15 April 2011

'CCM bado imevaa mfumo wa ufisadi'

*Kiongozi UVCCM adai utawasaidia waliotemwa kuibuka
*Msekwa asema kinachowaumiza ni mbio za urais 2015


SIKU chache baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kufanya kile kinachoitwa ni kujivua gamba, imeelezwa kuwa hatua hiyo haitasaidia, kwani 'imeondoa
watu badala ya mfumo dhaifu' ambao ndiyo jamvi la mafisadi ndani ya chama na serikali yake.

Imeelezwa kuwa pamoja na CCM kutaka baadhi ya watuhumiwa wa ufisadi katika kashfa mbalimbali ambazo zimekuwa zikiitikisa nchi kwa muda mrefu sasa, wajirekebishe au kukaa kando, bado wanaweza kutumia mfumo dhaifu uliolea ufisadi kwa muda mrefu, hata kama wako nje, kwani 'watu hao wana vibaraka na mawakala wao katika maeneo mengi nchini'.

Hayo yalisemwa jana na Mjumbe wa Mkutano wa Wilaya Umoja wa Vijana wa CCM, Moshi Vijijini, Bw. Paul Makonda alipozungumza na waandishi wa habari kuhusiana na hatua hiyo ya CCM, ya kuteua wajumbe wapya wa Kamati Kuu (CC) na sekretarieti, baada ya wale wa awali kujiuzulu.

Alipobanwa na waandishi wa habari, wakitaka kujua kundi lipi analitumikia kati ya yaliyopo ndani ya CCM, alisema kuwa anatumwa na wananchi wasiokuwa na sauti, wanyonge, wasiosikika, walioko vijijini, baadhi yao wakiwa ni wana-CCM, ambao wakati mwingine si rahisi kuvifikia vyombo vya habari na kupaza madai yao dhidi ya matatizo yanayoikabili nchi na chama chao.

Huku akitaja majina ya baadhi ya watuhumiwa wa ufisadi, Bw. Makonda alisema kuwa wametumia mwanya wa mfumo huo wa ufisadi kushawishi uteuzi wa mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na nafasi nyingine mpaka ngazi za chini ambao ni watiifu kwao, hivyo wanaweza kuwatumia kadri wanavyotaka, kwani 'ni mawakala na vibaraka wao'.

Akizungumza kwa ujasiri, Bw. Mkonda alisema kuwa anatumia nafasi yake hiyo pamoja na ile ya Mjumbe wa Mkutano wa UVCCM Mkoa wa Kilimanjaro kutoa maoni yake, ambapo alisema kuwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete anastahili pongezi kwa uamuzi huo mgumu wa Dodoma.

"Tumpongeze Rais Jakaya Kikwete kwa uamuzi mgumu, ambao kabla haukutarajiwa na yeyote awe mwanachama au si mwanachama. Uamuzi wa kuvunja sekretarieti ya chama siyo tu ulikuwa mgumu, bali athari zake hata sasa itakuwa ngumu kuchukuliwa na wahusika na washirika wao. Haya ndiyo maamuzi ambayo wanachama wanaweza kuandamana kuyaunga mkono.

"Hata hivyo kilichofanyika ni mkakati wa kujinusuru, ambapo sasa Sekretarieti mpya chini ya Katibu Mkuu Bw. Wilson Mukama inalo jukumu la kuhaulisha haiba ya chama iliyopauka machoni pa Watanzania na miongoni mwa wanachama na kuelekeza katika mkakati wa ushindi endelevu, kwa kukibadilisha chama kutoka utendaji kwa uzoefu, kwenda utendaji wa kitaalamu unaozingatia nyakati tulizonazo.

"Yaliyotokea Dodoma ni katika juhudi za chama kujinasua na mtego wa kuporomoka kwenye siasa za Tanzania na kimataifa...sasa ni wakati wa kuondokana na utendaji mazoea na kwenda kisayansi...kilichotokea ni kuondoa watu dhaifu na si kuondoa mfumo dhaifu, uliojengeka kwa kipindi kirefu ambao ulisababisha watu wenye uroho. Walioamua kuweka mustakabali wa taifa rehani kwa maslahi yao binafsi kuigeuza nchi kuwa jamvi la mafisadi.

"Ni mfumo huu dhaifu uliopelekea uimarishaji wa watu badala ya kuimarisha mifumo ya utawala, siasa, demokrasia na haki za binadamu, utawala wa sheria na ushiriki wa wananchi katika kujiletea maendeleo," alisema Bw. Makonda kwa kirefu, akiongeza kuwa haitoshi kuwaondoa akina Andrew Chenge, Edward Lowassa na Rostam Aziz.

Alisema kuwa kwa muda mrefu chama hicho kimejikita katika kuangalia matokeo kama njia ya kujihalalisha machoni pa watu na kuwatambia wapinzani, badala ya kuangalia mfumo unaokiwezesha kupata matokeo, hivyo kimeshtuka baada ya 'kuvuliwa nguo sehemu nyeti na wapinzani', kwa kushindwa katika maeneo aliyodai yalikuwa muhimu na ngome ya CCM, kwenye uchaguzi uliopita.

Kijana huyo ambaye alionekana kutoa maelekezo kwa sekretarieti mpya ya CCM, alisema kuwa kinatakiwa kujifanyia marekebisho ya kimfumo ndani ya chama, kuufanya utafiti wa mwelekeo wa kisiasa kuwa ndiyo kipaumbele cha ofisi ya katibu wa uenezi na itikadi, kutumia mifumo ya kisasa ya mawasiliano kutoa taarifa kwa haraka, bila kuwa na milolongo ya kusubiri vikao halali.

Akiwageukia wenzake wa UVCCM, ambao katika mkutano wa kwanza aliwapatia siku saba wajiuzulu akiwatuhumu kwenda kinyume na katiba na kanuni za CCM, alisema sasa yuko katika mchakato wa kuandaa UVCCM nyingine, ambayo amesema itaitwa UVCCM-Maadili, ambao uko mbioni kumalizika na kuwasilishwa mezani kwa katibu mkuu mpya.

Alisema kuwa anatumia haki ya ibara ya 15 katika katiba ya CCM kuunda UVCCM-Maadili, akiwataka vijana wengine wanachama wa CCM, wanaotaka kuitumikia nchi kwa uadilifu, kujitokeza na kumuunga mkono katika mchakato huo, akisema UVCCM iliyopo imeshindwa majukumu, badala yake viongozi wake wamekuwa vibaraka na mawakala wa mafisadi.

Pia alitoa madai mazito kwa mmoja wa makada wa chama hicho, wanaotuhumiwa kwa ufisadi, Bw. Rostam Aziz, akitaka aondolewe katika chama, pamoja na viongozi wa UVCCM, Mwenyekiti Beno Malisa, James Millya, Hussen Bashe na Martine Shighela, ambao alidai ni vibaraka wake, akisema mwenendo wao umeharibu chama na ustawi wa taifa kwa ujumla.

"CCM imetoa siku tisini kwa wale wenye tuhuma za ufisadi, walojihusisha na DOWANS, KAGODA, na mambo mengine yaliyoaibisha nchi na kushusha haiba ya chama mbele ya wapiga kura. Huu ni muda mrefu mno kwa watu kama hawa. Wanaweza kutumia muda huo kufanya mambo ya ajabu kabisa. Hivyo wao wenyewe wachukue hatua hizo mapema."

Bw. Makonda aliongeza kuwa iwapo Bw. Lowassa aliwahi kujiuzulu katika kashfa ya Richmond, mapema wakati bunge likiendelea na mjadala, basi anatakiwa kufanya vivyo hivyo katika hatua hii, pamoja na watuhumiwa wengine wote.

Msekwa ataja kinachotuumiza

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tazania Bara, Bw.  Pius Msekwa amsema kuwa miongoni mwa mambo ambayo yanakiumiza chama hicho ndani kwa ndani ni mbio za urais katika uchaguzi wa mwaka 2015.

Msekwa aliyasema hayo jana wakati akizungumza kwenye hafla fupi ya kutambulisha Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM taifa iliyochaguliwa hivi karibuni mjini Dodoma baada ya chama hicho ujivua gamba' na kujiuzuku kwa ile ya awali.

Msekwa alisema kuwa hivi sasa ndani ya chama hicho yapo makundi ya vinara wanaowania urais ambayo yamewagawa wanachama wa chama hicho  na hali hiyo imekuwa ikiathiri umoja na mshikamano ndani ya chama kwa kiwango kikubwa.

Alisema kuwa umoja na mshikamano ndani ya chama ni nguvu kubwa  inayowahakikishia ushindi katika mashindano na vyama vingine, hivyo tatizo hilo la vinara kuwagawa wanachama ni kubwa na linaathiri  chama kwa kiwango kikubwa, hivyo chama hakina budi  kulitafutia ufumbuzi wa haraka.

Akifafanua zaidi, alisema kuwa kiini kikubwa cha tatizo hilo ni utaratibu wa kupata wagombea wa CCM ambao unatumika hivi sasa kulingana na kanuni za uchaguzi wa kuingia katika vyombo vya dola zilizopo.

Kufuatia hali hiyo, Bw. Msekwa alisema kuwa NEC imefanya mageuzi kwa kuelekeza utafutwe utaratibu bora zaidi wa kupata mgombea urais kwa tiketi ya CCM ambao utalenga kuzuia matumizi makubwa ya fedha kwa nia ya kununua kura za wajumbe wa vikao vya uchujaji na vya uteuzi wa mwisho katika mchakato huo.

Naye Katibu Mkuu mpya wa chama hicho, Bw, Wilson Mukama alisema kuwa yaliyofanywa na chama hicho ni maamuzi ya kimapinduzi na wala  hayapunguzi heshima ya chama hicho, hivyo wana-CCM hawapaswi
kukaa kama kuku katika tenga, watembee kifua mbele kwani chama chao kimeimarishwa.

Mukama alisema kuwa mageuzi yaliyofanyika ndani ya chama si ya kujipodoa bali ya kukijenga upya ili kiweze kuleta ari mpya kwa wanachama wake na kuahidi kuwa kazi ya sekretarieti hiyo mpya wajiandae kuona matokeo mazuri.

Imeandaliwa na Tumaini Makene, Dar; na Pendo Mtibuche, Dodoma

22 comments:

  1. Ningekuwa mimi ni CCM nisingekuwa na maneno mengi... Ningefanya yale yanayotarajiwa na wananchi halafu niwataarifu wananchi tumefanya nini. Sio tutafanya nini.
    Tunasikia tambo nyingi sana kupitia Mukama na Nape Nnauye.
    Badala ya tambo, wao wachape kazi... Mwenye macho haambiwi tazama.. tutaona tu.
    Hata walipokumbatia mafisadi, hatukuambiwa, tuliona tu.
    Kama watabadilika na kufuata maadili, tutaona tu... Kelele na ahadi nyingi hazitusaidii

    ReplyDelete
  2. Debe shinda haliachi kutika! CCM inatika sana, haina lo lote. Kuwatosa wachache wakidhani wamewazuia kuwania urais 2015, wamejidanganya. Subira yavuta heri - tutaona wakati utakapowadia kwani wazungu husema "some of the things are time-factor" (baadhi ya mambo huamuliwa na wakati).

    ReplyDelete
  3. Jamani tusikilizane tuwache propaganda zilokuwa hazina maana ccm ni chama makini na kina viongozi wazuri sana ila baadhi ya wale wachache ambao wanaotaka kukichafua walikuwa mzigo sasa tumewabwaga chali na tutaendelea kukisafisha katika siku 90 kama alivyosema mwenyekiti wetu wa ccm Taifa kikwete kwahiyo hizi kelele na propaganda za chadema zisikukosesheni usingizi hawa ni wanasiasa wahuni ambao lengo lao ni kujitafutia umaarufu na ni chama ambacho cha kikabila ni hatari kubwa kwa taifa letu hili ,mimi binafsi naomba watanzania wenzangu tuisapotini ccm kwasababu ni chama kikongwa ambacho kinajali masilahi ya Taifa tusijiaribu kumpa nchi mtu ambae usomjua tutakuja kujijutia baadae mifano mengi tumeiona kuhusu hawa chadema hawana lolote kazi kutaka kujitafutia umaarufu na kujitafutia sifa ila nakuombeni sana achananeni nao chama bora jamani ni ccm ni chama kinajali masilahi ya taifa hili

    ReplyDelete
  4. yAANI WE UNAPONDA CHADEMA?BASI WEWE UNAPENDA MAFISADI TANGIA JAKAYA,LOWASA ROSTAM,CHANGE NA WOTE,UNAFAGILIA MAMBO YAO,SUBIRI PESA ZAO ZIKO NJE NJE UCHAGUZI MKUU UKIWADIA,GALAGABAHO!

    ReplyDelete
  5. HUYU ANAYETETEA MAFISADI NI MTANZANIA KWELI?!
    ANAJUA KUWA TANZANIA NI MASIKINI NA NI NCHI YENYE RASILIMALI NYINGI DUNIANI,LAKINI WANAOFAIDI NI HAO AKINA R ZIZI RAFIKI ZAKE

    ReplyDelete
  6. Kaka Bustani pole sana, hatuhitaji mganga wa kienyeji kutabiri kuwa wewe either ni kati ya mafisadi ya CCM ama uelewa wako ni mdogo sana juu ya maendeleo ya nchi. Rais Tangu aingie madarakani amekumbatia mafisadi sisi wote tunaona, halafu wewe unasema chama makini, hapa nadhani wewe pia miongoni mwao. CCM inakubalika vijijini kwa sababu ya uelewa mdogo wa watu, hwajui maendeleo nini na hawajahi pata maendeleo. ukienda mjini, waliko wasomi CCM haina chake. CCM imetoa siku 90, tuone kama kunachochote cha maana kitafanyika. hiyo danganya toto.
    Kwa wale wanaonufaka na CCM wanvitambi na magari ya Kifahari mnahakia ya kutetea CCM ila kwa wewe ambaye huna mbele wala nyuma na hujua hata leo utakulala nini ni upumbavu kwa kiasi kikubwa kuendelea kuwashibikia wenzako hali hata ahwakujui.
    CHADEMA chama cha wanyonge. Msikate tamaa.

    ReplyDelete
  7. Chadema chama cha Wanyonge! Hili ni wazo finyu kabisa. Mnyonge ni nani Chadema au mtu akisema mnyonge ana maana gani? Kisiasa, kiuchumi, kijamii, kiafya na mengineyo? Chadema ni chama cha siasa kama vyama vingine na waliomo ndani yake wanatetetea masilahi ya aidha wanachama wake au wananchi kadhaa. Mbowe, Slaa, Zitto na wengine wana unyonge gani kama si kutafuta nao sifa, heshima nk.? Chama ni chama na huwa kina malengo yake kwa jamii; malengo yake yakikubalika kwa jamii basi jamii hukichagua. Isiwe kila siku tunasema Watanzania ni wanyonge wanyonge, ni lini basi tutaondokana na unyonge huu? Hata Waamerika nao wanafanya hivyo hivyo chama kikionyesha jambo ambalo linakubalika kwa jamii basi kinapata ushindi. Kitambi si dalili ya kutokuwa mnyonge bali ni maumbile ya mtu, na maumbile ya mtu hayafuati uwezo wala utajiri maana kuna wengi wana vitambi lakini si matajiri wa mamilioni. UPO?

    ReplyDelete
  8. Hilo ndo tatizo la wanasiasi wa tanzania, most of the time mnapenda sana Direct translation, unyonge na vitambi ulivyofafanua hapo juu si kumaainisha hivyo.
    Nikianza na Vitambi, hapa naishutumu CCM kwa kuendeleza mfumo ulipekea income inequality ndani ya jamii, nina maana gap la wenye nacho na wasokuwa nacho linazidi kuwa kubwa. To me vitambi ni wale waliojilimbikizia mali za kifisadi, na wala sikumaanisha mwili mtu, kwani mwili wa mtu kuwa na kitambi kitaalam ni ugonjwa. katika hilo bado unanipa hofu na uelewa wako.

    Swala la chadema kuwa chama cha wanyonge, sikumaanisha kuwa chadema ni wanyonge, Hata ukitama kwa nje watu wa Chadema ni strong kulinganisha na CCM, huwezi ukalinganisha uwezo na uelewa wa chedema na CCM. Hata kwenye kura Chadema walishinda mijini kwenye watu wenye uelewa ila CCM ilishinda vijijini walikojaa wasiojua kusoma hata kuandika, Swala la Unyonge nilimaanisha kuwa Chadema kimeonesha kwa vitendo kuwa kinatetea wanyonge wasikuwa na sauti. Mfano uwizi wa Richimond isingekuwa Chadema Lowasa angewajibika?
    Umesisitiza kuwa Watanznia siyo wanyonge, nataka nikulize swali hivi wewe unajua kuwa Vijiji hakuna elimu, hakuna barabara, hakuna maji safi, hakuna umeme, hakuna huduma za afya, njaa kila mara na matatizo chungu nzima, lakini CCM akiomba kura wanaipa zote, kwangu mimi hiyo elimu finyu na unyonge wa wale wenye elimu.

    ReplyDelete
  9. Huyo bwana asiyejua hata wanyonge wakoje mi sipati shida kumsema kuwa ni kipofu wa mawazo ambayo hata kama macho yanaona ila hawezi kuona kwa mawazo, huyu anahitaji kusukumwa kama gari lililoshindwa kuwaka kisa betri haina nguvu. Naomba nimweleze kuwa, wanyonge ni watu wenye matatizo fulani ila hawana uwezo wa kuyapigia kelele kwani hata ukiwapeleka kwenye vituo vya televisheni na radio, wanahofu kuwa wakisema watakamatwa na serikali ya Mafisadi ila Chadema wanaweza kuwasemea na hao mafisadi wakapata hofu na kupunguza walau baadhi ya kero.

    ReplyDelete
  10. Walinioeleza hapo juu kuhusu unyonge na vitambi wamefanya vema lakini naona kuna mambo ambayo hawakuyafafanua kuhusu unyonge wa Mtanzania. Ninafahamu hakika hali ya nchi yangu maana hata mimi inanigusa kila kona. Ila napenda kusema ya kwamba mtu asitoe mawazo kwa mafumbo! Nilisema napenda kujua unyonge wa Mtanzania ni upi; kiuchumi, kielimu kisiasa kiafya nk. Vijijini mtu akisema hakuna elimu anamaanisha elimu gani? Maana kama nijuavyo mimi kila sehemu ya nchi yetu ina shule ya Msingi na siku hizi kuna mpango wa kila Kata kuwa na Sekondari! Je Ujenzi wa nchi unategemea Chama au unategemea juhudi za wanachi wazalendo wenyewe? wewe ukiwa mmoja wapo? Mimi sipingi wala kuona Chadema kama chama hakifai ila nisemalo ni kwamba sera zake zikikubalika basi tutawapa watuongoze 2015, ila kwa sasa tutatue matatizo yetu tukiitumia serikali iliyopo madarakani. Kama yupo fisadi awe wa CCM au CUF au CHADEMA nk basi huyu asikubalike na awajibishwe. Naitakia nchi yangu ambayo naipenda na kuithamini maana hata kama nitakufa kwa njaa basi nitafia Tanzania ila sitakubali kuendeshwa na siasa za chuki.

    ReplyDelete
  11. CCM wanapata ushindi vijijini ambako kuna ufukura usiokuwa wa kawaida na uelewa duni wa mambo.Kwa mjini si rahisi kwao kwani uelewa wa watu kupima ni mkubwa hata kama mtu hajaenda shule.

    Kwa vijijini watu bado wanaishi katika ujamaa na wengine ujima, hawajui effect ya hali ya hewa,rushwa wala utandawazi katika uchumi. Na mbaya zaidi hawajui umuhimu wa vyama vingi na hili linachangiwa na CCM.

    Kwao kikubwa ni mvua inyeshe walime mazao, wakivuna tuu kwao kila kitu kiko sawa. Mara nyingi shida yao kubwa ni njaa na mvua kutonyesha. Kwao Afya bora,Umeme,Elimu bora, uongozi bora,siasa ya ushindani sio vitu vya msingi. Sasa kwa upeo huo CCM itaendelea kushinda unless nyama vya upinzani vifanye operations kubwa ya kutoa elimu uraia.

    Tanzania tukijitambua na uchumi unaweza kukua hata kwa asilimia 8 mpaka kumi.

    ReplyDelete
  12. Baniani muuweni haki yake mpeni, wanacho fanya CCM ni kujikosoa, kujirekebisha na kujisafisha. Wengi ndani ya CCM ni viongozi bora lakini katika msafara wa mamba na kenge wamo! sasa ukishawatambua ukawauliza "kina kenge,mnakwenda wapi"? hii inawezekana ikiwa kwenye chama kuna watu wenye busara.

    CCM wafukuzeni kenge wote ndani ya chama ili safari ya watanzania iwe ya amani.

    ReplyDelete
  13. Hivi kweli Watanzania walioko vijijini ni mbumbumbu kiasi cha wale waishio mijini kuwaona wao hawana elimu wanaishi kwa kudra ya Mwenyezi Mungu tu? Ninasikitika sana kwa Mtanzania awezaye kuona hilo na kuona ya kwamba waishio vijijini hawana wanachojua. Unasahau ya kwamba nyanya, vitunguu, mahindi, mchele, ngongwe nk vinatokana na hawa hawa waishio vijijini wategemeao mvua. Ninafahamu ya kwamba mijini kuna viwanda ambavyo nayvo vinatoa huduma yake kwa watu. Najua hakika ya kwamba nchi yetu bado ipo katika hali mbaya ya uchumi lakini kama zilivyo nchi nyingine uchumi huletwa na watu wa nchi ile wote wakiungana kujenga nchi. Na hata katika nchi zilizo na uchumi mkubwa bado tabaka za watu huwepo. Watakuwepo walio na uwezo mkubwa wenye viwango vya elimu ya juu, kati na chini, wakulima na wafanyakazi na kadhalika. Siungi mkono uongozi wowote mbaya. Namshukru mchangia hoja hapo juu akisema ya kwamba , wengi ndani ya CCM ni viongozi bora lakini katika msafara kuna kenge! Basi kenge hao waondolewe! Hata CHADEMA,CUF nk wapo viongozi bora na kenge pia wamo hilo nalo lisisahaulike. Jamani tujenge nchi yetu kwa amani. Vijijini ndiko kuliko na Watanzania wengi. Wapewe pembejeo, mbolea nk ili mijini nao wasipungukiwe na chakula.

    ReplyDelete
  14. kusema chadema ni chama cha wanyonge si kweli. viongozi wake ni genge la wafanya biashara na ni matajiri watupu. Na wengine wanatumia chama kwa faida yao. Wanabuni operation mpya kila kukicha ili helicopter ipate ajira. Ndio zao. Ruzuku itaishia kulipia deni la helicopter. TUNAJUAAA!!

    ReplyDelete
  15. CCM TUTAAMINI KWAMBA MMEJISAFISHA KAMA MTARUDISHA MALI ZA UMMA MIKONONI MWA WANANCHI VIKIWEMO:-
    1.VIWANJA VYOTE VYA MPIRA MFANO SAMORA,SOKOINE,KIRUMBA,MAJIMAJI,ALLY HASSAN MWINYI NK.AMBAVYO VILIJENGWA KABLA YA 1992.
    2.OFISI ZOTE ZA CCM ZIKIWEMO ZA MIKOA AMBAZO ZILIJENGWA KABLA YA MFUMO WA VYAMA VINGI KUINGIA.
    BILA KUFANYA HIVYO,TUTAENDELEA KUWAITA MAFISADI NA SUBIRINI HUKUMU YENU 2015.

    ReplyDelete
  16. TUNATAKA CCM MTUAMBIE ZILE FEDHA ZA KAMPENI MLIPATA WAPI?AMBAPO MABANGO YA JK YALIBANDIKWA KILA NYUMBA KWA IDADI YA TOFALI ZAKE.WAGOMBEA UBUNGE NA UDIWANI WA CCM NAO VIVYO HIVYO.WANANCHI TUNAJUA ZILIKOTOKA NA NDIO MAANA BAADA YA UCHAGUZI TU!VITU VIKAPANDA BEI BILA SABABU ILI KUZIBA FEDHA MLIZOCHOTA.SUBURINI 2015

    ReplyDelete
  17. Sishangai mtu kukipenda chama fulani lakini tatizo nikwamba nashangaa namna ambavyo wana CCM wanavyoitetea CCM licha ya kwamba mfumo wake mzima umeoza hebu cheki mtiririko huu
    RAISI kapatikana kwa fedha za wizi na Rushwa
    Wabunge wamepatikana kwa rushwa kuanzia katika mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM,
    Sitarajii kama chama kitakuwa na sababu ya kuwatoa kafara wachache wakati mfumo mzima wa chama umejaa rushwa.

    ReplyDelete
  18. Mtoa maoni 2.46 AM unahoji pesa za mabango CCM ilizipata wapi?
    1. Mitambo ya IPTL iliamriwa iwashwe wakati mvua zikiwa mlangoni
    2. Hakuna pesa za mafao kwenye funds za akiba ya wastaafu e.g. PSPF, NSSF, PPF (list inaendelea. Wazee wa watu waliostaafu kuanzia mwaka jana 2010 hawajalipwa stahiki zao hadi leo. Wanaendelea kuzungushwa wakiambiwa kuna tatizo hili na lile. Kumbe pesa hakuna - zilifanyia kampeni na nyingine kujenda UDom kwa mbwembwe za kutafutia kujipendekeza wananchi waipende CCM
    3. Pesa za ruzuku ya kukwamua uchumi wakati ule wa mtikisiko wa uchumi hazikupelekwa kulikostahili. Zilielekezwa kwenye mabango
    4. Pesa zilichotwa hazina - nyingi tu.

    Sasa wewe unauliza majibu?

    ReplyDelete
  19. ELIMU YA MJINGA NI MAJUNGU ASIYEONA UBAYA WA CCM NAE KAFAIDIKA NAYO HAKIKA WATAZANIA YATUPASA KUBADILIKA WAKATI NI HUU.NDUGU ZANGU.

    ReplyDelete
  20. WATU WANAINGIA MIKATABA AMBAYO NI YA KINYONYAJI LEO MTU ANASEMA ETI HIKI CHAMA KIKO MAKINI? WE NEED CHANGE MBONA WATANZNIA HATUJIAMINI UWOGA HUU UMETAKA WAPI? JE NI ELIMU FINYU AU NI NINI?

    ReplyDelete
  21. HATUDANGANYIKE NG'OOO, KAMA UMETUMWA BASI UMEKOSEA NJIA. TANGU LINI CCM IMEJALI MASLAHI YA WANANCHI, AU WEWE UNAISHI NCHI GANI USIYEWEZA KUONA YANAYOTENDWA NA BABA ZAKO CCM. UKWELI NI KWAMBA CCM IMEOZA. USITUPOTOSHE

    ReplyDelete
  22. HAMNA MAANA HATA CHEMBE,NJAA INAWASUMBUA WAKATI WENZENU WANAOTAWALA NA WAPINZANI VIONGOZI WAO WANATAFUNA MAMILIONI YA WALALAHOI.

    ReplyDelete