10 March 2011

Watumishi 12 matatani Rombo kwa ufisadi

Na Martha Fataely, Rombo

KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), imeagiza Halmashauri ya Wilaya ya Rombo kuwasimamisha kazi na kuwafikisha mahakamani
watumishi wake 12 waliohusika katika ubadhirifu wa zaidi ya sh. milioni 941.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Bw. Augustine Mrema alisema hayo jana wakati wakipitia ripoti ya ukaguzi maalumu katika halmashauri ya wilaya hiyo kwa kipindi cha June 2007 hadi June 2009 ambayo ilitoa mapendekezo ambayo hayakutekelezwa hadi kufikia jana.

Alisema watumishi hao wakiwemo Mweka Hazina Emmanuel Masele, Mhandisi wa Wilaya ambaye alikuwa akikaimu nafasi ya Mkurugenzi, Elias Mshana, Ofisa Utumishi Alphonce Kasaanyi na Ofisa elimu Msingi Joseph Ngoseki.

Kamati hiyo imesema watumishi hao na wenzao wanane wa nafasi mbalimbali wameisababishia halmashauri hiyo hasara ya kiasi hicho cha fedha kutokana na ubadhirifu uliofanywa kupitia matumizi yaliyokiuka taratibu na kanuni zilizopo.

Aidha kamati hiyo imetoa onyo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Samweli Kibaja kwa kushindwa kutekeleza mapendekezo ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Azimio la Baraza la Madiwani lililotaka watumishi hao kusimamishwa kazi na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Huku ni kuchakachua maamuzi ya CAG, wewe mkurugenzi nini kilikushinda kutekeleza mapendekezo yale na maazimio ya Baraza la Madiwani hata viongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro hawakuwa na mamlaka kisheria kushauri kutotekelezwa kwa mapendekezo ya CAG, alisema.

Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo akiwemo Mbunge wa Kilombero Abdul Mteketa na Mbunge Viti Maalumu Tauhida Galoss walisema viongozi hao wanatakiwa kuondolewa katika nafasi zao ili kupisha uchunguzi kufanyika.

Kuna mtandao wa kulindana baina ya viongozi wa mkoa na halmashauri, wote hawa wanasababisha wananchi kuilalamikia serikali yao, tusipokuwa makini katika hili uenda yakatokea ya Misri na Tunisi, alisema Bw. Mteketa.

Akijibu hoja za wabunge hao, Bw. Kibaja alisema tayari walikuwa wameshachukua hatua kwa baadhi ya watumishi ambao walisimamishwa kazi huku wengine wakiendelea na kazi jibu ambalo lilipingwa na kamati hiyo.

2 comments:

  1. HONGERENI KAMATI KWA WAJIBU WENU MUHIMU UTEKEKELEZAJI WA MAAMUZI YENU YATIMIZWE, YASIISHIE KUTOA MAAMUZI BILA KUFANYIWA KAZI MAANA MAENDELEO MENGI YA MIKOANI NA WILAYANI YAKO MIKONONI MWA HALMASHAURI. LAKINI WAO WANAJILIMBIKIZIA MALI WENYEWE BINAFSI HUKU WANANCHI WANAOLIPA HIZO KODI WAKIACHWA HAWANA HUDUMA MUHIMU, MATOKEO YAKE MALALAMIKO YANAKWENDA SERIKALINI KUWA HAIWAJIBIKI NA HAIWAJALI WANANCHI WAKE. PONGEZI ZA DHATI KWA MWENYEKITI WA KAMATI MH;LYATONGA BIGUP WAJUWE KUWA HII NCHI INA WENYEWE SIO WABORONGE TUU HUKU WALIPA KODI KUZIDI KUWA HOHEHAHE,NA WAJUWE HIZO PESA SIO ZAO NI ZA HAWA WALIPA KODI

    ReplyDelete
  2. HONGERA KAMATI YA BUNGE KWA KUWAUMBUA MAFISADI WA HUKU KWENYE SERIKALI ZA MITAA.MJE NA MANISPAA YA SHINYANGA MUONE UOZO HASA IDARA YA AFYA AMBAPO BAADHI YA WATUMISHI WAMEJIBADILISHIA VYEO KWA LENGO LA KUPATA MSHAHARA MKUBWA KINYUME NA KADA WALIZOSOMEA.WAMEJIITA MAAFIOSA AFYA NA WAKATI HAWAJAWAHI KUSOMEA KAZI HIYO.MJE MTUSAFISHIE UFISADI HUU

    ReplyDelete