Na Peter Mwenda
MAZISHI ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli nchini (TRAWU) Bw. Silvester Rwegasira aliyefariki dunia ghafla kwa ugonjwa wa moyo juzi, anatarajiwa
kuzikwa leo kwenye makaburi ya Kinondoni.
Mwenyekiti wa TRAWU, Bw. Bakari Kiswala alisema jana Dar es Salaam, kuwa taratibu za mazishi ya marehemu Rwegasira zinafanyika nyumbani kwake ghorofa za TAZARA na mwili ya marehemu utaagwa kuanzia saa 5 asubuhi.
Bw. Kiswala alisema wafanyakazi wa Shirika la Reli Tanzania (TRL) na wale wa Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) na waombolezaji wengine wataanza kutoa heshima zao za mwisho saa 5 asubuhi mpaka saa 7 mchana.
Alisema shughuli za kuaga mwili wa marehemu zitafanyika katika stesheni ya Tazara na baadaye safari ya kwenda makaburini itaanza.
Alisema ibada ya kumuombea marehemu itafanyika Tazara ikiendeshwa na Paroko wa Kanisa Katoliki Chang'ombe, ambayo itakwenda sambamba na kuaga mwili wa marehemu.
Bw. Kiswala alisema marehemu Rwegasira alikuwa mfanyakazi wa TAZARA kabla ya kuazimwa na TRAWU miaka minane iliyopita kufanya kazi ya Katibu Mkuu wa chama hicho wadhifa aliokuwa nao hadi anafariki.
Bw. Rwegasira alifariki dunia Hospitali ya Dar Group baada ya kulazwa kwa muda mfupi akisumbuliwa na ugonjwa wa moyo na mwili wake kuhamishiwa Hospitali ya Amana.
No comments:
Post a Comment