29 April 2011

Wanafunzi bingwa kitaifa wazungumza

Na Tumaini Makene

KIJANA Muhagachi Peter Chacha ambaye ameongoza kwa kushika nafasi ya kwanza kati ya watahiniwa 10 bora waliohitimu Kidato cha Sita Februari, mwaka huu, ameeleza
kufurahishwa na matokeo hayo, akiweka wazi kuwa kwaq juhudi alizofanya angeumia sana kama isingekuwa hivyo.

Kijana huyo anatokea katika familia ya kawaida katika eneo la Stakishari, Ukonga Dar es Salaam, ambako baba yake anategemea ng'ombe wawili wa maziwa kwa kipato cha kuendesha familia yake, ikiwamo kumsomesha kijana huyo.

Akizungumza na Majira jana, kijana Chacha ambaye ana umri wa miaka 21 sasa, alisema kuwa hali duni katika familia yao, ilikuwa ni mojawapo ya sababu iliyomfanya asome kwa bidii, akiwa na malengo ya kusomea fani ya uhandisi, katika vyuo vikubwa duniani kama vile Havard cha Marekani.

Akiwa mtoto wa pili kati ya watoto wanne wa familia ya Bw. Peter Chacha ambaye ni askari magereza mstaafu, alisema kuwa angeumia roho iwapo matokeo yangekuja kinyume na matarajio yake, kutokana na jitihada alizokuwa amewekeza shuleni Kidato cha Tano na Sita, Shule ya Sekondari Kibaha, akisoma mchepuo wa sayansi, masomo ya Fizikia, Kemia na Hesabu (PCM).

"Kwa kweli nimeyapokea matokeo haya kwa furaha sana. Ningekufa moyo kama nisingefaulu. Malengo yangu ni kusomea mambo ya Telecommunication Engineering kwa sababu ina soko kubwa, unaweza kufanya kazi mahala popote duniani. Kwa kweli mazingira ya shule niliyosoma, Kibaha Sekondari, yamenisaidia, kama mnaweza kufika ni moja ya shule nzuri. Pia ushirikiano wa wanafunzi wenzangu.

"Nilikazana sana kusoma, maana nilijua natoka familia duni, hivyo sikuwa na kitu cha kurithi. Wakati watoto wa matajiri walipokuwa wakicheza na laptop (kompyuta ndogo), baadhi yetu tulikuwa prepo (kujiandaa darasani). Nataka siku moja niwe mvumbuzi, nigundue kitu changu mwenyewe, kama vile yule bwana aliyegundua facebook, nasikia anasoma Havard yule, pia nina ndoto za kusoma chuo kikubwa duniani kama vile Havard.

"Nawasihi wanafunzi wengine wasikate tamaa, hata kama wakati mwingine wanakwenda shule bila kuwa na pocket money, wanapaswa kukaza mwendo. Uvivu wa walimu na baadhi ya wanafunzi wasiokuwa na ushirikiano vilikuwa ni vitu vilivyokuwa vinanikwaza. Hasa walimu wale ambao wanatumia muda wa vipindi kufanya mambo mengine, hivyo wanaharibia wanafunzi wanaowategemea," alisema Chacha.

Baba yake kijana huyo, Bw. Chacha ambaye mbali ya kufuga ng'ombe hao wawili wa maziwa kwa kipato chake, anafanya kazi ya siasa ya kujitolea akiwa Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wilayani Ilala, alisema kuwa alipata furaha na faraja kubwa aliposikia mwanawe amefaulu mitihani na kuongoza kwa kuwa mwanafunzi wa kwanza kitaifa.

Alisema kuwa kijana wake amekuwa na juhudi katika masomo tangu akiwa shule ya msingi, ambapo alipofaulu kuingia kidato cha kwanza, hakuwa na uwezo wa kumsomesha, hali iliyomlazimu kuomba msaada serikalini, hivyo akasomeshwa na Mfuko wa Serikali Kuu hadi kidato cha nne, Shule ya Sekondari Ilboru, ambako aliibuka na ufaulu wa daraja la kwanza kwa pointi 10.

"Mimi ni fukara kabisa, tangu nilivyoacha kazi Jeshi la Magereza mwaka 1982, nimekuwa nikiishi kwa kutegemea ng'ombe wawili wa maziwa na hivi sasa nafanya kazi hii ya siasa ambayo ni ya kujitolea, nikiwa Katibu wa CHADEMA wilaya ya Ilala. Kwa kweli hata alipofaulu kwenda Ilboru nilipatwa na bumbuwazi sana, maana kila mzazi anapenda mtoto wake awe katika ushindani wa namna hii.

"Alipofaulu Kibaha nikafuatilia msaada ule tena serikalini, lakini nikaambiwa kuwa ulishafutwa, nikajitutumua mwenyewe kumsomesha, kwa sababu kijana mwingine wa kwanza alikuwa ameingia chuo kikuu na akapata mkopo, nikapata ahueni. Nimeishi kwa kujinyima sana ili watoto wasome, kijana mwingine sasa yuko form four na binti yuko form two," alisema Bw. Chacha kwa furaha.

Kwa upande wake, Amir Abdallah ambaye ameshika nafasi ya tatu kati ya watahiniwa 49,112 waliofanya mtihani huo wa Kidato cha Sita, anaishi na mama yake mzazi, Bi. Zainabu Hashimu, Yombo Vituka, Dar es Salaam. Baba yake alifariki mwaka 2008, wiki mbili kabla hajaanza kufanya mitihani ya kuhitimu Kidato cha Nne, Shule ya Sekondari Ilboru.

Kijana Abdalla ambaye Kidato cha Tano na Sita alisoma Shule ya Sekondari Feza (ya binafsi), amesoma pamoja na Chacha. Walikuwa darasa 'moja' Ilboru na wanafahamiana.

Mpaka alipopigiwa simu na gazeti hili na kumtaarifu kuwa ameshika nafasi ya tatu kitaifa, ndipo alipoamini taarifa alizokuwa amepewa na rafiki zake mapema asubuhi ya jana, kuwa amepata daraja la kwanza kwa pointi 3, yaani akiwa na alama A kwa masomo yote matatu ya mchepuo wa masomo ya Jiografia, Uchumi na Hesabu (EGM).

"Nilipigiwa simu na rafiki zangu wako Uturuki kuwa nimepata division one ya points 3. Nikajua wananizingua tu, ni utani, uongo kama ilivyo mara nyingi wakati matokeo yanakaribia kutoka. Nikapata pia message kutoka kwa mtu mmoja, sikuamini. Mpaka nilipopigiwa simu na mwandishi wa Majira akiniambia kuwa nimekuwa mtu wa tatu, hivyo nikaamini kweli nina division one ya points three.

"Baba yangu alifariki mwaka 2008 wiki mbili kabla ya mitihani ya form four. Kitu kikubwa ni determination (malengo) juu unachokifanya. Maana shule ya msingi nimesoma Yombo Vituka hapa hapa, O-level ndiyo nikaenda Ilboru, kwa kweli kule si kwamba mazingira ni mazuri sana, bali ni kwa sababu wanakutana wanafunzi wenye uwezo, muulizeni Chacha, huyo aliyekuwa wa kwanza atawaambia.

"Nilipata division one ya pointi tisa, hivyo mimi na mwenzangu aliyepata division one ya pointi saba tukapata sponsorship (ufadhili wa masomo) hapo Feza. Maisha yetu tangu baba afariki ni ya kawaida tu, tuna duka la vifaa vya ujenzi, ambalo ndilo tunategemea kwa kipato cha maisha yetu hapa nyumbani," alisema Abdalla, ambaye ndoto zake ni kusomea takwimu au uchumi.

Mama yake, Bi. Zainabu Hashimu anasema "kwa kweli nilipatwa na furaha. Unajua ile furaha inayokufanya utoe machozi. Siwezi kumsifia mazuri tu wakati hafanyi hivyo, lakini amekuwa ni kijana msikivu, namshukuru Mungu. Nilikuwa nikimwambia aepuke makundi, aangalie baba yake hayupo, tupo mimi na yeye, ingawa ndugu pia kama huyu baba yake mdogo wapo, lakini kuna kitu hivi unakikosa."

Naye John Daniel anaripoti kuwa Mshindi wa pili, Samwel Katwale alizungumza na Majira kwa simu kutoka Kijijini kwao Kanyama, Kisesa, Mkoani Mwanza, akisema kilichomfikisha katika hatua hiyo ni juhudi katika masomo na kutoingiza mchezo katika taaluma.

"Kilichonisaidia ni juhudi na ushirikiano kati ya walimu na wanafunzi wenzangu, nimefurahi sana," alisema.

Alipoulizwa shughuli za wazazi wake alisema, "Wazazi wangu ni wakulima na zao kuu ni mpunga, hata mimi nilikuwa shambani tangu asubuhi, nawashauri wanafunzi wenzangu wasicheze na masomo wapige mzigo," alisema mwanafunzi huyo alihojiwa saa 11 jioni.

Alisema matarajio yake ni kuwa Mhandisi ili kuziba pengo la upungufu wa wataalamu hao nchini, na kuwa hicho ndicho kilichomsukuma kuchukua masomo ya sanyasi, ya Fizikia, Kemia na Hisabati.

Mama mzazi wa mwanafunzi hiyo, Bi. Rachel Samwel, alisema amefurahi kiasi cha kukosa cha kusema.

"Kwa kweli nimepata furaha kiasi ambacho siwezi kuelezea, niseme tu namshukuru sana Mungu, sikutarajia, Mungu ndiye aliyemsaidia," alisema Bi. Samwel.

7 comments:

  1. Kweli inafurahisha mno hongerini vijana natumai hata huko juu mtafanya vizuri sana

    ReplyDelete
  2. Okay,; Kwanza nawapongeza vijana hawa kwa kiasi kikubwa mno maana wamejitahidi vya kutosha. Lakini naomba niwaulize au niwahoji waandishi au NECTA. Kwanini, watoto hawa WATATU wapate A'S zote kwa maana ya Div. I ya point 3, halafu mseme/ mtangaze kuwa huyu ni wa kwanza na huyu ni wa tatu hali ya kuwa wanalingana points??? Je hamuwezi kusema wamefungana/ wamelingana alama?? Ni busara kutafuta kigezo muafaka, otherwise mtawakatisha tamaa wanafunzi. Hivi kweli hamuuoni upungufu huo??????

    ReplyDelete
  3. Ndg yangu John Chriss ushindi haupimwi kwa points peke yake.wanaangalia pia alama za kila mmoja.ni kama sheria za football vile

    ReplyDelete
  4. Kwa kweli mazingira ya shule na aina ya walimu ndio siri nyingine inayoongeza chachu na hari ya kujitaftia maslahi zaidi kama alivyosema Chacha .

    Serikari boresheni mazingira ya shule na ya Walimu.

    ReplyDelete
  5. Napenda nichukue nafasi ya kuwapongeza wazazi wa watoto hawa. Kwanza kama nilivyosoma ya kwamba watoto hawa wanatoka katika familia za kawaida na kwamba wazazi wao walikuwa wakihangaika kwa njia moja au nyingine kuhakikisha ya kwamba watoto wao wanaendelea na masomo. Kutokana na malezi ya wazazi na jitihada zao watoto nao wakawashiwa moto wa kuona umuhimu wa kujitahidi kusoma na hata kufaulu. Jambo hili na liwe changamoto kwetu sote ili vijana wetu wapate moyo kama hawa. Ninaamini wapo wazazi wengi wanapendao watoto wao waendelee mbele japo kwa hali ngumu kiuchumi. Hali ya ugumu wa maisha iwapo mbaya tusife moyo maana hata Askari Mstahafu Mzee Chacha kwa ng'ombe wawili wa maziwa na misaada mingine kaweza. Mmoja yuko Chuo Kikuu, Wawili bado wapo Sekondari na ha huyu kafaulu Kidato cha 6. Nawapongeza vijana hao na kuwaomba wengine wajitahidi ili kujikomboa na baadaye kuleta maendeleo nchini mwetu.

    ReplyDelete
  6. Big up sana vijana Chaguen coarse sahihi chuo

    ReplyDelete
  7. RAJABU SALLA . SAUT - MWANZAApril 30, 2011 at 10:46 AM

    You scratch my back and I'll scratch yours. You help me and I'll help you. USIWASAHAU WOTE WALIO KUSAIDIA, INA WEZEKANA WALIJINYIMA VINGI KWA SABABU YAKO, HASA WAZAZI.

    ReplyDelete