28 April 2011

Mbatia kulipa mil. 9/- kumpinga Mdee

Na Rehema Mohamed

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imewataka walalamikaji katika kesi ya kupinga uchaguzi iliyofunguliwa na Mwenyekiti wa chama cha NCCR-Mageuzi, Bw. James
Mbatia na wenzake dhidi ya Mbunge wa Jimbo la Kawe Bi. Halima Mdee kulipa jumla ya sh. milioni 9 kama gharama ya dhamana ya kesi hiyo.

Uamuzi huo umetolewa jana na Jaji wa Mahakama hiyo, Bw. John Utamwa wakati kesi hiyo ilipofikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.

Bw. Utamwa alisema kuwa kila mlalamikaji atatakiwa kulipa sh. milioni 3 kwa kila mshtakiwa badala ya milioni 5/- kama sheria inavyosema. Wanaoshtakiwa katika kesi hiyo, ni Bi. Mdee, Msimamizi wa Uchaguzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Awali Bw. Mbatia aliiomba mahakama hiyo impunguzie kutoka sh. milioni 5 na badala yake alipe milioni moja kwa kila mshtakiwa kama dhamana ya kesi hiyo na wenzake kuomba kusamehewa kulipa fedha hizo, ambapo Bw. Utamwa alisema maombi hayo hayakuonesha sababu ya msingi ya kuwa hawana uwezo wa kulipa dhamana iliyopangwa kisheria.

Alisema kuwa mawakili wa pande zote mbili walionesha nia ya kupunguzwa kwa kiasi hicho cha fedha za dhamana ambapo walipanga walalamikaji walipe kati ya sh. milioni 1 hadi 2.5.

Alisema kutokana na maombi yaliyowasilishwa kwake aliamua kupanga kiasi cha sh. milioni 3 kwa kila mlalamikaji kama malipo ya dhamana ya kesi hiyo.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 17, mwaka huu itakapotajwa tena ambapo kiasi hicho cha fedha kinahitajika kulipwa kabla ya tarehe hiyo, ili iendelee kusikilizwa.

Bw. Mbatia kupitia mawakili wake, Bw. Mohamed Tibanyendera na Bw. Aloyce Komba, Novemba 25, mwaka jana walifungua kesi ya madai namba 111 kupinga matokeo ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 31, mwaka jana yaliyompa ushindi Bi. Mdee.

2 comments:

  1. Mbona Mhe. Mbatia ulisema wapinzani muache malumbano na mjenge nchi kwa faida na mustakabali wa watanzania; Je hilo (kesi) halimo ktk orodha ya kuacha malumbano na utata wa kufanyiana visa wenyewe kwa wenyewe?.

    Hivi karibuni umetoa mawazo mazuri wkt wa kujadili katiba hadi watu wamekuona una upeo mkubwa na uungwana wa kujali maslahi ya Taifa; tunakuomba wana NCCR tulioona heshima yako ilivyopanda ktk kujadili hoja za muungano na katiba zimekupa heshima kubwa, achana na hilo ni dogo na halina maana kwa sasa litakuvurugia credit uliyopata kuliko viongozi wengine wote.

    umekwisha kula plau na biriani nzuri, usijiburudishe kwa uji badala ya kinywaji baridiiiii (soft drink).

    ReplyDelete
  2. Hiro riMbatia naro wakati mwingine rinalopoka ovyo, wakati mwingine rinasema mambo ya busala. Harimuwezi Harima Mdoe kwa fire arichaguriwa kwa kula mingi sa wanchi wa huko Kawe. Wewe mbatia riria tu rakini usijalibu kumunyoshea Harima kidore.

    ReplyDelete