09 March 2011

Uhaba wa sukari janja ya wafanyabiashara

Na Tumaini Makene

BAADHI ya wasambazaji wa sukari nchini sasa wanaonekana kuishika ndevu serikali, wakisukumiwa tuhuma kuwa ndiyo wanaohusika katika kuendelea kuihodhi
 bidhaa hiyo ili ionekane ni adimu ili waendelee kunufaika kibiashara, Majira limeelezwa.

Imeelezwa kuwa uhaba huo wa sukari sasa unaonekana kuwa ni wa kutengenezwa kwa manufaa ya kikundi cha wafanyabishara wakubwa kwa lengo la kutaka kujinufaisha kwa faida kubwa, kwa gharama ya Watanzania.
Vyanzo mbalimbali vya habari vya Majira kutoka katika duru za wadau wa sukari nchini, vimesema kuwa wasambazaji hao ndiyo wanapaswa kubeba mzigo wa lawama za wananchi, na hata ikibidi, hatua za serikali iwapo itaamua kufanya hivyo, kwa bei ya bidhaa hiyo kuendelea kuwa juu, ikiuzwa zaidi ya sh. 1,700, kinyume na maelekezo ya serikali.

Mpaka sasa wazalishaji wakubwa wa sukari nchini ni viwanda vya TPC (Moshi), Mtibwa, Kilombero na Kagera. Wasambazaji wakubwa ni Mohamed Enterprises Limited (METL), Al Neem, TPC Distributors na Lake Zone.
Hivi karibuni serikali, kwa kuzingatia masuala yote ya kibiashara, kuanzia kwa mzalishaji, msambazaji hadi muuzaji wa mwisho, ilielekeza kuwa bei ya sukari haipaswi kuuzwa zaidi ya sh. 1,700, kwa bei ya rejareja kwa mtumiaji popote alipo nchini.

Akitangaza uamuzi huo, ambao ulitokana na kikao kati ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda na wadau wote wa sukari nchini, Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko, Dkt. Cyril Chami alisema kuwa;
"Kikao hicho kilipata takwimu zote na kubaini kuwa kiasi cha sukari kilichopo nchini hivi sasa, kinatosheleza mahitaji ya nchi nzima, kwa zaidi ya miezi miwili, yaani Februari hadi Aprili mwishoni, kabla ya uzalishaji kuanza tena Mei, baada ya viwanda kuwa vimefungwa.

"Kwa kuwa kiasi cha sukari kilichopo nchini ni cha kutosha, serikali imewaagiza wenye viwanda vya kuzalisha sukari pamoja na wasambazaji wasambaze sukari iliyopo katika maghala kwa wauzaji wa kati na wadogo mara moja, ili kuondoa hofu iliyopo ya kupungua kwa ugavi, hivyo kusababisha bei kupanda.
Katika tamko hilo, serikali ilifuta ushuru wa forodha kwa kiasi cha tani 37,500 kati ya tani 50,000 zitakazoagizwa kutoka nje ya nchi, ili kufidhishia hitaji la tani 50,000, kufidishia pengo la mahitaji kwa Mei hadi Juni, wakati uzalishaji wa viwanda vya ndani utakapoanza tena.

Chama cha wazalishaji wa Sukari nchini kimebainisha kuwa moja ya sababu inayodhihirisha kuwa wasambazaji ndiyo wanaendeleza tatizo la sukari nchini kwa sasa, ni kushuka kwa mauzo kwa tani kwa baadhi ya wazalishaji tangu kutolewa kwa tamko hilo la serikali.

Mwenyekiti wa chama hicho, ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa Kiwanda cha TPC cha mkoani Kilimanjaro, Bw. Robert Baissac alisema jana kuwa kabla ya tamko la serikali, kiwanda hicho kilikuwa kinauza takribani tani 300 kwa siku, lakini baada ya serikali kuondoa ushuru wa forodha ili sukari iagizwe kwa wingi zaidi kuondoa upungufu mkubwa, mauzo hayo yameshuka zaidi ya nusu, mpaka kufikia tani 125 kwa siku.
"Maana yake ni kwamba sasa hawanunui tena sukari kutoka kwa wazalishaji (viwandani), sasa wanauza sukari waliyokuwa wamehodhi kabla, ili itakapoanza kuingia ile ya kutoka nje iliyoondolewa ushuru, hiyo waliyokuwa nayo isije ikawadode, alisema Bw. Baissac.

Vyanzo vingine vya habari vimesema kuwa hata katika kikao na waziri mkuu, kabla hajakutana na wadau wote, wasambazaji walimwambia kuwa hawakuwa na sukari ya kutosha katika hifadhi yao, kwani wazalishaji wamepunguza uzalishaji, wakitolea mfano wa wazalishaji wawili ambao walikuwa na tani 9,000 tu kila mmoja, ikiwa ni jumla ya tani 18,000.

Lakini, jana Bw. Baissac alisema kiwanda hicho kina tani 16,000 za sukari kwenye hifadhi yake na wanaiuza kwa yeyote anayetaka bila kizuizi wala vikwazo, kwa bei ambayo baada ya gharama zote zinawezesha sulari kuuzwa sh 1, 550.

Imeelezwa kuwa wasambazaji walimwambia waziri mkuu kuwa mahitaji ya sukari kwa mwezi ni tani 30,000, na wakaongeza kuwa sukari iliyokuwepo wakati ule ingeweza 'kuisukuma' nchi kwa 'wiki mbili tu', baada ya hapo nchi nzima ingeingia kwenye ukosefu kabisa wa bidhaa hiyo. 
Lakini uhalisia uliobainika baadaye ilikuwa ni kwamba sukari iliyokuwepo yaani tani 61,050 ingeweza kutosha kwa miezi miwili (Machi na Aprili).

Pamoja na kupewa ruhusa ya kuagiza tani 12,500 kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kama sehemu ya tani 50,000 kutoka nje ya nchi kuondoa upungufu, vyanzo vimesema kuwa mpaka sasa wasambazaji wameagiza tani 1,200 pekee, hivyo kufanya hoja yao kuwa hawakuwa na sukari iwe hafifu, bali walikuwa nayo wakiihodhi.
Mtindo huo wa wafanyabishara kuhodhi bidhaa ili kujinufaisha wakati wa uhaba, ulielezwa na Dkt. Chami katika tamko lake, akisema kuwa unasukumwa na nguvu mbili, moja ikiwa ni kutaka kujinufaisha kwa bei ya juu zaidi siku za usoni kadri bidhaa husika inavyokosekana.

Akisema kuwa mtindo huo ni sehemu ya soko, aliongeza kuwa nguvu ya pili inayowasukuma wafanyabiashara hao kuhodhi bidhaa ni kutaka kujilinda dhidi ya 'wapinzani' wao sokoni, kwani mfanyabiashara akiishiwa bidhaa ilhali mshindani wake anayo, unaweza kuwa mwanzo wa kuondolewa sokoni huku pia wakinufaika na bei kubwa.

No comments:

Post a Comment