Na Amina Athumani
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Halid anatarajia kuwa mgeni rasmi katika sherehe za ufunguzi wa mashindano ya netiboli kwa nchi za Afrika Mashariki
yanayozinduliwa leo mjini Zanzibar.
Akizungumza kwa simu jana, Katibu Mkuu wa Chama cha Netiboli Zanzibar (CHANEZA), Rahma Bakari alisema mashindano hayo yatafunguliwa saa 9 alasiri na kiongozi huyo.
Alisema mara baada ya mashindano hayo kufunguliwa kutafanyika mechi ya ufunguzi kati ya mabingwa watetezi wa kombe hilo, NIC ya Uganda na timu wenyeji ya Mafunzo.
"Maandalizi yote ya mashindano haya yamekamilika na timu zote zimeshawasili na nyingine zinatarajia kuwasili leo jioni (jana jioni), hivyo tunawaomba wakazi wa Zanzibar kufika kwa wingi ili kushuhudia uzinduzi wa mashindano haya," alisema Rahma.
Timu zinazoshiriki mashindano haya ni kutoka Kenya, Uganda, Tanzania Bara, Zanzibar na Zambia ambayo inashiriki kama timu ya mualikwa ambapo jumla ya timu hizo ni 17 za wanawake na wanaume.
Rahma alisema mashindano hayo yanatarajia kumalizika Mei 4, mwaka huu na kumpata bingwa wa mpya wa Afrika Mashariki wa netiboli ambapo Uganda inatetea taji hilo.
No comments:
Post a Comment