Na Grace Michael
MUUGUZI wa Hospitali ya Hindu Mandal ya Dar es Salaam, Bi. Mastidia Anjelo (46) anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumuua mtalaka wake ambaye amezaa naye
watoto watatu.
Marehemu huyo Deus Malima (42) aliuawa Jumapili saa 5.00 usiku katika maeneo ya Mbezi Juu wakati alipokwenda kwa Bi. Anjelo kwa lengo la kutaka kuwachukua watoto wake.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Bw. Chaeles Kenyella alisema kuwa mwanamke huyo anashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za mauaji ambapo anadaiwa kumpiga marehemu na kitu kizito kisogoni na pia kumchoma na kitu chenye ncha kali kwenye paji la uso, hatua iliyosababisha kifo chake.
"Mtuhumiwa baada ya tukio hilo, alikwenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi cha Kawe kuwa kuna mtu kafa nje ya nyumba yake lakini baada ya polisi kufuatilia ilibainika kuwepo kwa mauaji hayo na mtuhumiwa alitiwa mbaroni kwa hatua za kisheria," alisema Bw. Kenyella.
Katika tukio jingine, alisema kuwa jeshi hilo limefanikiwa kukamata silaha aina ya bastola ikiwa na risasi saba ambayo iliibwa ndani ya gari la Bw. Mohamed Rweyemamu (53) wakati akiwa ameegesha katika maeneo ya Mbezi Beach.
Kamanda Kenyella alisema kuwa wakati gari hilo likiwa limeegeshwa, ndani ya gari kulikuwa na mke wa Bw. Rweyemamu, ghafla alitokea mtu mmoja ambaye ni mwanaume na kunyakua begi ambalo ndani yake kulikuwa na bastola, hati ya kusafiria na vitu vingine kisha kutokomea nayo.
"Bastola hiyo ilipatika kutokana na taarifa kutoka kwa wasiri wa jeshi kuwa aliyehusika na wizi huo ni mtu mmoja aliyetajwa kwa jina moja la Dulla ambaye ni mkazi wa Magomeni na katika msako wa polisi mtuhumiwa huyo akiwa Coco Beach na askari wakiwa wanamfuatilia alitupa chini mfuko wa rambo na kukimbia, na mfuko ulipekuliwa kulikuwa na bastola hiyo na hati ya kusafiria," alisema Kamanda.
Kutokana na hali hiyo, Kamanda Kenyella alitoa tahadhari kwa wamiliki wa silaha kuwa makini nazo kwa kuwa zinaweza kuangukia mikononi mwa wahalifu huku akisisitiza kuwa watakaozembea katika hilo watachukuliwa hatua zaidi.
Akizungumzia matukio ya makosa ya usalama barabarani, alisema kuwa kuanzia Aprili Mosi hadi 24, mwaka huu jumla ya magari 765 yamekamatwa kutokana na makosa mbalimbali ya usalama barabarani ambayo ni daladala 424 wakati magari mengine na pikipiki zikiwa 341.
Alisema magari hayo yamesababisha jumla ya makosa 1,528 ambapo faini iliyopatikana kutokana na makosa hayo ni sh. milioni 30.5 hivyo akatumia mwanya huo kuwataka madereva kufuata sheria za barabarani.
No comments:
Post a Comment