06 April 2011

Majira laongoza shindano la Ukimwi

Na Angelina Mganga

GAZETI la Majira ya limeibuka kidedea na kupata tuzo ya ushindi wa kwanza katika kutoa nafasi kubwa kwa makala zinazohamasisha wanandoa na wapenzi
kupima Virusi vya Ukimwi (VVU) kwa pamoja.

Gazeti hili limetunukiwa tuzo hiyo jana huku waandishi wake wawili kuibuka zawadi za fedha na vyeti kwa kushiriki katika shindano hilo.

Shindano hilo liliandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za  Ukimwi (AJAAT) kati ya Novemba 2010 na Februari 15, mwaka huu ambapo jumla ya makala 75 zilishindanishwa kutoka kwenye magazeti, redio na runinga.

Katika shindano hilo waandishi walioibuka na ushindi na kupatiwa zawadi ya fedha taslimu ni 15, ambapo kwa upande wa gazeti la Majira ni Bw. Reuben Kagaruki na Bi. Rehema Mohamed.

Washindi wengine ni vyombo vyao kwenye mabano ni Bw. Gerald Kitabu (The Guardian), Bw. Raymond Kamonyge (Mwananchi), Bw.  Abdallah Bakari (The Citizen) na Bw. Joseph Ndamalya (Radio One).

Wengine ni Bw. Martini Kuahanga (Radio Tumaini), Bw. Rosemary Mirondi (The Citizen), Bw. Stephen Baligeya (Uhuru), Bw. Alpha Nuhu (The Guardian), Bw. Fadhili Mohamed (Habari Leo), Bi. Margreth Tengule (Star TV) na Bw. Said Michael (Tanzania Daima).

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi wa Uraghbishi, Habari na Mawasiliano wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS), Bw. Geoffey Majengo alisema waandishi wa habari ni wadau wa kubwa katika kuelimisha jamii katika masuala mbalimbali.

Alisema shindano hilo lililenga kuhamsha mjadala kuhusu ushiriki wa jinsia zote kama njia ya kuhamasisha wanandoa kupima kwa pamoja ili kupunguza na hatimaye kuzuia maambukizi mapya ya VVU.

Alisema waandishi wana mchango mkubwa kwa jamii, ndiyo maana mwanafalsafa mmoja aliwahi kusema; "Lisiloonekana katika vyombo vya habari basi halipo."

No comments:

Post a Comment