makusanyo ya halmashauri yake imepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na sababu mbalimbali na kwamba kwa mwaka huo TAMISEMI ilipeleka katika halmashauri hiyo asilimia 25 tu ya ruzuku ya mwaka mzima jambo lililozorotesha shughuli nyingi katika halmashauri hiyo.

Aliongeza changamoto nyingine ni kuchelewesha au kutopata kabisa fedha kutoka hazina, TAMISEMI na kwa wafadhili na kwamba pamoja na ufuatiaji hakuna ufafanuzi unaotolewa na serikali.

No comments:

Post a Comment