Na Suleiman Abeid, Shinyanga
BARAZA Kuu la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani Shinyanga limemteua Bw. John Magale Shibuda kuwa mwenyekiti wa muda wa mkoa
huo kufuatia kifo cha Bw. Philipo Shelembi.
Akitangaza uamuzi huo muda mfupi kabla ya shughuli ya kuanza shughuli za kuaga
mwili wa marehemu Bw. Shelembi katika uwanja wa michezo ya Shycom mjini Shinyanga, Katibu wa Mkoa wa CHADEMA, Bw. Nyangaki Shilungushela alisema uamuzi huo ulifikiwa katika kikao cha dharura kilichofanyika juzi jioni.
Bw. Shilungushela alisema kufuatia kifo cha Bw. Shelembi ambaye alikuwa mwenyekiti wa mkoa wa CHADEMA Shinyanga, wajumbe wa baraza la mkoa waliketi katika kikao cha dharura na kumteua Bw. Shibuda kuwa mwenyekiti wa muda wa mkoa huo mpaka pale uchaguzi wa kujaza nafasi yake utakapofanyika.
“Mbali ya kumteua Bw. Shibuda kuwa mwenyekiti wa muda wa mkoa, lakini pia wajumbe wa baraza kuu la mkoa walimpendekeza kuwa mlezi wa mkoa wa Shinyanga, na atakaimu nafasi ya uenyekiti mpaka pale utakapofanyika uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi iliyoachwa na Bw. Shelembi,” alieleza Bw. Shilungushela.
Akitoa salaam zake wakati wa shughuli za uagaji wa mwili wa marehemu, Bw. Shibuda alisema katika kipindi chake kukaimu nafasi ya mwenyekiti wa mkoa atakuwa mstari wa mbele katika kuendeleza mapambano ya kutetea haki za wanyonge yaliyokuwa yameanzishwa na Bw. Shelembi.
Alisema wapo baadhi ya wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wanaoamini kuwa kifo cha Shelembi ndiyo mwisho wa mapambano ya wana CHADEMA kudai haki za wanyonge na kwamba fikra hizo ni sawa na fikra mgando.
“Ndugu zangu, ndugu yetu Shelembi pamoja na kututoka ghafla, lakini kifo chake siyo mwisho wa kupigania haki za wanyonge, napenda niwahakikishieni kuwa nitahakikisha naendeleza yale yote mazuri aliyokuwa akiyapigania kwa niaba ya wananchi wa Shinyanga.
“Pia napenda kuwaomba madiwani wote wa manispaa ya Shinyanga bila kujali itikadi za vyama vyao wahakikishe wanamuenzi mheshimiwa Shelembi kwa kuendeleza utetezi wa wanyonge na wafanyabiashara ndogondogo kama alivyokuwa akiwatetea,” alisema.
Alisema Bw. Shelembi hakuwa mtu wa kutangatanga katika maamuzi yake, alikuwa daimu muwazi, umasikini wake wa fedha haukumfanya kuwa masikini wa busara na fikra, japo kuwa kwa kawaida ukweli una tabia ya kuudhi masikio ya watu dhulmati.
Wakati huo huo Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Zanzibar, Bw. Said Issa Mohamed aliwaacha hoi waombolezaji 'Shelembi yuko hai' na kinachosubiriwa ni kufanyika kwa uchaguzi mwingine ili apatikane mbunge halali.
Bw. Mohamedi alisema umati wa watu waliohudhuria katika kuuaga mwili wa marehemu na kushiriki mazishi yake umethibitisha wazi kuwa Bw. Shelembi ndiye aliyekuwa ameshinda uchaguzi katika nafasi ya ubunge wa jimbo la Shinyanga mjini.
Marehemu Shelembi alifariki ghafla juzi alfajiri katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga alikokimbizwa baada ya kuugua kwa muda mfupi akisumbuliwa na tatizo la shinikizo la damu, kiharusi na malaria kali.
Mazishi yake yalihudhuriwa na viongozi wote wakuu wa CHADEMA Taifa, wakiongozwa na mwenyekiti wa Taifa, Bw. Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, Dkt. Willibrod Slaa, Naibu Katibu Mkuu, Bw. Zitto Kabwe, Makamu Mwenyekiti (bara), Bw. Said Arfi na yule wa Zanzibar Bw. Mohamed.
Mungu anajua yote. habari za kuaminika ni kuwa marehemu shelembi alilalamika mtu kampiga mkuki wakati amepanda pikipiki..na kuanzia hapo ndio akaugua ghafla hadi umauti....
ReplyDeletepengine hiyo ndiyo njuia ya kisayansi giza kufunga kesi dhidi ya steven masele ambaye alikuwa anaelemewa.......
daaah CCM bwana wee acha tuu... ukishawakuta wamekalia ngozi wanapuliza hapo hutoki...!!
ReplyDelete