17 April 2011

Bandari Saccos yatakiwa kujipanua zaidi

Na Charles Lucas

KATIBU Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bw. Julius Kashuliza amesema vyama vya kuweka na kukopa maeneo ya kazi kikiwamo cha Bandarini Saccos lazima vijitanue zaidi kupata wanachama walio nje ya ajira ya ili kujijengea uwezo wa kiuchumi.

Akizungumza wakati wa semina ya siku moja ya kuwajengea uwezo wanachama wa Bandarini Saccos Dar es Salaam jana, alisema ile dhana kuwa vyama vya kuweka na kukopa haviwezi kuwahusisha watu walio nje ya ajira ni potofu kwani kinakifanya chama husika kudumaa kwa kukosa wanachama walio wengi ambao ni wajasiriamali.

Naye Mwakirishi kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Julius Masota alisema BoT itakuwa tayari kutoa ushauri wa hali na mali ili kuviendeleza vyama kama Bandarini Saccos vinavyoonesha uwezo wa kundesha shughuli zake kwa mujibu wa taratibu za fedha ili kujenga uchumi.

Katika semina hiyo mada kadhaa zilijadiliwa katika kuboresha uendeshaji wa vyama vya ushirika ikiwamo hatima ya mwanachama wa Saccos anapostaafu mada iliyowavutia wengi wakiuliza maswali ya kujua hatima yao na nafasi waliyonayo kwa wakati huo.

Madsada nyingine iliyojadiliwa ni uendeshaji wa Saccos kwa utaratibu wa kibenki na utawala kifedha katika kutumia kanuni za fedha kuepuka ubadhirifu mada ambayo pia ilichangiwa na wanachama wengi

Katibu Mtendaji wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (SCCULT) Bw. Habibu Mhezi alisema ni vema wanachama kuwa makini katika kipindi wanachokuwa katika ajira ili kuchangia zaidi katika vyama hivyo ili kujiwekea akiba kwani huo ndio mwanzo wa maisha bora baada ya kustaafu.

Akitoa shukrani kwa wageni, Wanachama na wadau mbalinmbali walioshiriki kwa namna moja au nyingine kufanikisha semina hiyo Mwenyekiti wa Saccos hiyo Bi. Stella Mtayabarwa alisema Bandarini Saccos itajikita katika kuboresha huduma zake ili iwe mfano kwa vyama vingine pia itaandaa mazingira ya kujitanua zaidi ili iwe taasisi kubwa ya kufedha na kuwanufaisha wanachama wake.

No comments:

Post a Comment