17 April 2011

Pinda ataka katiba mpya imilikiwe na wananchi

Na Edmund Mihale, Dodoma

WAZIRI Mkuu, Bw. Mizengo Pinda amesema kuwa uongozi madhubuti wa wasisi na viongozi
waliopo sasa wanaongozwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Katiba ya
Zanzibar hivyo kubeza viongozi hao au Katiba ni kudhalilisha taifa.

Bw. Pinda alisema hayo wakati akiahirisha kikao cha tisa katika mkutano wa tatu wa
Bunge jana mjini Dodoma.  

Alisema kuwa Watanzania wanayo fursa nyingine ya kutazama upya Katiba hivyo
wanatakiwa kushirikiana kwa dhamira moja ya kutoa maoni, ushauri na mapendekezo
mbalimbali ili kwa pamoja kupata Katiba itakayowanufaisha Watanzania wote.

Alisema kuwa katiba itakayotokana na michango yetu mbalimbali na kumilikiwa na
Wananchi wenyewe, haina budi kutokana na Watanzania wote wenye nia ya kulitakia
Taifa hili na Wananchi amani, upendo na utulivu.

"Mheshimiwa Spika, baadhi ya Watanzania wanabeza Katiba zetu kwa msingi tu kuwa
zimerekebishwa mara nyingi na hivyo kuzifananisha na viraka.  Kama ilivyo kwa
Sheria, Katiba nazo hufanyiwa marekebisho kila inapobidi ili kuzingatia hali mpya
inayojitokeza katika taifa ambayo inaonekana kuwa na uzito wa kulazimika kurekebisha
Katiba ili kutambua hali hiyo Kikatiba. Ndiyo maana Katiba yetu imerekebishwa mara
14 tangu mwaka 1977.

"Mheshimiwa Spika, nimefahamishwa kuwa kwa msingi huo huo Katiba ya Afrika ya
Kusini iliyotungwa mwaka 1997 na iliyopitia hatua mbalimbali za  Kidemokrasia na
kusifika ulimwenguni kote kwamba ni Katiba ya Watu, katika uhai wake wa miaka 14
sasa tayari  imekwishafanyiwa marekebisho mara 16. Katiba ya Marekani nayo
nimejulishwa kuwa tayari imerekebishwa mara 27 na ile ya India mara 94 na bado
Wananchi wa nchi hizo wana fahari na Katiba hizo,"alisema Bw Pinda!

Alisema kimsingi Wataalam wa historia wanaeleza kuwa, katika kuona marekebisho ya
Katiba mbalimbali za mataifa mtu anaweza kuona historia kamili ya taifa husika na
kujua mabadiliko ya kijamii, kisiasa na kiuchumi katika kipindi husika.

Alisema amelazimika kuyasema hayo ili kuondoa ile dhana ya kuwa Katiba iliyopo
sasa  haifai, hasa kwa sababu imefanyiwa marekebisho mara 14.

Alisema kuwa ikumbukwe kuwa, mwaka 1992 Taifalilionesha ukomavu wake kwa  kutambua Mfumo wa Vyama vingi Nchini. "Huu ni ushahidi tosha wa ukomavu wa Taifa katika  Utawala wa Sheria na Demokrasia na si ishara ya upungufu unaosababisha kupewa jina la kuweka kiraka," alisema.

Alitoa wito kwa wananchi kuendelea kuiheshimu na kuifuata Katiba iliyopo mpaka pale Katiba Mpya inayoanza mchakato wake sasa itakapokamilika. Alisema kuwa katiba mpya inatungwa kwa  ajili ya kukidhi mazingira mapya ya leo na matakwa ya wananchi wa leo baada ya miaka 50  ya Uhuru kama alivyosema Rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake ya hivi karibuni.

Kuhusu muswada huo wa Kuunda Tume ya kukusanya maoni ya wananchi alisema  Serikali itahakikisha muswada unachapishwa kwa lugha ya Kiswahili na kuusambaza kwa wananchi kwa lengo la kuwawezesha kujadili kwa wepesi na kueleweka.  Alisema muswada huo pia utachapishwa katika  magazeti mbalimbali ya kawaida ya kila siku kwa lengo hilo hilo kama ulivyoshauriwa na tume.

Kuhusu umeme alisema tathimini iliyofanywa na  watalaamu wa TANESCO na Wizara ya Nishati na Madini mwanzoni mwa mwaka huu, ilionesha  kwamba patakuwepo na upungufu wa wastani wa Megawati 264 za nishati ya umeme katika  Mfumo wa Gridi ya Taifa mwaka 2011.

Alisema kuwa tathmini hiyo ilitokana na hali ya ukame iliyokuwa inaendelea, kutokana na kupungua kwa mvua za vuli mwishoni mwa mwaka 2010. Kutokana na  taarifa za  hivi karibuni za Wakala wa Utabiri wa Hali ya Hewa, bado hali ya mvua za masika hairidhishi ingawaje kumekuwa na mvua  ya hapa na pale katika maeneo mengi Nchini.

Alisema maji yanayooingia kwenye Vituo vya kuzalisha umeme bado ni kidogo ikilinganishwa na mahitaji. Hata hivyo, maji kidogo yaliyoongezeka yamesaidia kupunguza mgao wa umeme. Bwawa ambalo linategemewa zaidi ni la Mtera ambalo bado
kina cha maji kiko chini. 

Alisema katika mwaka 2010/2011, serikali iliahidi kuongeza Idadi ya walimu nchini
ili kukidhi mahitaji yanayotokana na ongezeko kubwa la Shule pamoja na Wanafunzi
katika ngazi zote za elimu nchini.

Alisema kuwa katika kutekeleza azma hiyo, Serikali imetoa kipaumbele cha kuajiri
Walimu 1,891 katika shule za msingi, sekondari na Vyuo vya ualimu kuanzia mwezi Julai 2010 hadi Machi 2011. 

1 comment:

  1. Mhe Pinda kurekebisha Katiba hata ikiwa ni mara elfu moja ni mchakato wa kawaida katika jamii zote zinazofuata misingi ya demokrasia. Hizo jamii ulizozitolea mfano zimerekebisha katiba ambazo wanajamii walizitunga wenyewe. Ugomvi na katiba yetu ni kwamba ilitungwa na wakoloni (kumbuka ukoloni na demokrasia vilikuwa havitangamani) wakati walipoamua kutuachia madaraka ya kisiasa. Kilichofanyika ni jina la Gavana kuwa-replaced na jina la Rais. Colony kuwa replaced na Republic. Muundo wa utawala ulibaki huo huo ambapo Rais, kama ilivyokuwa Gavana, ni rais-mfalme (ambayo ni hatari kwa jamii inayotaka kuendesha shughuli zao za kisiasa na kiuchumi kidemokrasia). Kwa hiyo Mh Pinda, hayo marekebisho 14 tangu 1977 yanaitwa viraka kwa sababu yalikuwa yanaweka wanja kwenye sura ya muundo wa utawala wa kikoloni tuliourithi. Kumbuka hakuna anayelaumiwa kwa kurithi huo muundo kwa sababu hali ndivyo ilivyokuwa. Lakini kama hatuandiki Katiba mpya wakati huu muafaka, basi watoto na wajukuu zetu watakuwa na haki ya kutulaumu milele. Kwa kifupi unarekebisha KITU ULICHOKIUNDA MWENYEWE, na sio ulichoundiwa!!!!!!

    ReplyDelete