20 April 2011

Idd Azzan atishiwa kunyanganywa kadi

Na Anneth Kagenda

MBUNGE wa Jimbo la Kinondoni, Bw. Idd Azzan amelalamika kuwa kuna watu ndani ya chama hicho mkoa wa Dar es Salaam wamemtishia kumnyanganya kadi
yake uanachama, jambo ambalo halimtishi.

"Kuna mtu mmoja aliniambia kwamba tutakunyanganya kadi yako ya uanachama kwa madai kuwa ninataka Sekretarieti ya CCM Mkoa na Kamati ya Siasa ijivue gamba, hata wakiitaka leo nitawapa lakini ni lazima tuseme ukweli ili kukinusuru chama chetu," alisema.

Hayo aliyasema Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake juu ya kuweka msisitizo kwamba hababaishwi na maneno ya baadhi ya watu pale anapotaka kusema ukweli ndani ya CCM kwa nia ya kukinusuru chama.

Alisisitiza kwamba Sekretarieti ya Mkoa na Kamati ya Siasa lazima ijiuzulu ili chama kiweze kujipanga na kujiwekea mikakati endelevu ya kushika dola bila kukumbwa na kashfa za hapa na pale zinazoendelea ndani na nje ya chama.

"Sekretarieti ya Mkoa inanitisha eti kwanini nilisema wajivue magamba, wananiambia watanionyesha, lakini mimi ninachoamini ni kwamba pale ukweli unaposemwa wazi wazi bila kificho huwa unauma lakini lazima tuuseme kila wakati.

"Viongozi wa Mkoa wamegawanyika katika makundi mawili ambayo yamechangia kwa asilimia kubwa kukidhorotesha chama tangu mwaka 2007. Yaliwaengua madiwani wa Kata na wale wa viti maalumu waliokuwa wakipendwa na wananchi, na kusababisha wananchi kuvipigia kura vyama vya pinzani," alisema.

Aidha alisema kuwa Aprili 14, mwaka huu Katibu wa CCM Mkoa, Bw. Kilumbe Ng'enda aliitisha kikao cha makatibu kata na madiwani na kuwaambia kwamba hajivui magamba ng'o na kusema kuwa alitakiwa kujibu kwa hoja siyo blabla.

Bw. Azzan aliongeza kwamba nia yake ya kutaka sekretarieti hizo zijiuzulu ni kutokana na kwamba kuna mambo mengi ambayo yamekuwa yakifanyika kimakosa ikiwa ni pamoja na viongozi hao kutotaka kuitisha mikutano ambayo watu watatoa dukuduku zao za namna ya kuboresha na kukiendesha chama.

"Tulikuwa tunatakiwa kufanya vikao tangu Novemba au Desemba lakini cha kushangaza mpaka leo hatujafanya kikao chochote, je, ni kwanini hawataki vikao hivyo vifanyike?.

"Sasa mimi ninasema kwamba wasipofanya vikao hivyo ndani ya mwezi huu ili viongozi watoe dukuduku lao juu ya kilichosababisha CCM kushindwa kufanya vizuri kwenye uchaguzi uliopita, nitaitisha mkutano na waandishi wa habari na kuyaanika yale yote waliyoyafanya mpaka chama kikapoteza majimbo mawili na kata nyingi," alisema.

4 comments:

  1. Sema IDD AZZAN wananchi tunasubiri magamba ya CCM tuyaone.

    ReplyDelete
  2. CCM JIDHIBINI KUKIMBILIA VYOMBO VYA HABARI.MALUMBANO HAYAWASAIDII KITU ZAIDI YA KUKIDHOOFISHA CHAMA.CHAMA CHENU KIMEKUWA HAKINA NIDHAMU KUTOKANA NA KUPOKEA VIONGOZI/WANACHAMA NDANI YA CHAMA KWA NJIA ZISIZO SAHIHI NA WASO NA SIFA

    ReplyDelete
  3. Njoo CUF! wasikuzingue.

    ReplyDelete
  4. Sekretariati ya DSM, hiyo jeuri ya kung'ang'ania gamba wamepewa na mapacha watatu. Ila wanacheza makida makida, waendelee na kidali poo...HAWAONI SABABU YA UFISAFI..WAMECHAFUKA HADI DAMUNI

    ReplyDelete