06 April 2011

Ajali zaua 10 Morogoro

Na Ramadhan Libenanga, Morogoro

WATU 10 wamefariki dunia na wengine 12 kujeruhiwa vibaya katika ajali tatu tofauti zilizotokea mkoani Morogoro ikiwemo ya basi la Sumry kugongana uso kwa uso na
gari ndogo katika maeneo ya Maseyu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro (ACP), Adolphina Chialo alisema kuwa ajali hiyo ilitokea saa 12:45 katika eneo la Maseyu Wilaya ya Morogoro.

Kamanda Chialo alisema kuwa gari lenye namba T 924 AHJ Nissani Pick-Up likiendeshwa na Athumani Mustafa (34) mkandarasi na mkazi wa Keko Dar es Salaamu iligongana na basi la Sumry lenye namba za usajili T 608 BEW likitoka Mwanza kwenda Dar es Salaam na kusababisha vifo vya watu watatu waliokuwa katika gari ndogo akiwemo dereva huyo wa Pick-Up.

Aidha Kamanda aliwataja waliokufa katika ajali hiyo kuwa ni Yohana Hamis (37) mkazi wa Manyoni mkoani Singida, na mwanamke mmoja mtu mzima aliyetambulika kwa jina moja la Lilian.

Kamanda Chialo alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi kwa madereva wote wawili, na baadaye yule wa basi aliyetambulika kwa jina la Samson Ibrahimu (50) mkazi wa Dar es Salaamu aliyetoroka mara baada ya ajali kutokea na polisi inaendelea kumtafuta.

Alisema kwa upande wa abiria katika basi la Sumry hakuna aliyejeruhiwa, wote walitoka salama na wameshapatiwa usafiri kuendelea na safari yao.

Katika ajali ya pili iliyotokea Aprili 5, mwaka huu majira ya 11 alfajiri huko Mkambarani Mikese Wilaya ya Morogoro na kuhusisha gari aina ya Toyota Hiace lenye namba T 908 BCM na lori namba T251 BBG yenye tera T 812 BEP mali ya Moses Stephano wa Tarime mkoani Mara.

Waliokufa katika ajali hiyo ni Said Nyangaji (42) aliyekuwa dereva wa Hiace, Nimley Salum (28), Suleimani Gogo (55), Rogasi David (35), Athumani Sadick mtoto wa miezi minane, na Phoeby Manda (50) wote wakazi wa Mkambarani, Mikese.

Majeruhi wa ajali hiyo ni Zurfa Omary (12), Nasima Rajabu (32), Safina Halali (mwezi mmoja), Subira Husein (14), Hawa Saidi (34), Mariam Hasani (22), Tausi Rashidi (32), Rehema Husein (35) Hadija Ally (40), Mwamtumu Fadhili (28), wote wakazi wa Mikese, Onesmo Maroda (33) na Samuel Cogan(35), wakazi wa Dodoma.

Kamanda huyo alisema kuwa chazo cha ajali hiyo ni mwendo kasi na kwamba Hiace hiyo ilikuwa ikitaka kuipita gari nyingine na kukutana na lori hilo na kugongana uso kwa uso.

Ajali ya tatu, mtu mmoja aliyetambulika kwa jina la Pastory Eria (37) mkazi wa Mkundi aligongwa na gari lisilojulikana eneo la mkundi na kufariki papo hapo, chanzo cha ajali pia ni mwendo kasi.

1 comment:

  1. Madereva jaman jaribuni kuwa makini na mpunguze mwendo kasi.

    ReplyDelete