06 April 2011

Mfumo wa kukopesha wanawake, vijana wapondwa

Na Mwandishi Wetu

MWONGOZO wa serikali juu ya kutoa mikopo kwa wanawake na vijana kwa kutumia mapato ya halmashauri umedaiwa kuwa haufai, umepitwa na wakati na
usiofanikisha malengo ya kupunguza umaskini wala kutengeneza ajira.

Imedaiwa kuwa mwongozo huo, ambao ulitolewa na iliyokuwa Wizara ya Maendeleo ya Vijana, Michezo na Utamaduni, siku za nyuma, unahitaji kuboreshwa ili uendane na wakati uliopo hasa katika vita dhidi ya umaskini, ili kufikia Malengo ya Maendeleo ya Milenia na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025. 

Hayo yalisemwa jana na Diwani wa Viti Maalumu katika Wilaya ya Karatu, Bi. Cecilia Peresso alipozungumza na Majira juu ya majibu aliyopewa baada ya kuwasilisha hoja yake binafsi aliyoiwasilisha katika Kikao cha Baraza la Madiwani, hivi karibuni.

Katika hoja hiyo, Bi. Paresso alitaka majibu kwa takwimu angalau kwa miaka minne, mpaka sasa, jinsi mikopo hiyo inavyotolewa na kwa namna gani walengwa wamenufaika nayo.

Pia alitaka kujua mazingira na vigezo vinavyozingatiwa, huku pia akihoji kiasi cha mikopo kilichotolewa kwa vijana na wanawake kwa mwaka huu wa fedha, akiomba apewe majina ya vikundi na mahali vilipo.

"Nimeridhika na majibu niliyopata na nimefuatilia kuhakikisha. Tatizo linaonekana liko katika mwongozo wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.

"Mwongozo huo kwa kweli haufai na umepitwa na wakati, bado unazungumzia kuwakopesha wanawake walioko katika kikundi cha watu watano wakopeshwe shilingi laki tano na warudishe riba ya asilimia 10 na mkopo wenyewe, mwezi wa tatu tangu kuanza kwa shughuli za kikundi.

"Vijana wao wanatakiwa kuwa katika makundi ya watu watatu au wawili, utaratibu huu ubadilishwe, laki tano si lolote wala chochote, haiwezi kupunguza vikwazo vya umaskini vinavyowakabili wanawake na vijana katika wakati huu, fedha hiyo iongezwe au kama haiwezekani basi riba ipunguzwe," alisema Bi. Paresso.

No comments:

Post a Comment