10 March 2011

Polisi waua wawili kwa risasi

Na Raphael Okello, Musoma

WATU wanne wameuawa, wawili kwa kupigwa risasi na polisi, na nyumba nane kuteketezwa kwa moto katika kijiji cha Nyamisisi katika Wilaya ya
Musoma vijijini.

Tukio hilo lilitokea juzi baada ya wananchi wenye hasira kuwaua watu wawili na kuchoma moto nyumba zao kutokana na imani ya kishirikina huku polisi nao wakifyatua risasi na kuua watu wawili katika tukio hilo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Bw. Robert Boaz amethibitisha tukio hilo kuwa waliouawa kwa imani za kishirikina ni Bi. Modesta Nyamhanga (60) na Bw. Cosmas Mniko (60) wakazi wa Kijiji cha Nyamisisi wilaya ya Musoma vijijini.

Waliouawa kwa kupigwa risasi na polisi katika tukio hilo ni Bw. Julias Hamphery (32) na Bw. Sese Kabari (30) wote wakazi wa kijiji cha hicho.

Akielezea tukio hilo lililotokea juzi saa 9:30 jioni Bw. Boaz alisema kuwa siku mbili kabla ya tukio mama mmoja alimtuma mtoto wake kuteka maji kisimani na mtoto huyo akamkuta Bi. Nyamhanga ambaye alimpaka dawa isiyojulika kichwani.

Kamanda alisema baada ya mtoto huyo kurudi nyumbani alitoa taarifa kwa baba yake ambaye aliwachukua mgambo kumfuata bibi huyo na kumpeleka katika Kituo Kidogo cha Polisi Kyabakari Musoma vijijini ili aandike maelezo na baadaye alipewa dhamana na kurudi nyumbani kwake.

Bw. Boaz alieleza kuwa kabla ya tukio hilo lililomhusu binti kupakwa dawa pia kuna mtoto mwingine alipotea katika kijiji hicho katika mazingira ya kutatanisha ambapo pia Bi. Nyamhanga alituhumiwa kuwa yeye ndiye aliyemficha.

Alisema kutokana na hisia hizo juzi siku ya tukio Marehemu Bi. Nyamhanga aliondoka nyumbani kwake na watoto wa kike wawili waliodaiwa kuwa ni watoto wake kuwapeleka katika Kituo cha Mabasi ya Nyamisisi ili kuwasafirisha kwenda  Mwanza kusalimia ndugu zao.

"Akiwa hapo stendi wananchi walimuona na ndipo walipompigia yowe kuwa alikuwa anamtorosha huyo mtoto aliyesaidikiwa kuwa alikuwa amemficha," alisema Bw. Boaz.

Alisema wakiwa katika kituo hicho cha mabasi licha ya Bi. Nyamhanga kukanusha madai yao wananchi hao waliendelea kumpiga wakimshurutisha arudi nyumbani kwake ili awaonyeshe alipo mtoto aliyedaiwa kutoweka kimiujiza hapo kijijini.

Bw. Boaz alisema wananchi hao walimpeleka hadi nyumbani kwake na walipofika hapo walimlazimisha aingie ndani huku wengine wakichoma moto nyumba hiyo na kumteketeza kwa moto.

Kwa mujibu wa kamanda wakati wanampiga, Bi. Nyamhanga aliwambia kuwa mtoto huyo yuko kwa mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Bw. Cosmas Mniko mkazi wa kijiji hicho jambo lililowalazimisha wananchi hao kwenda na kumkamata Bw. Mniko ambaye naye walimuua na kuteketeza nyumba zake saba na pamoja na mali zake.

Alisema wakati wanafanya vitendo hivyo askari polisi wa Kituo cha Kiabakari walikwenda kwenye tukio ambapo hata hivyo kamanda huyo alidai kuwa kutokana na umati wa watu ambao nao walianza kukabiliana na polisi ili wasiwazuie kutekeleza azma yao, polisi walifyatua risasi ambazo ziliwapata vijana wawili Bw. Sese Kabari na Bw. Julius Amphrey ambao wote walifariki dunia.

Bw. Boaz alisema kutokana na purukushani na hasira za wananchi hao ambao nao walikusudia kufanya uharibifu zaidi, alituma kikosi kingine cha polisi kutoka mjini Musoma ambao waliongeza nguvu na kufanikiwa kutuliza ghasia hizo.

Kamanda huyo alisema kuwa polisi waliofyatua risasi na kuua bado wanashikiliwa kwa mahojiano zaidi ili kuhakikisha kuwa haki inatendeka na ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi kutochukulia sheria mkononi.

5 comments:

  1. Upumbavu mtupu huu! Polisi walienda kuzuia watu wasiue watu au walienda kuua watu? Sasa walichofanya jeshi la polisi kina tofauti gani na kile watu hao walichokuwa wanafanya?

    ReplyDelete
  2. Yaani afadhali kile walichokuwa wanafanya wananchi kuliko hilo walililofanya polisi.Wananchi walikuwa na hasira ya vitendo vya kishirikina ambavyo hata wangeripoti polisi au mahakamani wangeambiwa serikali haimini katika ushirikina. Ushirikina ungezidi kushamiri, watoto kupotea, watu kuuawa bure n.k. Polisi walikwenda kuua kama ilivyo kawaida yao. Waliua Arusha, serikali ikawatetea, na sasa wameua Musoma, serikali inawatetea. Serikali ndiyo wauaji. JK tupishe Ikulu ili tuishi kwa amani bila hofu ya vifo kutoka jeshi la polisi.

    ReplyDelete
  3. police ya mwema imefundishwa hivyo kuwa taarifa za kiintelejensia na kuua watu pale tu wanapoona watu wamekusanyika.Hini serikali ya kishenzi na isiyopaswa kuheshimika tena. Na sisi wananchi tutaanza kuwaua police mitaani uvumilivu ukitushinda

    ReplyDelete
  4. Sasa ninaanza kufikiri kuwa baadhi ya polisi wetu hawana ujuzi wa wakati gani silaha inaweza kutumika na itumikeje. Hayo yamejidhihirisha Misri, Arusha na sasa katika tukio hili. Nitafurahi nikipata "feedback" ya uchunguzi wa polisi. Ingawa mazoea ya Tanzania, "feedback" huwa hazitolewi kwa jamii.

    ReplyDelete
  5. Wachangiaji kwenye ukweli tukiri ukweli na tusipindishe mambo. Unategemea wewe ungekuwa polisi na upo katikati ya watu kama hao wanachoma moto nyumba na kuua watu wewe ungefanya nini katika kukabilina na hali hiyo. Hapa polisi wako sahihi kabisa na wamefanya kazi yao kwani wangechelewa bila kutumia risasi wangudhurika wao. Wakati umefika kwa watanzania wenye uelewa kuchukua hatua za kutojichukulia sheria mikononi. inakuwaje umutuhumu mtu kuwa Mchawi na umuuwe bila kumpeleka kwenye vyombo vya dola. Nawashauri hawa ndugu zetu wa Musoma waache mambo ujima waende shule wafute ujinga huu na aibu hii. Naomba polisi waliofanya kazi yao wasishikiliwe au kunyanyaswa maana siku nyingine watakimbia na kuacha watu wafe au waumizwe maana watakuwa hawaruhusiwi kujihami hiyo haitakuwa polisi tena itakuwa ni siasa ya polisi.Mpo nyie walanchoka?

    ReplyDelete