Na Zahoro Mlanzi
ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Klabu ya African Lyon, Jamal Kisongo ameanika ukweli kuhusu sakata la mshambuliaji Mbwana Samatta kwa kusema aliyekuwa Katibu
wake, Jeshi Zakaria ndiye anayekuza mjadala huo wakati ukweli wa mambo anaujua.
Mbali na hilo, Kisongo alisema bado kuna mambo matatu ya msingi hawajamalizana na TP Mazembe ambayo yatamalizwa baada ya mchezo kati ya timu ya taifa ya vijana na Uganda 'The Kobs', ambapo watakwenda Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC).
Akizungumza Dar es Salaam jana, Kisongo alisema anashangazwa na Zakaria ambaye jambo hilo analijua kwa undani na alikuwepo wakati, Samatta akisaini mkataba wa kwenda Simba.
"Mimi nashangaa kila kukicha suala la Samatta katika vyombo vya habari, naomba mmuulize vizuri Jeshi Zakaria kwa kuwa suala hili analijua kwa undani na siku ya kusaini mkataba tulikuwa naye pale Magomeni pamoja na Makamu wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu," alisema Kisongo.
Alisema mchezaji huyo kuendelea kuandikwa kila kukicha, kutamfanya achanganyikiwe na kiwango chake kushuka wakati kuna mtu anajua kila kitu kuhusu hilo.
"Mimi nilitegemea kuona African Lyon wakidai fedha, lakini kukanusha kwamba Samatta si mchezaji wa Simba hapo wanakosea, huyo ni mchezaji halali, ninachowaomba wafuate taratibu za malipo yao kwa Simba," alisema Kisongo.
Wakati huo huo, Kisongo alisema mchezaji huyo ataondoka kwenda Lubumbashi hivi karibuni kwani kuna mambo ya msingi hayajamalizwa kati ya Simba, TP Mzembe na wakala wa mchezaji huyo, Damas Ndumbaro.
"Mimi ni mtu wa karibu sana wa Samatta na ndiye ninayempa ushauri kwa kila kitu, hata TP Mazembe walipokuja nchini kumsainisha nilikuwepo na nikawa shahidi wa makubaliano hayo, hivyo najua kila kitu kuhusu Samatta," alisema Kisongo.
Alisema Simba bado hawajamalizana na TP Mazembe, kuhusu muda atakaocheza soka huko ambapo mabingwa hao wa Afrika wao wanataka asaini miaka mitano na hawajaafikiana nani atakuwa na haki ya kuzungumzia suala lake itakapotokea ameuzwa klabu nyingine na pia suala la malipo ya bonus.
Kisongo alisema maandalizi ya safari ya mchezaji huyo kwenda Lubumbashi, yameshakamilika na Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Sunday Kayuni ametoa baraka lakini mpaka amalize mechi ya Jumamosi kutokana na umuhimu wake katika kikosi hicho cha vijana.
No comments:
Post a Comment