29 April 2011

Raza: Muswada wa Katiba upitishwe kwa uwiano

Na Mwajuma Juma, Zanzibar

MFANYABIASHARA Mohammed Raza, amesema mswada wa kuweka utaratibu wa
marekebisho ya katiba lazima upitishwe na wabunge, kwa
kuzingatia theluthi
mbili kutoka Zanzibar na Tanzania Bara.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Zanzibar, Bw. Raza alisema
mswada huo una umuhimu mkubwa katika misingi ya muungano na kulitaka bunge
lisipitishe muswada huo kwa kuangalia wingi wa idadi ya wabunge.

“Muswada wa kuweka utaratibu wa marekebisho ya katiba upitishwe kwa
kuzingatia theluthi mbili za wabunge kutoka bara na Zanzibar na sio wingi wa
kura,” alisema.

Alisema kwamba kabla ya muswada huo kupeleka bungeni matayarisho yake
lazima yaangaliwe na pande mbili za muungano, ili kuondosha mivutano kama ilivyojitokeza na kusababisha muswada huo kukwama kuwasilishwa hivi karibuni.

Hata hivyo, alisema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umeleta faida kubwa
kwa vile Wazanzibari wengi wanategemea soko la biashara la Tanzania Bara na
umesaidia kuwaunganisha wananchi wa pande mbili za Muungano.

“Asiyetaka muungano sio mwana halali, na bahati mbaya wanaopinga hawafahamu
faida za muungano, ikiwemo kuwa na umoja,” alisema Bw. Raza ambae aliwahi
kuwa mshauri wa Rais wa Zanzibar wa awamu ya tano, katika masuala ya michezo.

Aidha alisema kwamba wakati wa kuzungumza maslahi ya nchi mbili ni vizuri
Wazanzibari wakatumia nafasi hiyo kwa kujenga hoja, kuondoa woga na kuwa
wakweli.

Alisema matatizo mengi yaliyomo katika Muungano yalisababishwa na
wazanzibari wenyewe kutokana na kutokuwa wakweli hasa kusimamia maslahi ya
Zanzibar ndani ya Muungano.

Alitoa mfano alisema nafasi ya rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais wa
Muungano ilifutwa na Wazanzibari wenyewe kuwa mstari wa mbele kupitisha
suala hilo bungeni bila ya kuangalia maslahi ya Zanzibar.

Aidha alisema kwamba wapo Wazanzibari waliokuwa mstari wa mbele kupinga Rais
wa Zanzibar asiwe na uwezo wa kupigiwa mizinga 21 kwa wageni wa kitaifa
wanapotembelea Zanzibar, kwa vile sio Amiri Jeshi Mkuu wa Majenshi ya Ulinzi
na Usalama nchini.

No comments:

Post a Comment