08 April 2011

Barcelona yaifanyia kweli Shakhtar

BARCELONA, Hispania

MIAMBA ya soka ya Hispania, Barcelona juzi ilifanya kweli katika michuano ya Klabu Bingwa Ulaya baada ya kuichapa Shakhtar mabao 5-1, huku ikiwachukua dakika
mbili kuhesabu bao la kwanza.

Ushindi huo umewaweka Barcelona katika nafasi nzuri ya kuweza kusonga mbele katika hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.

Barca iliwachukua dakika mbili kuweza kuhesabu bao la kwanza dhidi ya wapinzani wao kutoka Ukraine.

Andres Iniesta alimpasia mpirea Lionel Messi, ambaye aliunasa mpira na kumchungulia kipa Andriy Pyatov na kufunga shuti la chini ambalo lilijaa wavuni.

Kisha Iniesta naye alitengeneza nafasi ya kufunga kwa kumpasia beki Daniel Alves, aliyekuwa peke yake na kufunga bao la pili dakika ya 34.

Barca ilipata bao la tatu dakika ya 53 wakati mlinzi Gerard Pique, alipounganisha mpira wa kona na kufunga goli la tatu likiwa pia goli lake la pili msimu huu.

Yaroslav Rakitskiy aliipa matumaini timu ya Ukraine kwa kupata bao la ugenini alipomfunga kipa wa Barcelona, Victor Valdes katika dakika ya 60.

Lakini Seydou Keita, akaifungia Barcelona bao jingine dakika moja baadaye.

Kiungo Xavi alikuja kufunga bao jingine zikiwa zimesalia dakika nne kabla ya mpira kuisha.

Ushindi huyo wa Barcelona umeifanya, Shakhtar iwe na mlima wa kupanda katika mechi ya marudiano ambapo italazimika kushinda mabao 4-0 ili kusonga mbele.

Ushindi huo umeweka dalili za kukutana Barcelona na Real Madria katika hatua ya nusu fainali baada ya Real, nayo kushinda mechi yake ya kwanza dhidi Tottenham mabao 4-0 Jumanne.

Lakini kocha wa Barca, Pep Guardiola amewaonya wachezaji wake kutoidharau timu ya Shakhtar, ambayo iliwahi kushinda mabao 3-2 katika Uwanja wao wa Nou Camp mwaka 2008.

Alisema: "Matokeo si ya mwisho. Wana timu nzuri sana."

No comments:

Post a Comment