*Asema Spika si dhaifu, ana uzoefu mkubwa bungeni
*Amwombea muda kuwafunda wabunge wapya vijana
*Atetea muswada wa serikali wa mabadiliko ya katiba
Na Tumaini Makene
BAADA ya wananchi mbalimbali kuanza kutoa maoni yao juu ya mwenendo wa bunge kama moja ya
mihimili mitatu ya dola, wakikosoa utendaji wa Spika Bi. Anne Makinda, mzigo umesukumiwa kwa wabunge wapya hasa vijana kuwa hawajui taratibu, hivyo spika huyo anahitaji muda wa kuwafunda ili wajue kanuni hadi wakae sawa.
Hayo yalisemwa jana na Katibu wa Bunge, Dkt. Thomas Kashilillah, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya mwenendo wa bunge kuanzia Novemba hadi Machi, utaratibu wa kutunga sheria na matumizi ya hati ya dharura pamoja na nafasi ya spika katika kusimamia mijadala bungeni.
Alisema kuwa mwenendo wa bunge la 10 ambalo lilianza Novemba mwaka jana baada ya uchaguzi mkuu, ambao wananchi wengi wameonekana kutoufurahia, ikiwemo kuzomeana na kuzungumza lugha isiyofaa au kutofuatwa kwa kanuni, kunatokana na wabunge wengi kuwa wageni, wakiwa takribani asilimia 69, huku pia wengi wao wakiwa ni vijana.
Dkt. Kashilillah ambaye alitumia muda mwingi wa mkutano huo na waandishi wa habari kuutetea muswada wa kurekebisha katiba, ambao hivi karibuni ulirudishwa serikalini kwa ajili ya kuubadili lugha na kuongeza muda wa kusikiliza maoni ya wadau, alisema kuwa itachukua muda mrefu kwa wabunge wapya kumudu uendeshaji wa bunge kwa kuzingatia weledi wa kanuni.
"Suala jingine ambalo nilitaka kulitolea ufafanuzi na mlielewe vizuri ni juu ya uendeshaji wa bunge, hasa juu ya mambo ambayo yamekuwa yakitokea bungeni, kurushiana maneno, wengine wamefikia hatua ya kulifananisha bunge na shule ya msingi, suala hili linasababishwa na wabunge wengi kuwa wageni.
"Bunge la sasa linatakiwa kuwa na wabunge 357 mpaka sasa wapo wabunge 350 kwa sababau rais hajamaliza kuchagua katika zile nafasi zake 10 alizonazo. Wabunge 239 wanatoka majimboni, watano wanatoka Baraza la Wawakilishi (Zanzibar) mmoja ambaye ni mwanasheria mkuu anaingia kwa nafasi yake, wengine 102 ni viti maalumu wanawake.
"Hivyo zaidi ya asilimia 69 ya wabunge wa sasa ni wapya, wengi wao vijana ambao hawajawahi kufanya kazi serikalini, hawajawahi kushiriki makongamano au mijadala kama ya bunge. Wanahitaji msaada. Tulifanya semina mbili hapa Dar es Salaam, vyama vikuu kwa maana ya Chama Tawala CCM na Chama Kikuu cha Upinzani CHADEMA navyo pia viliwapatia semina wabunge wao," alisema Dkt. Kashililla.
Akimtetea Spika Makinda kuwa si dhaifu, kwani ana uzoefu bungeni akiwa ameshika nafasi mbalimbali, Dkt. Kashililla alisema kuwa mwenendo wa bunge unaonekana kwenda mlama kutokana na wabunge wengi kutokuwa na uelewa juu ya kanuni za bunge ambazo ndizo msingi wa taratibu za uendeshaji wa mhimili huo.
Alisema kuwa itachukua muda kwa spika kuwasaidia wabunge hao wapya ili waweze kuelewa taratibu za bunge na kuendesha shughuli zao kwa weledi wa kanuni.
"Bado hawajapata uelewa mzuri juu ya kanuni, bado wana upungufu, lakini upungufu huu si wa makusudi bali wa kutoelewa kanuni. Bunge letu ni la kistaarabu sana kati ya mabunge machache katika Jumuiya ya Madola, kuna wenzetu hata kutupiana viti ukumbini wanasema ni moja ya starehe za bungeni.
"Kwa mfano kuna kitu tunaita kwa lugha ya bunge 'Catching Speaker's eye', yaani kumfanya spika akuone, kuna njia tatu ambazo mbunge anaweza kutumia mojawapo ni kusimama, au kumtumia memo spika au kubonyeza chombo cha kuzungumzia na atasme kama ni taarifa au ni kuhusu utaratibu...lakini pia;
"Kwa mujibu wa kanuni akisimama spika hakuna mtu mwingine mbunge anaruhusiwa kusimama, mbunge yeyote hata kama alikuwa anazungumza akimwona spika kasimama lazima asitishe kuzungumza na anapaswa kukaa, lakini siku hizi mnaona wenyewe spika amesimama lakini kuna wabunge karibu 10 nao wamesimama tena wanazungumza," alisema Dkt. Kashililla.
Dkt. Kashililla aliongeza kuwa Spika Makinda amekuwa akitumia busara ya kutowaadhibu wabunge ili wajifunze pole pole mpaka hapo watakapoelewa na kuwa sawa na wabunge wazoefu waliokaa muda mrefu bungeni, akisema kufukuzana bungeni au kusimamisha shughuli za bunge kwa sababu ya utovu wa nidhamu wa wabunge 'wawili watatu' si vyema.
Hi Thomas hizo ni kanuni gani ambazo ni ngumu kwa wabunge kuzielewa? Au na wewe ni kabarka wa CCM, I doubt. Wabunge wamechoka na hilo bunge lenu, sisi watu wa kawaida tunashindwa kuelewa mnaongelea nini wakati umasikini unazidi kutumaliza. Kheri yenu na hao mlionao bungeni. Lakini sisi tulioko nje tunaumia. Ninadhani hao wabunge wanauchungu nasi ndiyo maana wanapinga na kusimama ili waonekane.
ReplyDelete