15 April 2011

Vijana Stars vitani tena

*Waondoka na matumaini kibao

Na Addolph Bruno

TIMU ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 23 'Vijana Stars', imeondoka jana mchana kwenda Uganda ambapo kesho itacheza na Uganda katika
mechi ya kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika. Mechi itachezwa kwenye Uwanja wa Mandela (Namboole).

Vijana Stars imeondoka ikiwa na msafara wa wachezaji 21 na viongozi wanane ukiongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA), Hafidhi Ali Tahir pamoja na makocha Jamhuri Kihwelu 'Julio' na msaidizi wake Adolph Rishard.

Akizungumza kabla ya kuwakabidhi bendera Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la taifa (BMT), Kanali Mstaafu Idd Kipingu aliwataka wachezaji wa timu hiyo kucheza kwa bidii kama walivyofanya Jumamosi iliyopita ambayo iliwafunga Cameroon katika mchezo wa marudiano kwa mabao 4-3 kuitupa nje ya michuano ya kusaka tiketi ya kucheza michuano ya Olimpiki mwakani.

Kipingu ambaye aliwasifu wachezaji hao kwa juhudi walizozionesha walipoumana na Cameroon, alisema wanatakiwa kutambua kuwa hawana tofauti na Uganda na timu nyingine yoyote jambo ambalo ni silaha kubwa kwa timu zinazoshinda.

"Hatuna wasiwasi pia na benchi la ufundi linaloongozwa na kocha Julio, hongera sana kocha, lakini nawaombeni mzidishe bidii katika kufanya mamuzi, hiyo ndiyo silaha kubwa wanayoitumia wenzetu ongezeni bidii ni wakati wenu huu.

"Juzi mlipocheza na Cameroon mlionesha kweli mna nia, Watanzania wote tunaamini mtashinda na Uganda ni wenzetu tumewazoea na kama mkiondoka hapa na nia, mtashinda tu kwa sababu lengo ni kuwa bingwa na dawa ya kuwa bingwa ni kucheza na hata hao Nigeria tuliopangwa nao tutawashinda tu," alisema Kipingu.

Naye Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga aliwataka wachezaji hao kujiamini kabla na baada ya mchezo ili kuendeleza mafanikio mazuri ya juzi, baada ya Cameroon na kuongeza kuwa ushindi uliopatikana ni wa kihistoria.

Kwa upande wake, Julio alisema hana wasiwasi na vijana wake kutokana na mazoezi ya kujenga stamina na mengine waliyofanya na kuwaomba Watanzania, kutulia na kuacha kuwasifia kwa sasa mpaka watakapomaliza kazi waliyowatuma.

Akizungumzia mchezo huo wa kesho, nahodha wa timu hiyo, Shaaban Kado alisema hawana wasiwasi nao na kuahidi ushindi kutokana na kwamba wanaelewa wanachokifanya na kuongeza kwamba wameamua kuwafurahisha Watanzania.

Timu hiyo itacheza mechi ya marudiano na wapinzani wao Aprili 30, mwaka huu Jijini Dar es Salaam na ikiwa itashinda mechi hizo itacheza na mshindi kati ya Kenya na Eritrea ambapo fainali zitafanyika Maputo nchini Msumbiji Septemba 3 hadi 18 mwaka huu.

1 comment:

  1. Nikweli wachezaji wanatakiwa kucheza kwa bidii ili ushindi upatikane na sio kuingia uwanjani na dharau pamoja na mawazo yakuwa walishaifunga Cameroon kwa hiyo Uganda si chochote.Yoyote yule anayekuja mbele yako unatakiwa kupigana nae kwa nguvu zote bila ya dharau.Hii ni tahadhari natoa kwani wachezaji wa nyumbani walishazoea kutoa visingizio baada ya kufungwa kuwa wenzao waliwakamia sana kwa sababu walishaifunga Cameroon.Wanatakiwa kuingia uwanjani kwa ari kubwa na ikiwezekana washinde kwa ushindi mkubwa tu ili kuonyesha ya kuwa wao ni wazuri kwa kuingia vitani bila ya dharau na kupata ushindi mnono.

    ReplyDelete