15 April 2011

BTL yajitoa NSSF Cup

Na Mwandishi Wetu

TIMU za Business Times Limited (BTL) zimejitoa kwenye michuano ya vyombo vya habari ili kulinda heshima ya waandaaji na wadhamini NSSF.BTL ilitakiwa kucheza
kesho kutafuta mshindi wa tatu katika mpira wa miguu na netiboli kwenye viwanja vya Sigara, Dar es Salaam.

Kwa uamuzi huo, timu ya soka ya Uhuru itakuwa mshindi wa tatu na TBC itashika nafasi hiyo katika mchezo wa netiboli.

"Tunaiheshimu taasisi ya NSSF na uongozi wake kwa hiyo tusingependa uhusiano wetu mzuri uharibiwe na mtu au watu wachache wenye maslahi binafsi," alisema Meneja wa timu za BTL, Masoud Sanani.

Alisema Business Times inaamini kuwa NSSF ilianzisha michuano hiyo ikiwa na malengo mazuri na daima itakuwa inaamini hivyo hasa kwa kuelewa busara za Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dkt. Ramadhan Dau.

Lakini, Sanani akasema BTL imefikia hatua ya kuziondoa timu zake kutokana na kitendo cha kudhihirika bila shaka yoyote kuwa timu ya NSSF, ilichezesha wachezaji mamluki katika mechi ya nusu fainali ya soka iliyochezwa Aprili 12.

Kamati ya Mashindano ya michezo hiyo iliipiga faini ya sh. 500,000 NSSF kwa kosa hilo, jambo ambalo BTL imelipinga ikitaka Kanuni ya 5 za mashindano hayo inayohusu Taratibu za Mchezo namba 14 itumike au vyote kwa pamoja kutokana na ukubwa wa kosa.
 
Kamishna wa mchezo huo, Mohamed Mharizo wa New Habari alieleza kwenye kikao cha Kamati ya Mashindano jinsi ambavyo timu ya NSSF, ilivyofanya ujanja wa kumtoa mchezaji mamluki na kumwingiza mwingine bila kupitia kwa mwamuzi wa akiba.

Wachezaji wote wawili walitumia namba 16 kwa lengo la kutaka kuficha udanganyifu uliofanywa na timu ya NSSF, baada ya kupata fununu kuwa BTL imegundua.

No comments:

Post a Comment