17 April 2011

Uganda yaifunga Vijana Stars 2-1

*Yahitaji bao moja kusonga mbele

Na Mwandishi Wetu, Kampala

TIMU ya taifa ya vijana wenye miaka chini ya 23, ya Tanzania (Vijana Stars), jana ililala mabao 2-1, dhidi ya Uganda 'The Cobs', katika mechi iliyochezwa
kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole, Uganda.

Katika mchezo huo wa kuwania kucheza fainali za Afrika 'All African Games' zitakazofanyika nchini Msumbiji mwaka huu.

Bao la kwanza la The Cobs, lilifungwa dakika ya nne na Moses Oloya anayecheza soka la kulipwa nchini Vietnam.

Wakicheza nyumbani huku wakishangiliwa na mashabiki wao, Uganda walijipatia bao la pili dakika ya 23, kupitia kwa Kiiza Hamis.

Pamoja na kufungwa kwa mabao hayo, Vijana Stars, hawakukata tamaa, walizidi kuwabana Waganda na kulifikia lao mara kwa mara.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Vijana Stars wakisaka mabao ya kuwasazisha.

Dakika ya 46, Vijana Stars walipata bao lililofungwa na Kigi Makasi kwa shuti lililokwenda moja kwa moja wavuni.

Kutokana na kupata bao hilo, Vijana Stars walirejesha matumaini ya kuing'oa Uganda katika michuano hiyo, wakati watakaporudiana wiki mbili zijazo.

Kikosi cha Vijana Stars kilicho chini ya Jamhuri Kihwelo 'Julio', kitarejea nchini Jumatatu kikitokea nchini Uganda.

Vijana Stars wanatakiwa kushinda bao 1-0, katika mechi ya marudiano itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wiki mbili zijazo.Matokeo hayo, yanarudisha kumbukumbu nzuri ya Watanzania, baada ya kuitoa Camroon kwenye mechi za kuwania kucheza michuano ya Olimpiki.

Katika mechi yao ya kwanza iliyochezwa mjini Younde, Cameroon, Vijana Stars ilifungwa mabao 2-1, hivyo ikatumia vizuri uwanjani wa nyumbani.

1 comment:

  1. Mambo ndo kama yalivyo. Tumechoka na majigambo ya makocha. Maneno ya Julio hayana maana hata kidogo. Yeye anadai Nigeri haina kitu wakati anafungwa na Uganda. Kuitoa Cameroon iswe kigezo cha kuzdharau team nyingine. Julio awe mwenye kusoma alama za nyakati. Kama Tanzania imebadirika kimpira ni wazi kuwa hata nchi nyingine zimebadirika. Cha muhimu ni kufanya maandalizi ya kutosha kwa vijana wetu. Sasa anatakiwa kutafuta michezo mingi ya kirafiki kwa team hiyo. Sio lazima kwenda nje ya nchi. Vija wanaweza kupata mazoezi mazuri kwa kuztumia team za ndani ya nchi kama Police Dodoma, Mtibwa, Taifa Stars, na hasa zile zilizopanda daraja msimu huu.

    ReplyDelete