29 April 2011

Rooney akiri kuikosea Man United

LONDON, Uingereza

WAYNE Rooney usiku wa kuamkia juzi, alikiri kuwa alifanya makosa kutaka kuihama Manchester United.Mfungaji huyo wa England, alitaka kuondoka Old Trafford
miezi sita iliyopita baada ya kuhoji kuhusu malengo ya klabu na uimara wa timu.

Kwa sasa, United inakaribia kutwaa makombe mawili, la Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya. Rooney alisema: "Nikiangalia mambo yalivyo sasa, naona jinsi gani nilikosea!

"Wazi ninaelewa kuhusu makosa. Nilikiri hilo na kuomba radhi kwa hilo na nilitaka kujaribu kujisafisha mwenyewe, tena mbele ya mashabiki wa United. Ninafikiri ninafannya hivyo kwa sasa.

"Ni muda mrefu uliopita sasa na ninatumaini sasa ninaisaidia timu hii kufanikiwa.

"Itakuwa ni mwisho wa kusisimua kwa kutinga fainali ya Ligi ya Mabingwa na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu. Ninawajibika kwa silimia 100 kwa klabu hii."

Rooney alifunga goli la pili katika ushindi wa United wa mabao 2-0 kwenye mechi ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Schalke.

Mchezaji huyo amefunga magoli nane katika mechi 12.

Matokeo hayo ya ugenini, yamewaweka katika nafasi nzuri, United kutinga fainali ya Ligi ya Mabingwa kwa kucheza na ama Real Madrid au Barcelona, kwenye Uwanja wa Wembley, Uingereza Mei 28 mwaka huu.

Vijana wa kocha, Alex Ferguson watapambana na Arsenal katika Uwanja wa Emirates, Jumapili wakijua kuwa ushindi wa mechi hiyo na dhidi ya Chelsea wiki inayofuatia utafanya waweke rekodi ya kutwaa ubingwa wa England kwa mara ya 19 na kuipiku Liverpool iliyotwaa mara 18.

No comments:

Post a Comment