Na Grace Michael
SERIKALI imetoa mwezi mmoja kwa walimu waliochukua posho za awali wakati wakiripoti katika vituo vyao vya kazi na kisha kuondoka kurejesha fedha hizo kwa kuwa
vitendo hivyo ni wizi wa fedha za umma.
Agizo hilo lilitolewa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI),
Bw. George Mkuchika wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake
kuhusiana na tatizo la ucheleweshaji wa mishahara kwa walimu wapya walioajiriwa
Februari mwaka huu.
“Natoa agizo hili kwa walimu wote ambao walipangwa kwenye vituo vya kazi na
baada ya kuripoti na kuchukua posho zote zinazotakiwa na kisha kuondoka
kurejesha fedha hizo haraka kwani kitendo walichokifanya ni wizi...hao ni wezi
wa fedha za umma hivyo tunawapa mwezi mmoja na wasipofanya hivyo tutawatafuta na kuwafikisha mahakamani,” alisema Bw. Mkuchika.
Alisema kuwa taarifa za walimu hao bado zinaendelea kukusanywa katika
halmashari zote na baada ya kupatikana, wizara itatoa takwimu za walimu hao na fedha zilizochukuliwa.
Hata hivyo alisema kuwa endapo walimu hao wataamua kurejea katika vituo vyao vya kazi, watapokelewa lakini watapewa onyo kulingana na taratibu na kanuni za kazi.
Akizungumzia tatizo la ucheleweshaji wa mishahara, alisema kuwa kabla ya mwaka
2009, ulipaji wa mshahara kwa walimu wapya ulichukua muda usiopungua miezi
mitatu hadi sita kwa walimu kuanza kupata mishara yao, ili kuondokana na
usumbufu huo, serikali iliamua walimu wapya kuingizwa moja kwa moja kwenye mfumo wa malipo ili kuondokana na kero ya kuchelewa kwa mishahara yao.
Alisema kuwa pamoja na serikali kuwa na nia njema, kulijitokeza
changamoto ambazo ziliathiri udhibiti wa mfumo wa malipo ambazo ni pamoja na
baadhi ya walimu kutoripoti walikopangwa, baadhi kugundulika kuwa na sifa za
kughushi na hivyo kuachishwa kazi na wengine kuripoti na kuchukua posho na kisha kutoweka, hali iliyosababisha kuwepo kwa watumishi hewa kwenye mfumo wa malipo.
“Baada ya matatizo haya, serikali iliamua kuboresha mfumo na udhibiti wa malipo kwa kuondoa wataumishi hewa, taarifa za walimu waliothibitishwa na waajiri wao kwamba wameripoti na wako vituoni ndio huingizwa kwenye malipo na kutokana na uamuzi huo baadhi ya walimu wapya hawakuingizwa kwenye mfumo wa malipo,” alisema Bw. Mkuchika.
Alisema kuwa kutoingizwa kwa walimu hao katika malipo kumetokana na baadhi
kuchelewa kuripoti au ukamilishaji wa taarifa zao kuwa na upungufu au kuchelewa
kuwasilishwa kwa taarifa hizo ofisi ya Rais Utumishi hali iliyosababisha
malalamiko kutoka kwa walimu.
Kutokana na hali hiyo, aliwataka walimu kuripoti vituo vyao vya kazi kwa muda
uliopangwa ili kurahisisha ujazaji fomu maalum zenye taarifa ya kiutumishi ya
mtumishi ambayo itawezesha wakurugenzi wa halmashauri kuzituma Ofisi ya Rais
Utumishi kwa wakati.
No comments:
Post a Comment