LONDON, England
MLINDA mlango wa Manchester United, Edwin van der Sar amekiri kuwa walijiua wenyewe kwa kucheza chini ya kiwango na kisha wakakubali kufungwa na Manchester City
katika mechi ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la FA.
Mholanzi huyo anaamini kuwa mashetani hao wekundu hawakuwa kwenye kiwango kizuri na akasema timu yao ilichoka kwa kiasi fulani dakika za mwisho.
"Tulianza mpambano taratibu mno, lakini tukapata nafasi mbili za kuweza kushinda kwa haraka," alikiambia kituo cha televisheni cha MUTV. "Endapo moja ya nafasi ingeweza kuingia nyavuni mechi ingekuwa tofauti na ingebidi waanze kutufukuza," aliongeza.
Alisema kipindi cha pili wapinzani wao walifanikiwa kufunga bao, huku wao wakiwa wamebaki wachezaji 10 hivyo ilikuwa vigumu kwao kuwafukuza na kujaribu kusawazisha.
Mlinda mlango huyo alisema kuwa kuna wakati walikuwa almanusura kupata bao, ama kupata uwezekano wa kuingia ndani ya eneo la hatari lakini hakuna kilichotokea na hivyo wakabaki na matumani ya kupata bao dakika za majeruhi, lakini bahati haikuwa yao.
"Mara zote inakuwa vizuri unapokuwa wa kwanza kufunga bao, lakini haikutokea na nafasi tulizozipata zilitoweka," alisema na kuongeza kuwa hata hivyo hakuna mchezaji wa kumlaumu kwa maana wote walikuwa uwanjani na anadhani hakuna hata mmoja, aliyecheza kwa kiwango chake hivyo akawashauri kukaza buti kesho.
No comments:
Post a Comment