LONDON, England
MMILIKI wa Chelsea, Roman Abramovich ameripotiwa kuwa yupo tayari kumuonesha njia ya kuondokea kocha wake, Carlo Ancelotti ifikapo mwishoni mwa
msimu huu.
Gazeti la London Evening Standard, liliripoti jana kuwa hivi sasa Abramovich amekasirika na kitendo cha Chelsea kutupwa nje ya michuano ya Klabu Bingwa Ulaya na huenda akaamua hatima ya Ancelotti, ifikapo mwishoni mwa msimu huu.
Gazeti hilo liliripoti kuwa bilionea huyo alikuwa bado hajajiandaa kuchukua hatua kali, kutokana na kitendo cha juzi cha timu hiyo kufungwa na Manchester United lakini likaeleza kuwa inavyoonekana nafasi ya kocha huyo ipo mashakani.
Ancelotti, ambaye mkataba wake unamalizika majira ya joto yajayo alitarajiwa kufanya makubwa ndani ya klabu hiyo, lakini akashindwa licha ya timu hiyo kutwaa mataji mawili msimu uliopita.
Vyanzo vya habari vilivyopo karibu na Abramovich, vilieleza kuwa Mrussia huyo alitarajia timu hiyo kuonesha kiwango kikubwa baada ya kutumia pauni milioni 75 kuwasajili, Fernando Torres na David Luiz katika usajili wa Januari mwaka huu, lakini kwa sasa ana wasiwasi kuhusu jitihada na morali wa wachezaji hao walioonesha.
No comments:
Post a Comment