28 April 2011

Kikwete ateua katibu mkuu, manaibu 10

Na Mwandishi Maalumu

RAIS Jakaya Kikwete amefanya uteuzi wa Katibu Mkuu mmoja wa Wizara na Naibu Makatibu Wakuu 10 wa Wizara mbalimbali.Aidha, Rais Kikwete amemhamisha
Naibu Katibu Mkuu mmoja kutoka Wizara moja kwenda nyingine.

Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam na Kaimu Katibu Mkuu Kiongozi, Bw. George Yambesi jana, ilisema kuwa uteuzi huo wa maofisa hao waandamizi wa serikali unaanzia Alhamisi iliyopita na wataapishwa kesho saa sita mchana.

Katika uteuzi huo, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Bw. Job D. Masima ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo.

Vile vile Rais Kikwete amemhamisha Injinia Mbogo Futakamba aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji kwenda Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika.
 
Naibu Makatibu Wakuu walioteuliwa na Mheshimiwa Rais ni kama ifuatavyo Bw. Aphayo Kidata ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Ikulu. Kabla ya uteuzi wake, Bw. Kidata alikuwa Mkurugenzi wa Sera na Mipango katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Bw. Hab Mkwizu ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Kabla ya uteuzi wake, Bw. Mkwizu alikuwa Karani wa Baraza la Mawaziri.

Bw. Charles Amos Pallangyo ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu. Kabla ya uteuzi huo, Bw. Pallangyo alikuwa Mkurugenzi wa Uratibu – Ofisi ya Waziri Mkuu.

Bibi Mwamini Juma Malemi ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Kabla ya hapo alikuwa Msaidizi wa Makamu wa Rais katika masuala ya Maendeleo ya Jamii na Uratibu wa Malalamiko ya Jamii na Uratibu wa Malalamiko ya Wananchi.

Injinia Mussa Ibrahim Iyombe ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu katika Wizara ya Ulinzi na JKT. Kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkurugenzi wa Miundombinu ya Usafiri katika Wizara ya Ujenzi.

Injinia John Ndunguru ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu katika Wizara ya Ujenzi. Kabla ya hapo, alikuwa Mkurugenzi wa Huduma na Ufundi katika wizara hiyo.

Bw. John Mngodo ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu katika Wizara ya Uchukuzi. Kabla ya uteuzi wake alikuwa Mkurugenzi wa Usalama wa Chakula.

Bi. Anna Maembe ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu katika Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Kabla ya uteuzi wake, Bi. Maembe alikuwa Mkurugenzi wa Mazingira na Habari wa NEMC.

Bi. Sihaba Nkinga ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu katika Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo. Kabla ya hapo alikuwa Mkurugenzi wa Sera na Mipango katika Wizara ya Uchukuzi.

Injinia Bashir Mrindoko ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu katika Wizara ya Maji. Kabla ya uteuzi wake, Bw. Mrindoko alikuwa Kamishna wa Nishati na Mafuta ya Petroli.

1 comment:

  1. Huyu Bashiru Mrindoko si yule wa Richmond? Kweli CCM imevua Gamba au!

    ReplyDelete