*Mmoja alitibiwa kisukari akapona
*Alipata ajali akitoka kununua pembejeo
*Mwingine ni ndugu aliyemsindikiza
Na Hecton Chuwa, Moshi
WATU wanne wamefariki dunia katika matukio matatu ya ajali, wawili kati yao wanadaiwa
kufariki dunia wakiwa njiani kutoka Loliondo ambako walikwenda kwa ajili ya matibabu yanayotolewa na Mwinjilisti Msataafu Bw. Ambilikile Mwasapile.
Akithibitisha kutokea kwa matukio hayo Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro,Kamishina Msaidizi Mwandamizi Lucas Ng’hoboko, alisema kuwa katika tukio la kwanza watu wawili aliowataja kwa majina ya Clemence Shirima na Janet Shirima wote wakazi wa Rombo walifariki dunia juzi, wakitokea Loliondo.
“Wawili hawa walifariki dunia papo hapo katika ajali iliyotokea eneo la mji mdogo wa Boma Ng’ombe, wilayani Hai, saa kumi na moja jioni, baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kugonga mti, gari hilo aina ya Land Cruiser lenye namba T 697 BBG liliendeshwa na Prosper Abel, (24) wa shule ya sekondari Shauri Tanga ya wilayani Rombo," alisema.
Alisema katika ajali hiyo watu watatu walijeruhiwa na kupelekwa katika hospitali ya Rufaa ya KCMC kwa matibabu ambapo walilazwa.
Aliwataja majeruhi hao kuwa ni Calisti Shirima (53) ambaye ni Mkuu wa shule ya Sekondari ya Shauri Tanga na ambaye ni mtoto wa marehemu Clemence, Lightness John, mwalimu wa shule ya Shauri Tanga na dereva wa gari hilo Prosper.
Alisema miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti kilichopo katika hospitali ya rufaa ya KCMC.
Kwa mujibu wa mwanafamilia mmoja wa marehemu hao ambaye hakutaka jina lake litajwe, marehemu Clemence alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya kisukari kwa muda mrefu kiasi cha kutoweza kutembea kabisa na kwamba alipopata taarifa za Mchungaji huyo wa Loliondo aliomba apelekwe kwa tiba.
“Babu alikuwa hawezi kutembea kabisa kwa muda mrefu na alipokwenda huko alipata nafuu kiasi cha kuweza kutembea bila matatizo na hata alipofika maeneo ya Mto wa Mbu wakati wanarudi, aliagiza apitishwe duka la pembejeo ili anunue bomba la kunyunyuzia dawa za kuua wadudu kwenye mimea”, alisema.
Alisema kuwa hata hivyo safari yake na wenzake iliishia Boma Ng’ombe pale walipopata ajali hiyo ambayo ilisababisha yeye na mwenzake kupoteza maisha, maisha ambayo alikwenda kuyakoa huko Loliondo.
Wakati huo huo mtu mwingine alifariki dunia wilayani Same kutokana na ajali iliyoyahusisha magari mawili na pikipiki, iliyotokea eneo la Nkongei katika barabara ya Moshi- Dar es Salaam.
Kamanda Ng’hoboko alimtaja marehemu kuwa ni Samuel Myange (49), aliyekuwa abiria wa pikipiki yenye namba T 652 ARS iliyokuwa ikiendeshwa na Saburi Mapenzi 56) baada ya pikipiki hiyo kugongwa na gari aina ya Toyota Chaser lenye namba T 348 ANK lililokuwa likiendeshwa na Ally Hussein, (32).
“Lori aina ya Scania lenye namba T 281 AHA na semi trailer namba T 906 AGH likiendeshwa na Said Omar (35) liligongana na Toyota Chaser hiyo kabla ya gari hilo dogo kuigonga pikipiki na kusababisha kifo cha Myange”, alisema.
Kamanda Ng’hoboko alisema ajali ya tatu ilitokea juzi katika eneo la Kiboriloni, Moshi Mjini baada ya pikipiki iliyokuwa ikiendeshwa na Daniel Ngatuni kuacha njia na kuanguka na kusababisha kifo cha dereva wa pikipiki
hiyo.
Mipango ya mungu
ReplyDeleteAnchoamua muumba hakina wa kukizuia au kukosoa
ReplyDeletePoleni wafiwa wote kwa kuwapoteza wapendwa wenu. Kwa wale waliokuwa wamekunywa ile daya ya maji ya mchungaji bila shaka imani yao rohoni ilimtukuza mungu kwa matibabu yale ya kimiujiza. Then na iwe tiba yao pia kiroho,yawezekana utukufu waliounuia kwa MUNGU ukawa ni heri yao kwenye MBINGU YA MUNGU.AMEN. Pascal.
ReplyDeleteWafiwa salini kila wakati nakushukuru kwa kila jambo. Liwe baya liwe zuri kwa Mungu yote mema/ sawa
ReplyDelete