Na Mwali Ibrahim
BONDIA Mbwana Matumla, amefanya vyema katika mapambano yake ya majaribio baada ya kuwapiga mabondia Issa Sewe, Omari Bayi na Said Hofu lililofanyika
katika Ukumbi wa Panandipanandi, Dar es Salaam juzi.
Ushindi huo utakuwa umempa nguvu bondia huyo la kumpiga mpinzani wake kutoka Kenya, Gabriel Ochieng ambaye atapambana naye Mei Mosi mwaka huu katika Ukumbi wa PTA.
Akizungumza Dar es Salaam juzi mratibu wa pambano hilo, Rajab Mhamila 'Super D' alisema Mbwana ameweza kuonesha uwezo mkubwa katika mapambano dhidi ya mabondia hao, ambapo aliweza kumtwanga Omari Bayi katika raundi ya pili huku akioneshana ubabe na Issa Sewa na Said Hofu hadi raundi ya mwisho.
Alisema mapambano hayo yalikuwa ya raundi nne ambapo, Mbwana sambamba na kuyatumia kama maaandalizi yake ya mwisho ya pambano lake la ubingwa wa UBO dhidi ya Ochieng la uzito wa Kg. 55 la raundi 12, pia alikuwa akitoa hamasa kwa mabondia wa Ilala kuupenda mchezo huo.
Super D alisema kutokana na uwezo aliouonesha, bondia huyo ana nafasi kubwa ya kuchukua ubingwa katika pambano lake la Mei mosi kwani ameonekana kuiva.
Kwa upande wake, Mbwana alisema anajiona yupo katika nafasi nzuri kiushindani na kuahidi kutetea vyema mkanda wake alioutwaa mwaka jana.
Pambano hilo litasindikizwa na mapambano mengine ya utangulizi kati ya bondia Ambukile Chusa atakayedundana na Emmanuel Kayala katika uzito wa kg. 69, Faraji Magia atazichapa na Issa Sewe uzito wa kg. 61 na Omari Zungu watazikunja na Fadhili Awadhi uzito wa kg. 59.
Mabondi wengine watakaosindikiza ni Said Momba ambaye atapigana na Jumanne Mapombe uzito wa kg. 57, wakati Fadhili Magia ataoneshana kazi na Kijepa Omari katika uzito wa kg. 52 na John Mbwana atambana na Ally Mahiyo katika uzito wa kg. 49 ambapo mapambano yote yatakuwa katika raundi nne.
No comments:
Post a Comment