08 April 2011

Shein aongoza hitma ya Karume

Na Mwandishi Wetu

RAIS wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein jana aliongoza hitma ya kumuombea dua Rais wa Kwanza wa Zanzibar Marehemu Abeid Amani Karume, iliyofanyika katika
Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui mjini Zanzibar.

Hitma hiyo pia, ilihudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, pamoja na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, Rais Msataafu wa Jamhuri ya Muungano Ali Hassan Mwinyi na wanafamilia ya Mzee Karume.

Wengine ni viongozi wa serikali zote mbili na viongozi wastaafu, viongozi wa vyama vya siasa, mashekhe kutoka Zanzibar na Tanzania Bara, wabunge na wawakilishi pamoja na mabalozi wadogo waliopo hapa Zanzibar.

Hitma hiyo ilitanguliwa na Qur-an tukufu Suratul Fuswilat, iliyosomwa na Ustadh Sharif Abdulrahman na kuongozwa na Shekhe Mohammed Kasim kutoka Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Zanzibar.

Mara baada ya hitma hiyo, Shekhe Thabit Noman Jongo alitoa mawaidha na kumuelezea marehemu Karume kuwa ni kiongozi aliyewatetea wanyonge na aliyepigania maendeleo ya wananchi wa Zanzibar.

Alieleza kuwa katika uongozi wake, marehemu Karume aliwajali watu wote kwa nafasi zao wakiwemo wazee, vijana, walemavu, wavuvi na watoto mayatima ambapo pia alifanya juhudi za kuhakikisha wote hao wanaishi katika mazingira bora.

“Aliyoyafanya mzee Karume sisi hatuna cha kumlipa isipokuwa ni kumuombea dua Mungu amlaze mahala pema peponi, Amin,” alisema Shekhe Jongo.

Aidha, Shekhe Jongo alieleza kuwa juhudi za viongozi waliotangulia ndizo zinazosababisha hadi leo Zanzibar kupata maendeleo makubwa na kusisiti za kuwa Zanzibar ni njema atakaye aje.

Viongozi wengine ambao pia, walihudhuria katika hitma hiyo ni Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Devis Mwamunyange, mwakilishi wa familia ya Baba wa Taifa hayati Mwalimu Nyerere, Madaraka Nyerere, Jaji Mkuu mstaafu, Augustino Ramadhan, mzee Kingunge Ngombale-Mwiru, Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Shekhe Khamis Haji, Naibu Mufti Mkuu, Shekhe Saleh Omar Kabhi na Shekhe Mussa Salum kutoka Mkoa wa Dar-es-Salaam

Baada ya kisomo hicho cha hitma ambacho hufanyika kila mwaka Aprili 7, viongozi hao na wananchi walimuombea dua, marehemu  Karume katika kaburi lake lililopo pembezoni mwa ofisi hiyo.

No comments:

Post a Comment