Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Bw. Shamsi Vuai Nahodha ameiagiza Idara ya Uhamiaji kufanya operesheni maalumu kuwakamata na kuwarejesha
makwao watu wote ambao si raia wa Tanzania wanaoishi nchini kinyume cha sheria.
Bw. Nahodha alisema hayo jana wakati akizungumza na viongozi na watumishi wa idara hiyo Dar es Salaam katika ziara yake ya siku moja kufuatilia utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa mapema mwaka huu, alipoitembelea baada ya kuteuliwa kushika nwadhifa huo.
Alisema kumekuwepo na wimbi la wahamiaji haramu nchini, hivyo ni vyema kila mtu awe Mtanzania au mgeni kuheshimu sheria za nchi.
Hata ukitembea tu barabarani utajua tu mtu huyu si Mtanzania, wako watu wengi ukipishana naye tu njiani bila hata kupata taarifa zake za kina utagundua ni mgeni na hayuko nchini kwa njia halali. Ndugu zangu yafaa jambo hili litazamwe upya na kwa kina zaidi kuliepushia taifa letu madhara ya siku za usoni,รข€ alisema Bw. Nahodha.
Katika hatua nyingine Waziri Nahodha ameitaka Idara ya Uhamiaji kutafuta na kuanzisha mfumo mpya na wa kisayansi wa ukusanyaji wa mapato yanayotokana na huduma za uhamiaji, ikiwemo, pasi za kusafiria, ukaazi na hati nyinginezo ili kuweza kukusanya mapato stahiki.
Waziri Nahodha amesema kwa sasa haridhishwi na mfumo unaotumika katika ukusanyaji wa mapato ambao alisema unaikwamisha idara hiyo.
Alisema mfumo wa sasa unawapa ushawishi mkubwa watumishi wa idara hiyo kutokuwa waaminifu kutokana na hali ya udhaifu wa kibinadamu.
Wakati umefikia ndugu zangu uanzishwe utaratibu kwa wafanyakazi kuhusika na makaratasi tu lakini makusanyo yote yafanyike kwa njia ya Credit Card kama nchi nyingine zinavyofanya, alisisitiza Bw. Nahodha na kuongeza kuwa kutumika kwa mfumo mpya kutapunguza mianya ya vitendo viovu vinavyosababishwa na kukosekana kwa uaminifu pale mtu anapopokea fedha mkononi.
Alisema kupatikana na kuanza kutumika kwa mfumo wa kisayansi kutasaidia idara hiyo kupata makusanyo stahiki yatakayochangia kuboreshwa kwa huduma za uhamiaji pamoja na mishahara ya wafanyakazi wa idara hiyo.
No comments:
Post a Comment