20 April 2011

Serikali yajitutumua kudhibiti mishahara hewa

Na Waandishi Wetu, jijini

SIKU chache baada ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) kutaja halmashauri ambazo anadai kuwa ni vinara wa mishahara hewa, serikali imetangaza vita na watumishi wa
umma wasio waaminifu waliobainika kujichotea mishahara hewa ya wafanyakazi waliokufa.

Akizungumza juzi katika kipindi maalumu kinachorushwa na kituo cha televishen cha ITV, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti na Utumishi, Bi. Hawa Ghasia, alisema wale wote waliotumiwa nafasi zao kazini kwa kujichotea fedha hizo atahakikisha wanaburuzwa mahakamani kujibu mashtaka hayo.

Alisema ili tabia hiyo ikomeshwe uchunguzi wa kina umefanywa ambapo taratibu za kuwafikisha mahakamani zinafanyika.

Aliongeza kuwa uchunguzi wao umebaini kuwa ulipaji mishahara hewa limekuwa tatizo sugu kutokana na wafanyakazi kuhamishwa vituo na wengine kuacha kazi ambapo waajiri hushindwa kutoa taarifa wizarani ili mishahara hiyo isitishwe.

“Kutokana na hali hiyo, mishahara hewa imeendelea kutolewa huku waajiri wakiendelea kujineemesha na baadhi yao kupata mishahara mara mbili,” alisema Ghasia.

Alisema kitendo hicho wamechoka nacho na kamwe hawawezi kuendelea kulifumbia macho, hivyo watumishi watakaobainika hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Pia serikali imeendelea kupata hasara kutokana na waajiri wazembe ambao wamekuwa wakishirikiana na ndugu kuendelea kuneemeka kwa kupata mshahara pindi mtumishi anapokufa.

Ghasia alisema ndugu yoyote ambao wamewahi kujichotea fedha za ndugu zao waliofariki warejeshe haraka fedha hizo ama sivyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

“Serikali imepoteza mamilioni ya fedha kutokana na uzembe huo katika maeneo mbalimbali ya nchi na bado uchunguzi unaendelea, hivyo kwa wale wanaojiona kuwa wameingia kwenye mtego huu waache na waliozichukua wazirejeshe haraka,” alisema.

No comments:

Post a Comment